Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imejivunia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.
Mafanikio hayo ni pamoja na kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, kushuka kiwango cha maambukizi ya malaria na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa waganga wakuu wa wilaya na mikoa Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe alisema mafanikio hayo yameiwezesha wizara kuvuka lengo namba nne la Maendeleo ya Milenia kabla ya kumalizika mwaka 2015.
“Katika eneo la huduma za afya ya uzazi na mtoto, tumefanikiwa kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kutoka 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2005 hadi 432 mwaka 2012, vifo vya watoto vimepungua kutoka 99 mwaka 1999 hadi 45 kwa kila vizazi hai 1000,” alisema.
Alisema maambukizi ya VVU yamepungua kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi 5.3 mwaka 2012 na maambukizi kutoka kwa mjawazito kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 26 mwaka 2010 hadi 15 mwaka 2012.
“Katika kuboresha zaidi, wizara iliongeza na kusogeza huduma za upimaji wa VVU karibu na wananchi hatua iliyofanya idadi ya watu waliopima kuongezeka kutoka milioni 4.9 mwaka 2013 hadi milioni 25.4 mwaka 2013,” alisema.
Alisema huduma za wagonjwa nyumbani zimepanuliwa na kufikia watu 338,547 na mashine ndogo 525 za kupima CD4 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati.
Naibu Waziri alisema kiwango cha maambukizi ya malaria kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2008 hadi asilimia 9.2 mwaka 2012 ikiwa ni asilimia 50.
“Hata hivyo suala la kukusanya fedha, utunzaji, matumizi na uwajibikaji usioridhisha katika utekelezaji wa sera, kanuni na miongozo ni changamoto zilizotukabili,” alisema.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal aliipongeza wizara hiyo kwa jitihada zake za kupambana na magonjwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini.