Na MWANDISHI WETU-MONDULI
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameagiza kufukuzwa kazi Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Monduli, Kitundu Mkumbo kwa kukiuka sheria na taratibu za kutoa hati miliki za mila.
Agizo hilo alilitoa jana mbele ya wakazi wa Kijiji cha Engarooji wilayani Monduli ambao wamekua katika mgogoro wa ardhi kwa muda mrefu hali iliyowalazimu kugawanyika katika makundi mawili yasiyoelewana.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Lukuvi, alisema mwenye mamlaka ya kumilikisha mtu ardhi zaidi ya ekari 50 ni Rais pekee.
“Ofisa huyu wa ardhi ambaye ingawa awali mlishawahi kumsimamisha kazi kwa makosa mengune kama haya, lakini kwa sasa makosa haya ni makubwa na sasa afukuzwe kazi, haiwezekani amilikishe ekari zaidi ya 1,500 kinyume na sheria,” alisema Lukuvi.
Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi amezifuta hati zote za mila zilizotolewa na ofisa ardhi huyo kwa sababu zilitolewa kinyume na utaratibu kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 ambayo hairuhusu kutoa hatimiliki za mila zaidi ya ekari 50 bila idhini ya Rais.
Miongoni mwa watu waliomilikishwa maeneo makubwa katika Kijiji cha Engarooji wilayani Monduli ni Paulo Ndari mwenye ekari 716, Lekashu Ng’ene mwenye ekari 301 na Salimu Orkoskos mwenye ekari 268 ambazo zote Waziri Lukuvi amezifuta.