25.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wakuu wa wilaya 70 matatani

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

RAIS John Magufuli amewashukia wakurugenzi na wakuu wa wilaya 64 ambao mbio za mwenge zimeanika matatizo kwenye mradi katika maeneo yao.

Inaelezwa kuwa  wengine watano   waliweka miradi hewa kwenye mbio za mwenge za mwaka jana.

Alikuwa akizungumza Ikulu  Dar es Salaam jana baada ya kupokea wakimbiza mwenge wa mwaka huu.

Rais Magufuli aliwataka wakurugenzi na wakuu wa wilaya hizo kutoa maelezo ya namna gani wanashughulikia miradi hiyo ili ikamilike.

Alisema endapo watashindwa kuweka mikakati ya kuhakikisha miradi hiyo inakamilika atawachukulia hatua kali.

“Katika wilaya 64 kuna baadhi ya miradi ambayo ni mibaya na ndiyo maana jana Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) alitoa maagizo kwamba wakuu wa wilaya wa miradi hiyo na wakurugenzi walete taarifa ni kwa namna gani wanashughulikia miradi ile.

“Wasipoeleza mikakati ya kuhakikisha miradi ile inakamilika nitachukua hatua na hatua zitakuwa kubwa.

“Kwa hiyo ni uhakika yale maagizo yako Waziri Mkuu uliyoyatoa wale wakuu wa wilaya na wakurugenzi wataeleza kwamba ni namna gani sasa ile miradi wanaitekeleza au wamepanga programu gani ya kuishughulikia ile miradi,” alisema Rais Magufuli.

Alitaka wakuu hao wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa mikoa hiyo kupewa taarifa kuwafahamisha ni miradi gani iko katika maeneo yao ambayo haijakamilika waweze kuweka mikakati ya kuikamilisha au kuitolea maelezo zaidi.

“Ninafahamu  baadhi ya wakuu wa wilaya ni wapya kabisa, wameingia kwenye maeneo ambayo wameanza hiyo kazi lakini najua kuna wakurugenzi ambao ni wapya tumewapeleka kule.

“Lakini upya wao au ukuukuu wao ni lazima washughulikie haya kwa sababu ndiyo wajibu wao,” alisema.

Miradi hewa

Dk. Magufuli pia aliwanyooshea kidole wakurugenzi na wakuu wa wilaya tano ambazo miradi yake ilizinduliwa wakati wa mbio za mwenge mwaka jana lakini mwaka huu miradi hiyo imebainika haipo.

Alisema mwaka jana ilizinduliwa miradi yenye thamani ya Sh bilioni moja ambayo baada ya mwenge huo kuipitia, mwaka huu imebainika baadhi haipo tena.

“Kwa utaratibu wa mwaka huu ambao waliuweka ndani ya wizara husika, wakimbiza mwenge wa mwaka huu waliipitia pia baadhi ya miradi kuicheki kama hiyo miradi bado ipo.

“Imegundulika kuna miradi mitano ambayo haipo, ilizinduliwa mwaka jana lakini wamepita mwaka huu haipo.

“Moja ni duka la dawa Bariadi na jingine sijui ni nini. Hili nataka wakuu wa wilaya hizi wajieleze vizuri, hii maana yake hawasimamii vizuri hiyo miradi iliyozinduliwa.

“Kwa mfano Bariadi duka la madawa walipomaliza kulizindua kulikuwa na madawa yote halafu wamerudi hakuna kitu,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema kutokuwapo kwa miradi hiyo kunaonyesha miradi hiyo iliandaliwa kwa ajili ya maonyesho wakati wa mbio za mwenge wa uhuru na baada ya kuzinduliwa ikatoweka.

“Kwa hiyo baada ya kufungua yale maduka yakaondoka, kwa hiyo yalikuwa ni kama show (maonyesho) ya mwenge mwaka jana walipopita wakute duka limejaa pale hospitali lakini baadaye is nothing (hakuna kitu).

“Sasa yale maelezo ya kina Waziri Mkuu lazima watoe, kwnini wanadanganya mwenge, kwnini wanamdanganya Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) ambaye ni kiini na mwanzilishi halali wa mwenge huu wa taifa, ambao madhumuni yake hayawezi mtu yeyote anaya-undermine,” alisema Dk. Magufuli.

Naye Majaliwa, alisema tayari amewapatia taarifa wakurugenzi na wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wanakamilishwa miradi hiyo na kuchukua hatua kwa miradi yote ambayo haiendani na thamani ya fedha iliyotumika.

“Nimewapa siku 10 hadi kufikia Oktoba 25, taarifa hiyo iwe imekwisha kufika Ofisi ya Rais Tamisemi ambayo itafanya majumuisho ya miradi yote na wataileta kwetu ili tuone hatua zilizochukuliwa.

“Muhimu zaidi ni miradi iliyolengwa kutekelezwa iweze kukamilika  wananchi waweze kutumia fursa za miradi hiyo,” alisema Majaliwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, alisema katika mbio hizo, miradi 1,432 yenye thamani ya Sh bilioni 660.6 ilizinduliwa, kufunguliwa na kuwekwa mawe ya msingi, huku miradi 80 iliyopo katika halmashauri 64 ikikutwa na dosari mbalimbali.

Mhagama alisema dosari hizo ni pamoja na ubora hafifu wa miradi na kukosekana kwa uhalisia wa thamani ya mradi.

Alisema pia ilikaguliwa miradi 94 iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka jana na kubaini miradi mitano  kati yake haifanyi kazi.

“Rais tumeamua kuboresha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kuwatumia wakimbiza Mwenge kubaini ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma katika miradi na kuchukua hatua wakiwa hukohuko kwenye miradi,” alisema Mhagama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles