Na Safina Sarwat Moshi
Wanafunzi3,035 wa shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Kilimanjaro wamenufaika na uchunguzi wa moyo, kupitia Taasisi ya Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Martin Shao.
Uchunguzi huo unaotekelezwa kupitia taasisi hiyo inayoitwa Bishop Martin Fuatael Shao (BMFS), unaongozwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Profesa John Shao na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Akizungumza jana mjini hapa, Dk. Shao alisema taasisi hiyo imelenga kuwasaidia wasiojiweza kufikia gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto waliozaliwa nao na wale wanaoupata kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Alisema hadi sasa wanafunzi waliofikiwa na huduma hiyo ni wa shule tano zilizopo katika Wilaya ya Hai, Siha na Moshi.
Dk. Shao alisema katika uchunguzi huo wamebaini wanafunzi wengi katika shule za msingi na baadhi wa sekondari wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya, achilia mbali ugonjwa wa moyo.
“Taasisi hii ina malengo mengi, lakini miongoni mwa hayo ni kusaidia wasiojiweza, wahitaji na yatima kupata huduma za kiafya katika hospitali na vituo vya afya, na tumegundua kuna matatizo mengi ya kiafya kwa watoto wetu, hivyo tunapaswa kuchukua hatua,” alisema Dk. Shao.
Alisema taasisi hiyo inahitaji zaidi ya Sh milioni 60 kwa mwaka mmoja kuendesha kliniki za uchunguzi wa moyo na magonjwa mengine kwa ujumla.
Dk. Shao alisema pia taasisi hiyo husaidia yatima na hadi sasa imesaidia wanafunzi 86 kupata kadi za bima ya afya na wengine kusaidiwa gharama za matibabu kulingana na maombi yaliyowasilishwa kwao.
Akitoa ufafanuzi wa kitaalamu kuhusu kliniki zinazoendeshwa na BMFS, Dk. Elichilia Robert wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, alisema timu ya madaktari na mafundi maabara wanaotoa huduma hiyo, hutoa matokeo ya uchunguzi baada ya wiki mbili katika eneo husika ili wazazi na walezi waweze kufuatilia watoto wao watapataje huduma za tiba au kushauriwa na daktari.