KAMPALA, Uganda
MWANAMKE mmoja nchini hapa, Lulu Jemimah ambaye hivi karibuni alitangaza kujioa, amekaribia kufikia malengo yake baada ya kupata nusu ya ada ya kujisomesha katika Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32, mbali na kutafuta ada, lengo lake kubwa lilikuwa ni kuionesha jamii yake kuwa inawezekana kufikia malengo kimaisha bila ya msaada wa mwanamume.
Mwanamke huyo anayesoma chuo maarufu cha Oxford, ili kumalizia mwaka wa pili wa masomo yake anahitaji pauni 10,194.
Alitumia ndoa yake hiyo, ambayo baadhi ya watu wanaiona kama kituko, kufanya kampeni mtandaoni ili kupata usaidizi wa kulipa ada hiyo.
Kampeni yake ambayo ina wiki ya pili sasa katika mtandao wa Go Fund Me, imeweza kufanikisha nusu ya malengo. Ameshakusanya pauni 5,122 kutoka kwa watu 96 sehemu mbalimbali duniani.
Katika mwaka wake wa mwanzo wa masomo, Jemimah alisema alikumbana na changamoto nyingi za kifedha zilizomfanya aishi katika mazingira magumu.
Alisema licha ya kuchangiwa na watu kadhaa, alishawahi kulala maktaba kutokana na kukosa pesa ya kodi ya chumba.
Jemimah alisema haikuwa dhamira yake kuomba msaada, lakini hofu ya kufutwa chuo kutokana na kukosa fedha imemlazimu afanye hivyo.
“Nimepata bahati ya kuwa katika chuo bora chenye wanafunzi makini na walimu wenye weledi mkubwa.
“Nimefikia hapa kutokana na msaada wa marafiki na watu nisiowafahamu. Kwa mara nyingine tena naomba msaada wenu,” alisema juzi mwanamke huyo.
Licha ya mafanikio ya kielimu kwa kujiunga na chuo maarufu duniani, alisema watu waliendelea kumuuliza swali moja ambalo kwa miaka kadhaa hakuwa analifurahia ambalo ni anapanga kuolewa lini, ili aanzishe familia na kupata watoto.
“Hawaamini kuwa kinachonifanya kuwa macho usiku sio hofu ya uwezekano wa kutopata bahati ya kutembea altareni kwenda kufunga ndoa.
“Nikiwa na miaka 16 baba yangu aliandika hotuba yake kwa ajili ya kuisoma siku ya harusi yangu. Kila nilipokuwa nasherehekea siku yangu ya kuzaliwa mama yangu alikuwa akiniombea na kwa miaka ya karibuni maombi yake yalikuwa pamoja na kupata mume bora, ambaye atanifaa,” alisema Jemimah.
Kutokana na hali hiyo, Jemimah alisema aliamua kuchukua uamuzi wa kuwatuliza baada ya kufikisha miaka 32 kwa kuamua kujioa.