29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

INAPENDEZA WASANII KUSHIRIKI KATIKA TAMASHA LA URITHI


Kuelekea tamasha la urithi litakaloanza kufanyika Septemba 15 mpaka Oktoba 13 mwaka huu sehemu mbalimbali nchini, uwepo wa wasanii wa muziki na sanaa nyingine katika tukio hilo lililoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii limetuvutia wengi.

Wasanii wameendelea kupata nafasi ya kushiriki katika matukio makubwa na muhimu ya nchi, ikiwa ni ishara ya heshima ambayo sekta ya sanaa inajipatia kutokana na kazi zao zinazoonekana mbele ya viongozi na wakuu wa nchi.

Kwa maana hiyo, halitakuwa jambo la ajabu tena wasanii kushiriki katika miradi mkubwa ya Serikali, kwa kutumia nafasi zao kwenye jamii kama wasanii na vioo vinavyotazamwa na wengi kufikisha jumbe mbalimbali zinazokusudiwa.

Kama tunavyojua muziki au sanaa kwa ujumla ndiyo kitu pekee kinachoweza kumfikia mtu na kumpa elimu ya jambo fulani bila bugudha yoyote na akaitumia hiyo elimu kujiletea mabadiliko chanya mwenyewe kwenye maisha yake.

Hivyo basi ushiriki wa wasanii mbalimbali katika tamasha la urithi, ni mpango ambao nimeuelewa kwa sababu lengo kubwa ni kuhakikisha jamii inakumbuka kule ilikotoka na urithi ambao tunao kama nchi.

Tayari mastaa wa muziki nchini kama vile Jux, Joel Lwaga, Joh Makini, Nikki wa Pili, G Nako, Ditto, Nandy, Mario, Mrisho Mpoto, Mimi Mars, Vanessa Mdee, Bright, Amin, Mwasiti, Jay Melody na wengine wengi wameingia studio za Epic Records kuandaa wimbo wa tamasha hilo maarufu kama Kachumbali La Urithi.

Tamasha  hilo ambalo linatarajia kupita katika mikoa kadhaa Tanzania kama vile, Dodoma (Uwanja wa Jamhuri), Zanzibar (Stone Town na Mapinduzi Square), Dar es Salaam (Mnazi Mmoja), Mwanza (Furahisha), Karatu (Viwanja vya Mazingirabora) na Arusha katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume, limedhamiria kuikumbusha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya urithi wetu kama Tanzania.

Kupitia sanaa na matukio mengine yatakayofanyika katika matamasha hayo malengo yatakwenda kutimia kwani kuanzia mavazi, chakula, maliasili, vivutio na vingi vya kuiuza nchi yetu duniani vitakwenda kuongezewa mkazo mbele ya jamii.

Tamasha la urithi limejiwekea malengo ya kutangaza utambulisho wa Mtanzania, alama za Taifa, umoja na mshikamano wetu. Tanzania kuna utajiri wa mbuga, milima na vingine ambavyo Mungu ametujalia.

Hali kadhalika tamasha hilo limelenga kuongeza thamani ya asili ya Mtanzania, kutangaza vivutio vyetu ambavyo vinapatikana Tanzania pekee na si nchi nyingine duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles