28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

KERO HIZI HAZIPASWI KUMSUBIRI RAIS

 



Leo ni siku ya sita tangu Rais Dk. John Magufuli aanze ziara ya kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Katika ziara hiyo, ambayo tunaweza kusema kwa uhakika imepandisha joto kwa viongozi walioko chini yake, pia imeibua kero ndogondogo ambazo sisi tunaona hazikuwa na sababu ya kusubiri maagizo ya Rais Magufuli.

Mfano wa kero hizo ni ukarabati wa shule, migogoro ya ardhi, wakandarasi kutotekeleza miradi kwa wakati, matumizi mabaya ya fedha na mambo mengine kadha wa kadha.

Kero hizo, ambazo Rais Magufuli amekutana nazo katika ziara hiyo, zimetoa taswira moja tu kwamba wapo baadhi ya viongozi ambao ama hawafuatilii utendaji wa kazi wa watu waliochini yao au hawayafanyii kazi malalamiko ya wananchi.

Tunasema hivyo tukiwa na uhakika kwamba ni viongozi wachache mno ambao wanaweza kuwa na ratiba ya kufuatilia watu wake wa chini.

Viongozi wengi wa aina hii ni wale ambao wanasubiri mambo yaharibike ndipo wachukue hatua.

Tuliwahi kuandika huko nyuma kwamba kazi kubwa ya kiongozi ni kuondoa matatizo na si kuyaongeza.

Kipimo cha uongozi ni jinsi gani kiongozi anaweza kuleta ushawishi kwa watu na kufikia maendeleo yaliyotarajiwa.

Kiongozi bora hana muda wa kulalamika, bali anatafuta ufumbuzi wa matatizo ya watu, yaani wananchi au watu walio chini yake.

Kwa kutambua udhaifu wa baadhi ya viongozi wa chini, Rais Magufuli mwenyewe amewataka watendaji wake wa chini kuhakikisha kero hizo alizokutana nazo zinashughulikiwa na si kusubiri viongozi wa nchi kuzitatua na kama wakishindwa atawaondoa.

Rai yetu ni kwamba viongozi wafanye kazi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, ambayo inawaelekeza kufanya jitihada za kuongeza na kutumia rasilimali zilizopo ili kuboresha maisha ya wananchi.

Misingi ya utawala bora ambayo ipo katika vitabu ni pamoja na utawala unaozingatia demokrasia kwa maana ya kuushirikisha umma katika masuala yote yanayohusu maendeleo.

Misingi mingine ni kuhakikisha utekelezaji wa utawala wa kisheria, lakini pia haki na usawa kwa watu wote.

Misingi mingine ni uwazi katika kuendesha shughuli za maendeleo na uwajibikaji katika utendaji.

Sisi tunaamini misingi hii ikizingatiwa na kutekelezwa lazima mabadiliko yataonekana.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na kushuhudia Rais akishughulika na matatizo makubwa, huku kero ndogondogo zikitatuliwa na wasaidizi wake kwa mawasiliano ya karibu na wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles