Na FRANCIS GODWIN-IRINGA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, imetoa uamuzi mdogo wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuwa ana kesi ya kujibu.
Nondo amekutwa na hatia katika shtaka la pili.
Akitoa uamuzi huo mdogo jana, Hakimu Mfadhiwi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa, Liad Chamshana alisema kielelezo cha pili kilichotolewa mahakamani hapo wakati upande wa Jamhuri wakiwakilisha maelezo aliyotoa polisi kuwa mshtakiwa alitekwa, alikikubali kipokelewe kama sehemu ya ushahidi na anapaswa kuithibitishia mahakama hiyo.
“Mahakama imemkuta mshtakiwa ana kesi ya kujibu hivyo ana haki ya kujitetea kwa kiapo ama bila kiapo ama kukaa kimya. uamuzi ni wake,” alisema Chamshana .
Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Wakili wa upande wa utetezi, Chance Luoga aliiambia mahakama hiyo kuwa watakuwa na mashahidi wasiopungua watano ambao hakuwataja huku akiiomba mahakama iwatumie wito maalumu.
Wakili Luoga alisema kuwa wameshindwa kwenda mahakamani hapo na mashahidi hao kwa sababu walikuwa wamefika kwa ajili ya kusikiliza uamuzi mdogo na hawakujipanga kwa ajili ya kuanza kujitetea na Hakimu Chamshama aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18 na 19, mwaka huu.