Na Eliya Mbonea, Arusha
WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya Salum, amepatwa na mshtuko baada ya kusikika kwa milipuko mitatu ya mabomu ya kutoa machozi jirani na Hoteli ya Naura Spring, jijini hapa.
Waziri Mkuya alikuwa jijini hapa akifungua mkutano wa wadau wa Taasisi za mapato za nchi za Afrika uliowajumuisha wadau, wataalamu na wawekezaji wakubwa katika gesi, mafuta na madini.
Akiwa tayari amejiandaa kufanya mahojiano na waandishi wa habari, ghafla milipuko miwili ilisikika, kisha ukafuata mlipuko mwingine uliosababisha Waziri Mkuya kusita kidogo kuendelea kuzungumza.
“Heee! Jamani hii nini tena, kuna usalama? Huu mji vipi, unajua msichukulie vitu kirahisi, hii ni kawaida?” alihoji Waziri Mkuya.
Taharuki hiyo ya milipuko ya mabomu imekuwa ikilikumba Jiji la Arusha hasa katika mikusanyiko ya watu ambayo imesababisha vifo pamoja na majeruhi.
MTANZANIA lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas kuzungumzia milipuko hiyo iliyosikika katika eneo la nyumba za askari polisi, hakuweza kupatikana kwa simu yake ya mkononi.
Akizungumzia mkutano huo, Waziri Mkuya alisema umelenga kuwapa fursa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ili wajifunze na kubadilishana uzoefu wa kukusanya mapato kutoka nchi za Afrika zilizoanza kuchimba gesi na mafuta.
Alisema wataalamu hao na wawekezaji wakubwa katika sekta za gesi, mafuta na madini watabadilishana uzoefu katika suala la ulipaji wa kodi, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji mapato kwa upande wa serikali.
“Wadau hawa wanajadili namna kodi inavyolipwa, pia kupata uzoefu vipi kodi itakuwa katika sekta ya gesi na mafuta, hasa kwetu sisi Tanzania, kwani ndio tumeanza kuchimba, hasa gesi.
“Lakini pia wakati wakiangalia msukumo zaidi katika kulipa kodi, Serikali au watawala tunapaswa kuweka mazingira mazuri ya ulipaji kodi kwa wawekezaji ili kuendelea kupata mapato zaidi,” alisema Waziri Mkuya.
Mkuya aliendelea kueleza kwamba katika kuendelea na mikakati hiyo ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi, tayari serikali imeondoa misamaha katika mafuta.
“Lengo letu ni kuona tunaimarisha ukusanyaji wa mapato na tayari tumeshachukua fursa za kupunguza misamaha ya kodi,” alisema Waziri.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, alisema kwamba mkutano huo unazishirikisha nchi 19 za Afrika.
Alisema baadhi ya nchi zinazoshiriki mkutano huo ni zile zilizoanza kunufaika tayari na mapato ya rasilimali za asili, kama gesi na mafuta.
“Pamoja na uzoefu wa nchi hizo, pia wawekezaji katika gesi na mafuta wapo hapa tukijadiliana namna ya kupata mapato katika uwekezaji, hasa kwa kuangalia kodi za kimataifa na kodi za ndani zinavyoweza kutunufaisha,” alisema Kamishna Mkuu Bade.
Mkutano huo wa majadiliano kuhusu kodi kwa nchi za Afrika umezikutanisha baadhi ya nchi, zikiwamo Kenya, Malawi, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ghana, Namibia na mwenyeji Tanzania.