Susan Uhinga, Tanga
Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kimemuenzi Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa kulifanyia ukarabati gari alilokuwa akilitumia wakati wa harakati za kutafuta Uhuru wa Tanganyika.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA Nchini, Dk. Pancras Bujulu, wakati wa maonyesho ya wiki ya vijana ambayo kitaifa inafanyika mkoani Tanga.
Dk. Bujulu amesema wameamua kulikarabati gari hilo ili kumuenzi hayati Mwalimu Nyerere, ambapo kazi hiyo imefanywa na vijana wanaopata mafunzo ya ufundi stadi kutoka Moshi, mkoani Kilimanjaro.
“Gari hilo aina ya Austene yenye namba ya usajili MS 5480, inahisiwa lilitengenezwa mwaka 1947, lilikuwa limehifadhiwa kwenye ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kwetu ilikuwa kama fursa kwa vijana wetu kuonyesha namna walivyoiva kwenye ufundi tukaliomba na kupatiwa na kwa sasa tumelitengeneza na linatembea,” amesema mkurugenzi huyo.
Kwa mujibu wa Dk. Bujulu, gari hilo lilitumiwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1961 wakati wa harakati za kutafuta uhuru.
Gari hilo linatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali Oktoba 14, siku ya kilele cha maonyesho hayo.