25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkanda wa sauti wadaiwa kufichua namna Khashoggi alivyouawa  

ISTANBUL, UTURUKI

MKANDA wa sauti uliorekodi dakika za mwisho za uhai wa mwandishi wa habari raia wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi, unadaiwa kufichua namna alivyouawa katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini hapa Oktoba 2 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Gazeti la Middle East Eye (MEE), mkosoaji huyo mkubwa wa Saudia aliburuzwa kutoka ofisi ya Balozi Mdogo wa Saudi Arabia, Mohammed al Otaibi kwenda katika meza ya chumba jirani cha kujisomea.

Kuwapo  ushahidi kuwa Khashoggi, ambaye pia ana asili ya Uturuki aliuawa, kulifichuliwa mapema na wachunguzi wa Uturuki

MEE linasema sauti ya Balozi al Otaibi mwenyewe inasikika katika kanda hiyo iliyonasa kifo cha Khashoggi.

Chanzo kimoja cha habari chenye uhusiano wa karibu na serikali kilimnukuu balozi huyo akidai kuwa Saudi Arabia ilituma majasusi  Istanbul: ‘Msiseme hili. Mtanitia mashakani.’

Otaibi alirejea   Riyadh Jumanne wiki hii.

Sauti za mkoromo wa kutisha zilisikika, kwa mujibu ya walioshuhudia waliokuwa kwenye chumba vya chini, chanzo cha habari kimesema.

“Balozi mdogo mwenyewe aliondolewa kutoka chumba hicho. Hakukuwa na jaribio la kumhoji. Walikuja kumuua,” chanzo hicho kililiambia MEE.

Sauti   zenye kelele ya kuogofya zilisimama wakati Khashoggi, ambaye mara ya mwisho alionekana akiingia katika ubalozi huyo Oktoba 2, alipochomwa sindano yenye kimiminika kisichofahamika.

Salah Muhammad al-Tubaigy, ambaye ametambuliwa kama mkuu wa kitengo cha Ushahidi wa Alama za Vidole, Idara ya Usalama wa Jumla Saudi Arabia, ameelezwa kuwa mmoja wa kikosi cha watu 15, walioingia Ankara mapema siku hiyo kwa ndege binafsi.

Magari kadhaa ya Saudi Arabia yenye nambari ya usajili ya diplomasia yalinaswa kwenye kamera za usalama za CCTV yakiingia ubalozini chini ya saa mbili baada ya  Khashoggi kuingia humo siku hiyo.

Tubaigy anadaiwa alianza kuukata mwili wa Khashoggi ukiwa mezani wakati akiwa bado hai, chanzo hicho kilidai.

Mauaji hayo yalichukua dakika saba, chanzo hicho kilisema.

Wakati akianza kuukata kata mwili, Tubaigy aliweka spika ya masikio ‘earphones’ masikioni na kusikiliza muziki. Aliwashauri wenzake kumuiga.

“Wakati nikifanya kazi hii, huwa nasikiliza muziki. Nanyi mnapaswa kufanya hivi pia,” Tubaigy alirekodiwa akisema, kwa mujibu wa chanzo hicho kwa MEE.

Sehemu ya mkanda huo ilipatiwa gazeti la Sabah la hapa ambalo bado halijautoa.

Chanzo hicho cha habari pia kililiambia gazeti la New York Times kuwa Tubaigy alikuwa ameshikilia msumeno wa kukatia mifupa.

Maofisa wa Saudi Arabia wamekana vikali kuhusika na kutoweka mwandishi huyo wakidai aliondoka ubalozini hapo kwa mlango wa nyuma muda mfupi tu baada ya kuwasili.

Hata hivyo, wameshindwa kutoa ushahidi kuunga mkono madai yao na wanadai kuwa kamera za video hazikuwa zikirekodi wakati huo.

Jumanne baada ya awali kuionya Saudi Arabia, Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo walijitokeza kuikingia kifua Saudi Arabia, mshirika wao muhimu Mashariki ya Kati.

Kutokana na sababu hiyo, kupotea kwa Khashoggi kumeuweka utawala huo katika hali ya kutatanisha.

Lakini akizungumzia mkanda huo, Trump alisema hawezi kuamini hadi watakapopatiwa na kuuchunguza.

Trump alidai kuzungumza na Mrithi wa Ufalme, Prince Mohammed bin Salman na amekana kufahamu tukio hilo.

Akiendelea kuutetea ufalme huo, Trump alisema amehakikishiwa kutakuwa na uchunguzi wa kina na wa haraka kuhusu suala hilo.

Rais Trump aliwaambia wanahabari Ikulu ya Marekani  kuwa, “Tumeomba kupatiwa nakala ya kanda hiyo, kama kweli ipo.”

 

Akigusia sauti iliyorekodiwa na ambayo inadaiwa kuwa na ushahidi wa mauaji ya Khashoggi, Trump aliongeza: “Sina uhakika wa kuwapo   sauti hiyo, lakini huenda ni kweli ipo.”

Trump alisema anatarajia ripoti kutoka kwa Waziri wake, Pompeo ambaye alikuwa   Saudi Arabia na Uturuki.

Rais Trump alisema ukweli kuhusu suala hilo utajulikana kufikia mwisho wa wiki.

Jumatatu iliyopita, Televisheni ya  Marekani ya CNN liliripoti kuwa maofisa wa Saudi Arabia wanajiandaa kutoa ripoti itakayoonesha kifo cha Khashoggi kilitokana na mahojiano ya uchunguzi yaliyoenda mrama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles