BARAZA la Taifa la Mitihani (NECTA) limesema watahiniwa 775,729 wakiwamo wasichana 414,227 na wavulana 361,502, wanatarajiwa kufanya mitihani ya taifa ya kuhitimu darasa la saba leo katika shule 16,096 za Tanzania bara.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde alisema jana kuwa mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili (leo na kesho) na itahusisha masomo matano ya Kiswahili, Kiingereza, Hisabati, Sayansi na Maarifa ya Jamii.
“Maandalizi yote ya mitihani hiyo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambaza karatasi za mitihani, fomu maalumu za OMR za kujibia mitihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo,” alisema Dk. Msonde.
Alisema watahiniwa 748,514 watafanya mitihani kwa Kiswahili na wengine 27,215 watafanya mitihani yao kwa Kiingereza, lugha ambazo wamekuwa wakizitumia siku zote kujifunzia.
Watahiniwa 76 wakiwamo wavulana 49 na wasichana 27 ni vipofu huku wengine 698 wakiwa na uoni hafifu, alisema.
Dk. Msonde alisema watahiniwa hao hupewa upendeleo kwa kuongezewa dakika 20 katika kila saa moja kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa masomo mengine.
Alitoa wito kwa wanafunzi, walimu na wasimamizi wote kila mmoja kwa nafasi yake kuzingatia taratibu za kufanya mitihani na kusisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka taratibu hizo.
Pia aliitaka jamii kutoa ushirikiano kwa siku hizo mbili kuhakikisha watahiniwa wanafanya mitihani katika hali ya utulivu na kwamba kamati za mitihani za mikoa na wilaya zimejipanga kuhakikisha shughuli za kampeni za uchaguzi hazileti usumbufu.