Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli, ameagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi na makamanda wote wa Wilaya ya Kyerwa wasimamishwe kazi mara moja kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika kuvusha magendo ya zao la kahawa na tuhuma nyingine.
Taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imewataja makamanda wengine kuwa ni  Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kyerwa, Justine Joseph, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kyerwa Everist Kivuyo na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kyerwa, Robert Marwa.
Aidha, Rais Magufuli amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu na Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na hatua stahiki zinachukuliwa endapo watabainika kuhusika tuhuma hizo kwa mujibu wa sheria.
Tuhuma dhidi ya viongozi wa polisi katika Wilaya ya Kyerwa zimebainika jana wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa polisi wa wilayani humo husindikiza kahawa za magendo kwenda nchi jirani ambapo alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi kuwachukulia hatua askari polisi wote wa Wilaya ya Kyerwa wanaotuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo.