Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
TIMU ya Simba imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi wa Wekundu hao unaweza kuwa faraja kwa mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye Oktoba 11 alikumbwa na mkasa wa kutekwa na watu wasiojulikana waliomshikilia kwa siku tisa kabla ya kumwachia huru alfajiri ya Jumamosi iliyopita.
Mabao ya Simba yalifungwa na Clatous Chama dakika ya 30, Emmanuel Okwi dakika ya 45, huku bao la tatu likiwa la kujifunga la beki wa Stand, Eric Mulilo, dakika ya 77.
Ushindi huo uliifanya Simba kufikisha pointi 17 na kupaa hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, baada ya kucheza michezo nane, ikishinda mitano, sare mbili na kupoteza mmoja.
Mchezo huo ulianza kwa kasi na hasa  Simba kusukuma mashambulizi kuelekea kwa wapinzani wao kwa lengo la kutafuta bao la mapema, huku Stand United ikianza taratibu kwa kuisoma Simba.
Dakika ya tatu, mkwaju wa Meddie Kagere, ulipanguliwa na kipa wa Stand, Mohamed Makaka na kuzaa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.
Dakika ya nane, Kagere alipoteza nafasi ya wazi ambayo angeweza kuiandikia Simba bao la kuongoza Simba kama angekuwa makini baada ya kupokea pande safi ya Mohamed Ibrahim, lakini kiki yake ilikwenda nje.
Dakika ya 10, Hafidh Mussa wa Stand United, aliipenya ngome ya Simba kabla ya kuachia mkwaju uliopaa juu ya lango la Simba.
Dakika ya 24, Shiza Kichuya, alipoteza nafasi ya kuiandikia bao Simba, baada ya kupokea pasi safi ya Clatous Chama na kupiga shuti lililokwenda nje ya lango la Stand United.
Dakika ya 30, Chama aliiandikia Simba bao la kuongoza baada ya kupokea mpira wa Mohamed Ibrahim kisha kuwahadaa mabeki wa Stand na kuachia mkwaju  uliomshinda Makaka.
Dakika ya 35, Kocha wa Stand United, Niyongabo Amars, alifanya mabadiliko akimtoa Juvenary Pastory na kumwingiza Chinonso Charles.
Dakika ya 43, kipa wa Simba, Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada kupangua shuti lililopigwa na Kitenge na kuzaa kona ambayo hata hivyo haikubadili matokeo.
Kabla ya mapumziko, Okwi aliiandikia Simba bao la pili dakika ya 45 baada ya kupokea pasi ya Chama na kumchambua Makaka.
Dakika ya 64, Kocha wa Simba, Patrick Aussems, alifanya mabadiliko, alimtoa Mohamed Ibrahim na kumwingiza, Hassan Dilunga.
Dakika ya 70, Hafidh Mussa, nusura aipatie bao Stand United baada ya kuachia shuti kali la mbali, lakini Manula alipangua na kuzaa kona ambayo haikuwa na faida.
Dakika ya 74, Stand ilifanya mabadiliko alitoka Chinonso Charles na kuingia Jisend Mathias.
Dakika ya 77, beki Erick Mulilo wa Stand, alijikuta kwenye majonzi baada ya kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira, hivyo kuizawadia Simba bao la tatu.
Dakika ya 81, Simba ilifanya mabadiliko mengine, alitoka Kichuya na kuingia Marcel Kaheza.
Dakika ya 87, Simba ilifanya mabadiliko, alitoka Kagere na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Salamba.
Pamoja na mabadiliko hayo, dakika 90 za pambano hilo zilimalizika kwa Simba kuondoka na ushindi wa mabao 3-0.
Ligi hiyo iliendelea pia maeneo mengine ya nchi, Lipuli FC ilishindwa kutamba nyumbani baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar, mchezo uliochezwa Uwanja wa Samora, Iringa.
Bao pekee la Kagera Sugar lilifungwa na Selemani Mangoma dakika ya 61.
Mbao FC ilitakata baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Bao lililoipa pointi tatu Mbao katika mchezo huo lilifungwa na Said Khamis dakika ya 48.