NI kitendo chenye madhara makubwa kwa afya na hata kuchukua uhai wa mwanadamu, lakini hakielekei kukoma
miongoni mwa wanawake kwa sababu tu ya kuabudu urembo.
Ni uchomaji sindano makalioni ili kuyakuza kuwa katika ukubwa wanaoutaka, ambao hapa Tanzania kwa jina la mitaani unajulikana kama makalio ya Kichina.
Wanawake kote nchini Marekani na kwingineko duniani wamekuwa wakihatarisha maisha yao kwa kumiminika katika ‘soko jeusi’ la upandikizaji makalio ili wapate yenye ukubwa wanaotaka.
Mwelekeo huo umezidi kushika kasi kutokana na ongezeko la wanaotamani kuwa na maumbo kama ya wasanii
nyota, Jennifer Lopez, Nikk Minaj na Kim Kardashian ambao wanajulikana kwa kuwa na makalio makubwa.
Lakini vifo kutokana na makalio yanayotokana na kuchomwa sindano za kuyakuza vimeripotiwa katika miji ya
Alabama, Georgia, Florida, Pennsylvania, Nevada na New York nchini humo.
Mtaalamu mmoja wa urembo katika jimbo la Mississippi nchini humo, anakabiliwa na mashitaka ya kusababisha vifo vya wanawake wawili waliochoma sindano yenye kemikali katika makazi yake.
Nchini Venezuela, taifa la Amerika ya Kusini vitendo hivyo vya ukuzaji makalio kwa njia haramu vimekithiri kutokana na dhana iliyoenea kuwa mwanamke mwenye makalio makubwa ndiye anayependeza zaidi.
Hivyo wamekuwa tayari kuhatarisha afya na maisha yao ili tu waonekane warembo. Hata hivyo, wanawake wengi
wamekuwa wakifariki dunia kwa sababu ya kuchoma sindano zinazokuza makalio.
Lakini bado hilo halionekani kuwaumiza vichwa hasa wale ambao hawajaonja mateso yanayofuatia kitendo hicho,
pia halijakomesha biashara hiyo haramu.
Miongoni mwa wasiotishika na takwimu hizo ni Dk. Gus, ambaye ukimpatia dola 300 sawa na karibu Sh 500,000
za Tanzania hawezi kusita kumdunga sindano mwanamke katika makalio yake kwa kutumia
kemikali ijulikanayo biopolymers katika makazi yake mjini Caracas.
Mwandishi wa Shirika la Habari la ABC News alishuhudia Dk. Gus akiendesha mchakato huo wa upandikizaji makalio kwa mwanafunzi wa chuo mwenye umri wa miaka 20, aitwaye Sofia.
Kwanza alimchoma Sofia sindano ya ganzi makalioni kisha kusokomeza mrija wa cannula mwilini mwake ambamo kemikali ya biopolymer huingizwa kupitia mabomba 10 ya sindano.
“Nikiwa mtoto ilikuwa ndoto yangu kuwa na makalio makubwa. Ili kuwa mrembo, unatakiwa kuwa jasiri – ujasiri
wa kutosha kuhimili maumivu ya kuingizwa vitu vigeni katika mwili wako,” anasema Sofia katika hali ya kuhalalisha kitendo hicho.
Dk. Gus naye haonekani kuwa na wasiwasi wala kutishika na shughuli zake hizo haramu licha ya kusababisha vifo vya watu 17 mwaka jana kufuatiwa kuchomwa sindano yenye kemikali za kukuza mwili.
“Kitu cha kwanza mwanamume anachoona kwa mwanamke ni kalio lake. Nimeifanya shughuli hii kwa miaka mingi tangu nilipokuwa kijana, ” anasema.
Dk. Gus hutumia dakika 90 katika kila kalio la Sofia, akimchoma sindano moja baada ya nyingine na anakiri mteja wake hupatwa na maumivu makali, ambayo alidai ni kitu cha muda tu. Wakati anapoondoa sindano
ya mwisho kutoka kalio la Sofia, silicon huonekana zikitoka katika mwili wake kupitia cannula.
Lakini kemikali ambayo inaingizwa katika mwili wa Sofia kwa sindano haiwezi kuondoka moja kwa moja.
Ni tofauti na utumiaji wa sindano za siliconi ambazo zina kemikali zinazoweza kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine ikiwamo hadi miguuni au juu ya uti wa mgongo hivyo kusababisha maambukizo makali.
Wakati nchini Marekani kukiwa na hali ya utambuzi kuhusu mwili, nchini Venezuela ni waabudu wa miili na upandikizaji plastiki mwilini ni kitu cha kawaida sawa na safari za kwenda kumuona mtaalamu wa meno.
Pamoja na kupigwa marufuku nchini Venezuela, ambako mauzo ya silicone yanabeba adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela, Chama cha Wapandikizaji wa Plastiki nchini humo kinakadiria kuwa wanawake 2,000 kila mwezi wanachomwa sindano za kukuza makalio yao.
Katika nchi yenye watu milioni 29, ambayo urembo na mashindano ya urembo ni kipaumbele, si ajabu kuona
Venezuela ikiwa na malkia wengi wa urembo kuliko taifa lingine lolote lile duniani.
Mwanamke kutoka Georgia, Karima Gordon (23) aliyechomwa sindano huko Mississippi mwaka 2012, alikufa kwa shinikizo la damu katika mapafu yake miaka michache baadaye.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizofunguliwa mahakamani Septemba mwaka jana, kulikuwa na kiwango kikubwa cha vitu
kama kemikali ya silicone katika makalio yake ambayo yaliongezeka na kusambaa hadi sakafuni wakati mtaalamu wa afya alipojaribu kuyakata.
Mwanamke mwingine Michelle Brown (46) kwa sasa hana mikono na miguu baada ya kuchomwa kemikali za kukuza
makalio ambazo zilikaribia kumuondoa uhai.
Madaktari wanasema matokeo yoyote mabaya kutokana na sindano kama alizodungwa Sofia yanaweza yasionekane hadi baada ya miaka kadhaa.
Sofia aliiambia ABC kwamba alikuwa na wasiwasi kuwa kalio lake la kushoto lilinywea kidogo kwa ndani, hivyo anapanga kumwambia Dk. Gus ili aendelee kumchoma sindano zaidi.
Mwanamke mwingine Denny wa Venezuela, akiwa anabubujikwa na machozi, anakumbuka vyema alivyoamka
siku moja na kujikuta akiwa na uvimbe sawa na ukubwa wa mpira katika sehemu ya chini ya mgongo wake.
Hakuweza kutembea wala kuinama na uchungu ukawa mwingi kupita kiasi.
Hata kabla ya kumwona daktari, Denny, mwenye umri wa miaka 35 ambaye pia ni wakili, alijua kuwa hiyo ilikuwa athari ya kudungwa kemikali ya silicon.
Uvimbe huo ulisonga hadi katika sehemu ya chini ya mgongo wake na kuanza kuumiza uti wake wa mgongo. Yote kwa sababu ya kutafuta urembo.
“Nilishtuka mno. Nisingeweza kutembea na hivyo ndivyo masaibu yangu yalivyoanza,” anasema Denny.
Sindano hizo zilipigwa marufuku na serikali mwaka 2012, miaka sita baada ya Denny kudungwa.
Hata hivyo, wanawake wengi kama tulivyokwishaona, wanaendelea kujiongezea makalio nchini humo.
Takriban asilimia 30 ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 na 50 wanatumia
ilicon kuongeza ukubwa wa makalio yao.
Wapenda makalio makubwa hatarini kupata saratani ya ubongo Wanawake wengine wanasema kuwa wanalazimika
kuongeza ukubwa wa makalio kutokana na shinikizo kutoka kwa wapenzi wao.
Lakini madhara yanapowakuta ni wao wanaoteseka zaidi. Hali ilivyo nchini:
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) inasema wanawake wanaotumia vipodozi vya kuongeza makalio na matiti
wanaweza kupata madhara ya figo, ubongo na kansa ya ngozi. Ofisa uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza anasema, kumekuwa na wimbi kubwa la wanawake wanaotumia vipodozi vingi ambavyo havisajiliwa na
mamlaka hiyo.
Anasema vipodozi hivyo vimekuwa vikiingizwa nchini na kuuzwa kwa kificho huku wateja wakubwa wakiwa ni wanafunzi wa sekondari na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
“Wanawake wanaponunua vipodozi wanatakiwa kuwa makini kwa kuangalia kama vimesajiliwa na mamlaka,”
anasema Simwanza.
Anasema watumiaji wa vipodozi wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka kununua vipodozi vyenye viambata vyenye sumu kama Chloqinone, Chloroform na Mercury compound.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Willy Sangu anasema, kinachofanyika katika dawa hizo ni kushtua seli za mwili ili ziongezeke ukubwa na wingi isivyo kawaida.
Anasema kiasili vichocheo (homon) viko ndani ya mwili na kwamba kinachowekwa kutoka nje huwa kina madhara
makubwa kutokana na kuvuruga uzalishaji wa kawaida wa vichocheo.
“Hali hii inaweza kusababisha kutofautiana kwa viungo isivyotegemewa na wakati mwingine kusababisha
saratani,” anasema Dk. Sangu.
Anashauri watu waziogope dawa hizo kwani badala ya kuwafanya kuwa warembo zimewafanya kuwa vituko zaidi.
“Kama ni lazima kufanya hivyo wafanyiwe uchunguzi wa kina ili kujua kiasi na wingi wa mahitaji lakini kwa hapa nchini hatuwezi kufanya hivyo ni vyema wakaacha kabisa kuzitumia,” anasema.
Dk. Sangu anasema mtu aliyetumia dawa hizo pia anaweza kuathirika kisaikolojia na kuwa na dalili za kujikataa.
Makala hii imeandaliwa na Joseph Hiza na Nora Damian kwa m