29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Stigler’s chakula kilicho mezani tusihofie kupaliwa Pilipili

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

MWAKA 1982 na kabla ya hapo, hata pale Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lilipotoa hadhi ya kuwa urithi wa dunia kwa Pori la Akiba la Selous tayari kulishakuwapo andiko la kutekeleza mradi wa umeme.

Selous ina Kilometa za Mraba 50,000, huku eneo la mradi Stigler’s Gorge kunakojengwa mradi wa umeme kukikadiriwa kuchukua Kilometa za Mraba 1,800 sawa na asilimia nne ya eneo lote.

Mradi huo mkubwa wa kitaifa utakaozalishaji umeme kwa kutumia maporomoko ya maji unatazamiwa kuzalisha kiasi cha Megawati 2,100 zitakazo wezesha nchi kuimarika kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji wa aina mbalimbali.  Kwa kufanikisha hilo nchi itakuwa na umeme wa kiasi cha mara mbili ya uliopo sasa na hivyo kufikiria kuuza mwingine nje.

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), ndio yenye dhamana ya kusimamia mapori ya Akiba, Tengefu, oevu na mengineyo kwa kuhakikisha rasilimali zilizo kwenye maeneo hayo zinalindwa na kutunzwa.

Ni wazi kwamba utekelezaji mradi wa umeme wa Stigler’s upo ndani ya eneo la kiuhifadhi, yaani Pori la Akiba Selous ambalo kwa miaka mingi limeainishwa kuwa eneo la urithi wa dunia. Hii pia ni heshima kwetu ila sasa tunaifanyia marekebisho kwa mahitaji mapana zaidi ya Taifa.

Akizungumzia utekelezwaji wa mradi huo katika eneo la kiuhifadhi, Mkurugenzi Mkuu TAWA, Dk. James Wakibara anasema, mradi huo mkubwa kwa taifa unategemewa kuleta mabadiliko zaidi katika uchumi.

“Huu ni uamuzi sahihi kwa serikali hasa ikichukuliwa ulibuniwa miaka mingi iliyopita si suala jipya tunaloweza kusema limeshituliwa, lilikuwapo miaka mingi.” Isitoshe lilikwisha kuanza kufanyiwa kazi na sasa ni mwendelezo tu baada ya kupata uwezo na haja kujidhihirisha zaidi.

“Faida za umeme kwa nchi zinaeleweka kinachofanyiwa kazi ni umeme kuzalishwa bila kuleta madhara makubwa katika mazingira na si kuundoa mradi.

“ Tumeendelea kuzungumza na jamii ya kimataifa na kuielimisha kwani si kitu cha ajabu kufanyika kwetu, yapo maeneo mengi yenye urithi wa dunia kumefanyika miradi kama hii,” anasema Dk. Wakibara na kuongeza:

“Mengine tayari yametekeleza miradi kama huu kwa hiyo kinachozungumzwa hapa si kutokufanya bali ni jinsi gani ya kufanya ili faida zipatikane bila kuleta athari kubwa kwa mazingira,” anasema.

Akifafanuza kiuhifadhi anasema, katika masuala ya uhifadhi hawaongelei kutokufanya kitu, bali kukifanya kwa utaratibu ambao athari zake zitakuwa ndogo kiasi cha kutosababisha mradi kukwama.

“Na hiyo ndio maana ya tathimini ya athari kwa mazingira, si kuzuia bali kufanya katika namna itakayosababisha mradi kuwapo bila kuathiri mazingira kwa kiwango ambacho kita athiri tena mradi husika,” alisema.

“Tathimini imefanyika kwa weledi taarifa imetolewa na kupelekwa vyombo vya UNESCO mazungumzo yanaendelea wametuelewa,” anasema Dk. Wakibara.

Mdau wa mazingira aliyefanya kazi TANESCO Kidatu, na kushiriki uanzishwaji mradi huo Benson Kibonde anasema, maendeleo duniani yamejikita katika kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji nishati wa kutosha.

Akiwa ndiye Mratibu shughuli za uwindaji wa kitalii Kampuni ya Mkwawa  Hunting Safari iliyowekeza Pori la Akiba Selous, Kibonde anasema, taifa linalotaka kuendelea lazima lihakikishe suala nishati linakuwa la uhakika.

“Naamini wazo la kuendeleza shughuli za umeme Stiegler’s Gorge si la leo. Tunaangalia fursa ya kutoa nishati, taifa lina fursa nyingi na Tanzania inasemekana ni nchi ya tano kuwa na rasilimali za kuzalisha umeme barani Afrika.

“Rasilimali kubwa kwetu ni maji kwa maana ya maporomoko yanayoweza kusaidia uzalishaji umeme. Na umeme unaotokana na maji rahisi zaidi kuliko vyanzo vingine,”

“Gridi ya taifa hupokea umeme kutoka vyanzo mbalimbali lakini umeme kutoka kwenye maji ndio  rahisi  kuliko na hivyo unapoza bei za umeme kwa wananchi.

“Huwezi kuzungumza viwanda bila nishati na huwezi kuzungumzia nishati bila ya maji, unaweza kuzungumzia nishati kutokana na gesi lakini gesi ni ghali zaidi na mara nyingi huisha kama  rasilimali,” anasema Kibonde na kuongeza:

“Kwa ufahamu wangu mdogo vitalu vingi vya gesi vimegawiwa kwa Kampuni za kimataifa, havipo kwenye umiliki wa serikali, baadaye huenda vikagharimu taifa kwa kuongeza bei ya umeme,” alisema.

Akielezea kuhusu hofu ya kuwapo athari za kimazingira katika mradi huo Kibonde anasema,maendeleo yeyote yanapofanyika duniani huwa hayawezi kukosa athari. Wafaransa wanasema kuwezi kutengeneza omleti bila kuvunja yai.

“Kitaalamu tunazungumzia athari kuwapo, lakini na juhudi za kupunguza athari hizo, nini kifanyike ndio maana inatakiwa tuseme kitu ambacho kitaathiriwa na taifa litafanya nini kupunguza athari hizo.

Eneo la mradi la Kilometa za mraba 1,800 ni sehemu ndogo sana, zipo nchi zilizoendelea zimefanya miradi ya nishati ya maji kwa kuzingatia ushauri wa kimazingira.Haya mambo tunaamini taifa halijakurupuka linafanyia kazi.

“Hatuwezi kuogopa kula chakula kilicho mezani kwa kuhofia kupaliwa na Pilipili, hili ni suala dogo sana tena la mpito,” anasema Kibonde.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko anasema, kazi kubwa waliyonayo mbali ya kutunza vivutio vya utalii wanalojukumu pia la kulinda vyanzo vikubwa vya maji.

“Tuna mradi mkubwa wa umeme ili ufanikiwe ni lazima vyanzo vyote vya maji yanayopelekwa maporomoko ya Stigler’s Gorge lazima vitunzwe vizuri,” anasema Meja Jenerali Mstaafu Semfuko.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kata ya Msolwa Station wilayani Kilombero mkoani Morogoro wanaoishi jirani na Pori la Akiba Selous wanasema kwa sasa wameanza kunufaika na uwekezaji katika maeneo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wake Diwani wa Kata hiyo Hakimu Songa asema kwa sasa wamekuwa na ushirikiano katika masuala ya maendeleo kwa wananchi.

“Jukumu kwetu viongozi wa wananchi ni kuhakikisha tunatoa elimu kwa tunaowaongoza wajue umuhimu wa uhifadhi ili tuendelee kupata misaada inayotoka kwa wawekezaji wa vitalu vya uwindaji.

“Faida kubwa ambayo wananchi tunapaswa kuisubiria ni kuanza kuzalishwa umeme wa Stigler’s ambao sisi wananchi jirani na Pori la Akiba Selous itakuwa ni faida zaidi kwetu kufikiwa na maendeleo hayo,” anasema Songa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles