25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

JAMAL KHASHOGGI: Mwandishi anayezigombanisha Saudia, Uturuki na Marekani

LONDON, UINGEREZA


JESHI la Polisi nchini Uturuki linalochunguza tuhuma za mauaji ya mwandishi habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi, limepanua wigo wa uchunguzi ili kuwezesha kupatikana taarifa za kutosha juu ya kadhia nzima iliyotokea kabla na baada ya kutoweka kwake.

Maofisa wa Uturuki ambao hawajatajwa wanasema mwili wake huenda umetupwa katika msitu ulio karibu au katika shamba.

Khashoggi alitoweka baada ya kuingia katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul mnamo Oktoba 2 mwaka huu, sehemu ambayo maofisa wa Uturuki wanatuhumu aliuawa kabla ya kutupwa eneo jingine.

Kwa upande wao, Mamlaka ya Saudi Arabia inakana kuwa na ufahamu wowote wa kilichomkabili na kujitakasa kuwa haihusiki na tukio hilo baya ambalo linavuruga uhusiano wa nchi hizo mbili pamoja na washirika wao.

Sampuli zilizochukuliwa kutoka ubalozi na makazi ya balozi wakati wa upekuzi wiki hii zinafanyiwa majaribio kwa kulinganishwa na chembechembe za vinasaba (DNA) kama ni vya Khashoggi.

Uturuki imewahi kusema ina ushahidi wa kanda ya sauti na video ya mauaji ya Khashoggi, lakini hazijafichuliwa wazi hadi leo, licha ya Marekani kuitaka Uturuki itoe ushahidi huo hadharani.

Mkasa huu umesababisha mvutano mkubwa kati ya Riyadh na washirika wake wa mataifa ya magharibi, ikiwamo Marekani.

Jamal Khashoggi ni nani?

Jamal Khashoggi ni mwandishi maarufu aliyechambua masuala mbalimbali kwa mashirika tofauti nchini Saudia. Alipata elimu ya msingi na sekondari nchini Saudi Arabia, kisha shahada ya kwanza katika masomo ya usimamizi wa biashara alipata katika Chuo Kikuu cha Indiana nchini Marekani.

Alizaliwa Oktoba 13, 1958 mjini Medina. Babu yake, Muhammad Khashoggi, alikuwa na asili ya Uturuki aliyeoa mwanamke wa Saudi Arabia.

Aidha, Muhammad Khashoggi alikuwa mkufunzi binafsi wa viungo wa Mfalme Abdulaziz Al Saud, ambaye ndiye mwanzilishi wa dola ya Saudi Arabia.

Jamal Khashoggi na Dodi Fayed (mtoto wa Mohamed al Fayed) ni mtu na binamu yake. Dodi ndiye aliyekutwa na mauti akiwa kwenye uhusiano mzito wa kimapenzi na Princess Diana wa United Kingdom kule jijini Paris nchini Ufaransa.

Aliunda urafiki na Osama bin Laden katika miaka yake ya kwanza alipoanza kuwa mwandishi wa habari na alifahamika kama mzaliwa maarufu wa Saudia aliyelazimika kutoroka nchi hiyo.

Kabla ya kutoweka kwake katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Khashoggi alilazimika kuishi baina ya nchi za Marekani, Uingereza na Uturuki.

Aliondoka Saudi Arabia Septemba mwaka jana, baada ya kukosana na maofisa katika ufalme wa nchi hiyo. Akiwa uhamishoni, alikuwa akiandikia gazeti la Washington Post la Marekani ambako makala zake nyingi zilikosoa utawala wa Saudia, na pia katika akunti yake ya Twitter ambako alikuwa na wafuasi zaidi ya milioni 1.6 aliendeleza ukosoaji huo.

Alipokuwa akifanya kazi katika gazeti la al-Madina katika miaka ya 1990, aliandika pakubwa kuhusu wanamgambo wa Kiislamu nchini Afghanistan waliokwenda kupigana katika uvamizi wa Usovieti.

Alifanya mahojiano mengi tu na raia wa Saudia, Osama bin Laden, ambaye anaarifiwa kumfahamu tangu ujana wake nchini Saudi Arabia. Bin Laden kwa wakati huo alikuwa bado hajakuwa mtu anayefahamika sana katika mataifa ya magharibi kama kiongozi wa kundi la al-Qaeda.

Khashoggi alimtembelea katika mapango kwenye milima ya Tora Bora, na pia aliwahi kumhoji nchini Sudan pia mnamo 1995.

Khashoggi mwenyewe aliwahi kuhojiwa na gazeti la Ujerumani, Der Spiegel mnamo mwaka 2011 kuhusu uhusiano wake na Osama bin Laden.

Khashoggi alikiri kwamba anakubaliana na mitazamo ya bin Laden katika siku za nyuma kuhusu kutumia mbinu zisizo za kidemokrasia kama kupenya katika mfumo wa kisiasa au kutumia mbinu za ghasia kuziondosha tawala fisadi katika mataifa ya Kiarabu.

Lakini tangu hapo, Mwandishi huyo aligeuka kuwa mojawapo ya watu waliozungumza wazi kuhusu maendeleo ya nchi hiyo, aliyenukuliwa na vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi kama mtaalamu kuhusu masuala ya itikadi kali katika dini ya Kiislamu.

Alionekana kama mtu aliye karibu na watawala wa Saudia, aliyekutana mara kwa mara na familia ya ufalme nchini humo.

Alishikilia nyadhifa tofuati na alifanya kazi na vituo kadhaa vya TV akianza kama mwandishi wa masuala ya nje ya nchi, hadi kuwa mhariri mkuu.

Kituo cha Al-Arab kilionekana kuwa mpinzani kwa shirika la utangazaji la Al-Jazeera, linalofadhiliwa na Qatar. Lakini muda mfupi baada ya kuzinduliwa, kituo hicho cha televisheni kilichokuwa chini ya usimamizi wa Khashoggi kilifungwa kwa kupeperusha mahojiano na kiongozi wa upinzani wa Bahraini.

Khashoggi kwa wakati huo pia alikuwa akihojiwa na vyombo vya habari vya mataifa ya nje, akishutumu ufalme wa Saudi Arabia, akieleza kwamba kuna haja ya kuwa na mfumo wa kidemokrasia kuhakikisha utulivu wa nchi hiyo katika miaka ijayo.

Wakati maandamano katika nchi za Kiarabu yalipoanza kudai mabadiliko ya uongozi, Khashoggi alikubaliana na upinzani uliotaka mabadiliko nchini Misri na Tunisia.

Msimamo wake ulikuwa kinyume na sera rasmi ya ufalme wa Saudia, uliotazama maandamano hayo kama tishio kwa uwepo wake.

Mnamo Desemba 2016, wakati Mwanamfalme wa Saudia alipokuwa akijenga uhusiano na Rais mpya wa Marekani, Donald Trump, Khashoggi anaarifiwa kushutumu uhusiano huo.

Vyombo vya habari Arabuni vinaashiria uandishi wake kuhusu suala hilo ulipigwa marufuku kwa sababu hii. Khashoggi pia alikosoa uamuzi wa Serikali ya Saudia kuvunja uhusiano na Qatar, akiuomba Ufalme ushirikiane na Uturuki kuhusu masuala ya ukanda, nchi ambayo ni mshirika wa karibu na Qatar.

Mwandishi huyo wa zamani aliondoka Marekani mnamo Septemba 2017, akimshutumu kiongozi wa kudumu wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Mohammed bin Salman, kwa kulenga upinzani.

“Nimeondoka nyumbani kwangu, nimeiacha familia yangu na kazi yangu na ninapaza sauti yangu. Kufanya jambo jingine lolote itakuwa ni kuwasaliti wanaoteseka gerezani. Naweza kuzungumza wakati wengi hawawezi. Naweza kusema Mohammed bin Salman anajifanya kama Putin. anatenda haki kibaguzi,” aliandika katika makala yake kwenye gazeti la Washington Post.

Aliendelea na shutuma zake dhidi ya kiongozi wa Saudia hadi alipoingia katika ubalozi huo mjini Istanbul. Ndio mara ya mwisho alipoonekana.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika ya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles