25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri awatangazia vita wajanja wa maji

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Maji,  Profesa Makame Mbarawa ametangaza kiama cha watendaji wajanja wanaotumia kampuni zao au nyingine zinazowapa asilimia 10 na kuzipa tenda kwa upendeleo wa uchimbaji wa visima.

Alisema watu wa aina hiyo muda wao umefikia mwisho.

Waziri Mbarawa alitoa onyo hilo   Dar es Salaam jana alipokuwa katika ziara ya kutembelea na  kuzungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA).

Pamoja na mambo mengine aliwaahidi  wafanyakazi hao kukomesha watendaji wanaotoa tenda za uchimbaji wa visima kwa kampuni binafsi zisizokuwa na uwezo kwa manufaa yao binafsi.

“Hivi sasa watendaji wa aina hiyo hawatapata nafasi hiyo na badala yake serikali itakuwa ikiwatumia wakala hii ya serikali ya DDCA kufanya kazi hizo kwa ufanisi.

“Sitaruhusu tena mtendaji kuacha kuwachukua kufanyakazi za serikali kisa kuwapo mtendaji anayetaka kujinufaisha kwa asilimia 10 anazokuwa anapata,” alisema.

Akizungumzia   ombi la viongozi wa wakala hao wa maji kutotaka kushindanishwa kwenye tenda za visima vya serikali, Profesa Mbarawa, alikubaliana nao na kuwataka kufanyakazi kwa ubora wa hali ya juu   wanapopewa kazi hizo.

“Jambo hilo la kutoshindanishwa na wengine kwenye tenda za uchimbaji tutalifanyia kazi ila tukiwapa msituangushe, ingawa nawaamini katika utendaji wenu wa kazi,” alisema Mbarawa.

Waziri  aliwataka watendaji wa Wakala wa Uchimbaji kuhakikisha wanatengeneza visima vinavyotoa maji na kama visipotoa maji serikali haitawalipa chochote.

Kuhusu maombi ya kuwasaidia fedha za ukarabati wa vifaa na ununuzi kutokana na kukaa kwa muda mrefu, alisema Serikali haitakuwa tayari kuwapa fedha bila kuzifanyia kazi.

Mbarawa aliwataka viongozi wa wakala hao kutenga fungu la fedha katika fedha watakazopewa na serikali,  Sh milioni 756 zilizotokana na madeni ambayo yamelipwa kutokana na msukumo wa waziri huyo.

“Mnatakiwa kuendesha wakala wa uchimbaji katika jicho la biashara kwa sababu  mkiendelea na fikra za kuomba wizara hatutaweza kuwavumilia,” alisema.

Mbarawa alizengumzia  wasiwasi wake wa wakala huo kutofanikiwa kufikia lengo walilokuwa wamejiwekea, la kuhakikisha wanachimba visima 700 kwa mwaka  huu.

“Hadi sasa ikiwa imekatika nusu ya mwaka mmechimba visima 42 hivyo inaonyesha wazi bado kuna kazi kubwa ya kufikia visima 700 ila mtaweza kama mtakubali kujipanga na kubadilika katika utendaji wenu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles