BONN, UJERUMANI
KIONGOZI wa Ujerumani, Kansela, Angela Merkel na Rais Vladimir Putin, jana walitarajiwa kukutana katika mkutano wao wa kwanza wa kilele tangu Urusi ilipoinyakua rasi ya Crimea, jirani na Ukraine miaka minne iliyopita.
Mkutano huo umetoa fursa kwa viongozi hao kuimarisha mahusiano katika wakati ambapo kuna wasiwasi kufuatia sera mbovu za Rais Donald Trump wa Marekani ambazo ni pamoja na ushuru wake kwenye bidhaa ya chuma cha pua na bati kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya na hatua ya Marekani ya kuiongezea Urusi vikwazo.
Merkel na Putin walikutana kwa mara ya mwisho mjini Sochi Kusini mwa Urusi miezi minne iliyopita kwa mazungumzo yaliyoangazia mzozo wa Ukraine wakati ambapo pia kulianzishwa upanuzi wa bomba la gesi asilia moja kwa moja kutoka Urusi hadi Ujerumani.
Mkutano huu pia unatarajia kuzungumzia mzozo wa Ukraine, mradi wa bomba la mafuta wa Nord Stream 2 na vita vya Syria, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa Serikali ya Ujerumani, Steffan Seibert.