29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

BALOZI AFICHUA WATANZANIA WANAVYOIBIWA INDIA

Na BENJAMIN MASESE -MWANZA                      |                 


BALOZI wa India nchini, Sandeep Arya, amefichua jinsi maelfu ya Watanzania na Wahindi, hususani wafanyabiashara, wanavyoibiwa mabilioni ya fedha wakati wanapoagiza bidhaa zao katika nchi za Tanzania na India.

Alifichua hayo jijini hapa jana katika mkutano wa pamoja uliowakutanisha wafanyabiashara wa India na Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), kwa lengo la kutambua fursa za kiuchumi zilizopo katika pande hizo mbili.

Alisema wafanyabiashara wa India wanaogiza bidhaa kutoka Tanzania, wamekuwa wakiibiwa katika biashara ya korosho na madini na Watanzania wanaoagiza bidhaa India, wamekuwa wakiibiwa wanapofanya biashara ya vifaa vya kilimo, dawa, matrekta, bajaj, mashine mbalimbali, vifaa vya umeme na teknolojia.

Kuepukana na wizi huo, alishauri wafanyabiashara kutoiamini mitandao ya kijamii ambayo ndani yake kuna kampuni nyingi zinajitangaza kuzalisha ama kusambaza bidhaa fulani kumbe si kweli.

Alisema ni vema Watanzania wanapotaka kuagiza bidhaa kutoka India wakafika ofisi za ubalozi huo kupewa orodha ya kampuni halali zinazotambulika ili kufanya nazo biashara kwa njia halali ya kimaandishi.

“Tanzania na India ni mataifa ambayo yameanza kushirikiana miaka michache baada ya kupata uhuru wake mwaka 1961, ndiyo maana ubalozi wetu hapa nchini una miaka mingi na mazingira ya nchi hizi yanafanana kwa asilimia 80.

“India tulikuwa masikini sana, lakini hivi sasa tupo katika uchumi wa kati na tumeendelea katika masuala ya sayansi na teknolojia, kemikali, vifaa vya kilimo, dawa na vifaa vya usafiri, sasa Watanzania tumekuwa tukishirikiana nao masuala ya biashara, lakini hivi sasa pale ofisini kuna malalamiko mengi ya wafanyabiashara kuibiwa fedha zao.

“Tatizo wanaingia katika mitandao kwa ajili ya kupata taarifa ya bidhaa wanayotaka, pale wanakutana na kampuni nyingi ambazo zinadai kusambaza bidhaa fulani na bila kujiridhisha wanatuma fedha, lakini baadaye hawapati kile walichoagiza na hakuna mawasiliano tena.

“Si kwamba Watanzania ndio wanaibiwa pekee, hata kule Wahindi nao wanalia sana kutapeliwa na Watanzania katika suala la korosho na madini. Kuna wafanyabiashara wanaagiza korosho kutoka Tanzania, lakini hawapati, hivyo hivyo madini,” alisema.

Kutokana na India kuwa mnunuzi mkuu wa bidhaa za Tanzania, alisema hafurahishwi na malalamiko na upotevu wa fedha za wafanyabiashara unaoendelea na aliwataka kufika ubalozini kitengo cha biashara na kuonana na mtumishi mmoja, Baleshi Ally, ili kupata orodha ya kampuni halali za India.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Dk. Elibariki Mmari, alisema katika mkutano huo, Tanzania imeipatia India maeneo ya uwekezaji yakiwamo viwanda vya nguo kutokana na uwepo wa zao la pamba, viwanda vya ngozi, samaki na majengo makubwa ya kifahari kwa kuwa Mwanza ni kitovu cha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema jamii za watu wa India ndio wa kwanza na wengi kuishi hapa nchini na wapo ambao hawajawahi kwenda kwao kutokana na mazingira ya Tanzania kuwa mazuri, uwepo wa amani, upendo na utulivu.

Alisema India ndio nchi ya tano kufanya biashara na Tanzania na aliwataka wafanyabiashara wa hapa nchini kutumia fursa zilizopo ili kufikia uchumi wa kati kama ilivyo kwa nchi hiyo iliyokuwa masikini, lakini leo hawakamatiki kiteknolojia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles