NA DK. CHRIS MAUKI
MARA nyingi ni kitu kinachoonekana hakiwezekani na ni kigumu kwa wengi. Ugumu huu si tu kwa watu wa maisha ya chini bali hata kwa wenye vipato vikubwa, watu wa nchi zinazoendelea na nchi zilizoendelea.
Wote bado inatuwia vigumu kuweka uwiano wa kazi tunazozifanya na maisha mengine. Hapa kazi namaanisha majukumu yako ya kila siku, kazini kwako, kwenye biashara zako au kokote ulikojiajiri mwenyewe.
Je, unawezaje kuweka uwiano wa maisha yako ya kazi na maisha mengine kama vile maisha ya kijamii, kuwaona na kuwatembelea ndugu, kuwa na muda na familia, kushiriki ibada, kushiriki michezo, kupumzika au hata kuwa na nyakati za likizo “holidays” na familia yako?
Bado kuna mvutano na mjadala mkubwa kwenye hili suala la kuwa na uwiano mzuri kwenye kazi na maisha mengine, wapo wanaosema hakuna haja ya kuwa na uwiano mzuri kama kweli unapenda unachokifanya, kama kweli unaipenda kazi yako basi komaa nayo na kama unaipenda familia yako zaidi basi kuwa nayo zaidi. Wengine wanasema haiwezekani ukaweka uwiano wakati una ndoto zako unazikimbiza na unataka zote zitimie. Wengine wanasema kama una vitu umepanga kuvifanya kabla haujafa ili uviache kwenye ulimwengu na kuweza kukumbukwa kwavyo basi ni ngumu sana kusema eti uwe na uwiano wa kile unachofanya na maisha mengine. Pamoja na ukweli wa yote yanayopendekezwa katika mijadala hii, bado ukweli unabaki pale pale kwamba wapo waliokimbizana na ndoto zao, wapo waliokimbizana kutimiza majukumu yao ili waache majina makubwa yanayokumbukwa duniani lakini mashinikizo na misongo ya mawazo ya majukumu hayo hayakuwaruhusu kusimama, wengine wamepata matatizo ya moyo, wengine mashinikizo ya damu na wengine magonjwa ya sonona “depression”.
Hii inatuonyesha kwamba kuweka uwiano mzuri wa majukumu yetu ya kila siku na maisha mengine ni jambo la muhimu sana na lisiloepukika. Tunahitaji kile mfanyabiashara na mwandi- shi maarufu, Nigel Marsh, anachokiita eneo la katikati “middle ground” ambalo tunaweza kuikusanya furaha ya kazini kwetu na furaha ya kutoka maeneo mengine ya maisha, ili kuepuka kuwa na furaha iliyoegemea upande mmoja tu na kupungua pande nyingine.
Je, tunafikiaje eneo hili? Au tunafanikiwaje katika hili?
1. Tenga muda maalumu wa vitu vinavyokupa furaha Kama wanavyosema wachumi kwamba kama ukiamua kuwalipa fedha wengine kwanza ili itakayobaki iwe ya kwako basi ujue hakuna itakayobaki kwa ajili yako, lakini kama ukianza kwanza kuhifadhi inayokuhusu utakuta fedha ya kumalizana
na wengine inapatikana. Vivyo hivyo kwenye maisha mengine, ukisema utumie muda kwanza kwa mambo yanayowahusu wengine, yanayohusu ofisi au kazi au biashara yako na labda siku moja utapata muda wako wa kupumzika, nataka nikuahidi kwamba muda huo kamwe hautatokea maana kila siku kitaibuka kitu chakufanya na cha kukuweka bize. Anza kwa kuutenga muda huo kwanza, ruhusu akili yako iufahamu muda huo na kuuheshimu. Muda ambao utafanya vile vitu ambavyo nafsi yako inavikubali sana, inavipenda na kuvifurahia. Vitu hivi vinavyopangwa kwenye muda wa kuitafuta furaha yako binafsi ni pamoja na muda wa mazoezi, kupata kahawa na marafiki jioni, muda wa kusoma kitabu unachokipenda, chakula cha mchana na rafiki, au kupata muda wa kuoga pekeyako kwafuraha nk.
2. Punguza au epukana na vitu vinavyokuongezea mizigo, ongeza vile vinavyokupunguzia mizigo
Viko vitu vingi sana tunajihusisha navyo pasipo kujiuliza au kuvitathmini kwa kina, hatu-
pati muda wakujiuliza kama vitu hivyo ni vya msaada kwetu au vinatuongezea hasara, hatuchunguzi kama vitu hivyo vinatuongezea au kutupunguzia mizigo. Mwanasaikolojia mkongwe Marilyn PuderYork anashauri kila mtu kuweza kujitathmini kama vitu anavyofanya vinamwongezea thamani au vinampunguzia thamani hata kama ni kidogokidogo na kwa muda mrefu. Unaweza kuwa hauoni kwamaana hasara, mzigo au kupunguziwa thamani kunakoletwa na vitu hivi hakutokei ghafla bali taratibu na ukija kugundua ni hatari kubwa. Kwamfano; umeshawahi kutathmini faida au hasara ya kukaa kazini kwa muda mrefu, tena hadi usiku na kuchelewa kurudi nyumbani?, kusikiliza umbea, kupoteza muda kwenye mitandao ya kijamii, au kukaa muda mrefu ukiongea na simu. Vitu hivi hupunguza ufanisi wetu pasipo sisi kujua. Kwa kuamua kujitathmini na kubadili namna tunavyofanya mambo itatusaidia kuhakikisha tunafanya kazi kwa umakini mkubwa, tunamaliza majukumu yetu haraka, tunatoka ofisini au makazini kwetu haraka na kupata muda wa kufanya yale mambo tunayoyafurahia.