Raymond Minja, Iringa
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Asas ameahidi kuwalipia ada kwa miaka minne wanafunzi 10 wanaotoka katika mazingira magumu wanaosoma kwenye shule ya sekondari ya Bread of Life iliyoko nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.
Asas ambaye amejinasibu kuwa ni mdau wa maendeleo ya elimu mkoani hapa amesema hayo katika mahafali ya shule hiyo na kuongeza kuwa nia ni kumpunguzia mzigo kwa kuchukua wanafunzi na kuwalipia ada kwa miaka minne kila mmoja kama juhudi za kuendelea kuchangia elimu mkoani hapa.
“Mzigo mkubwa alio nao mkurugenzi wa shule hii ni mkubwa mno hivyo hana budi kushikwa mkono kwani kila kukicha nimekuwa nikimuona akihangaika kuwasaidia na kuwajali watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu.
“Huyu bwana ni mtu mweye roho ya aina yake sijawahi kuona mtu mwenye roho ya pekee kama huyu, yaani amekuwa akihangaika huku na huko kuhakikisha hawa watoto hawa wanapata elimu nzuri kama wanavyopata watoto wake,” amesema.
Aidha, Asas amesema ni watu wachache sana wenye moyo kama mchungaji huyo kwani ni wachache sana wanaoamua kurudisha kile kidogo walichobarikiwa kwa watu wasio na uhitaji huku akiahidi kuendele kushirikiana na shule hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo .
Hata hivyo, Asas aliwataka wanafunzi waliomaliza kidato ha nne waende kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo na wakailinde nidhamu na heshima waliyopata katika shule hiyo ili waweze kufikia malengo waliyokusudia na kuja kuwasaidi wengine wakiwamo wazazi na walezi wao.