26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TUENDAKO: ABSALOM KIBANDA ACHAMBUA FIKRA ZA SHIVJI, MAARIFA YA ZITTO KWA CCM NA JPM

Na Absalom Kibanda           |          


NIANZE mapema kukiri kwamba ninao udhaifu mkubwa kifikra, ambao kwa kiwango kikubwa ndio umekuwa mwongozo wa tafakuri zangu kwa takribani miaka 26 sasa.

Udhaifu huo si mwingine bali ni ujinga wangu wa kuamini kwamba msingi wa hoja zangu kila ninapoangalia mustakabali wa kiuongozi na hatima ya taifa letu, unapaswa kuakisi fikra za wanafalsafa mahiri wawili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Profesa (mstaafu) wa sheria, Issa Shivji.

Yumkini, wasomaji wa maandishi yangu ambao kinara miongoni mwao ni mimi mwenyewe, watakubaliana nami kwamba udhaifu wangu wa kurejea fikra za wanazuoni hao wawili, hauko katika misingi ya ukasuku wa kukubaliana au kupinga chochote ambacho ama waliwahi kukisema au kukiandika.

Nimeanza na kukiri udhaifu huo ili kupata uhalali wa kurejea tena juu ya kile ambacho kilipatwa kusemwa na Profesa Shivji miaka 26 iliyopita, wakati taifa lilipokuwa ndio kwanza linajiandaa kurejea katika mfumo wa siasa na demokrasia ya vyama vingi.

Nilikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kipindi cha kati ya mwaka 1991/92, wakati Profesa Shivji aliposimama ndani ya ukumbi maarufu wa Nkrumah na kutoa maoni yake juu ya aina ya siasa ambayo taifa letu lilipaswa kuchukua.

Hicho kilikuwa ndicho kipindi ambacho dunia ilishuhudia kuibuka kwa fikra mpya za wakati huo, zilizokwenda sambamba na kumalizika kwa vuguvugu la miaka takribani 70 ya vita baridi ambavyo viliigawa dunia katika pande kuu mbili – Mashariki na Magharibi.

Vuguvugu hilo ndilo ambalo hapa nchini lilichagizwa na uamuzi wa Rais Ali Hassan Mwinyi, kuunda tume iliyokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo, Jaji Francis Nyalali na kukusanya maoni ya Watanzania juu ya aina ya mfumo wa siasa wa ama kuendelea na chama kimoja au kurejesha vyama vingi.

Tume hiyo ilipofika Mlimani, mwanazuoni ambaye maoni yake yaliibua kishindo kikubwa cha hamasa na ushabiki wa zama zile za ‘mapinduzi ya fikra’ alikuwa ni Profesa Shivji, ambaye alitumia muda wa kutosha kueleza mawazo yake.

Akizungumza kwa umakini na ufasaha, Profesa Shivji ambaye hakuna shaka kwamba ndiye aliyekuwa mwanazuoni maarufu zaidi chuoni hapo wakati huo, alisema changamoto kubwa ya kuukubali mfumo wa vyama vingi hapa nchini ni sura halisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Profesa Shivji aliiambia hadhara iliyojaa Nkrumah siku hiyo, kwamba CCM haikuwa ni chama cha siasa bali kwa historia yake na kwa mizizi ya kiuongozi na kiutawala iliyojijengea, ilikuwa na taswira ya kuwa chama dola zaidi.

Hakuishia hapo, bali alikwenda mbele na kueleza iwapo kweli taifa lilikuwa linataka mfumo thabiti na halisi wa demokrasia ya vyama vingi, basi taswira hiyo ya CCM ya chama-dola, ilipaswa ‘kufa’ kwanza kabla ya kuruhusu vyama shindani vya siasa kuchuana katika uwanja tambarare (level playing field).

Wakati ukumbi ukiwa umetulia kumsikiliza, Profesa Shivji aliwageukia wasomi na wanasiasa na kusema wasomi wa aina yake walikuwa ni watu waliokuwa wakipenda kuchambua masuala ya siasa kisomi na kwa uhuru, tofauti na wanasiasa ambao kwao mwelekeo wowote wa fikra miongoni mwao hitimisho lao lilikuwa ni kusaka fursa za madaraka.

Kwa maneno yake mwenyewe Shivji alisema; “Wasomi wanapenda siasa, hawapendi madaraka, wanasiasa hawapendi siasa wanapenda madaraka.” Mvumo wa shangwe, kelele na makofi ulisikika bayana masikioni mwa umati mkubwa wa jumuiya ya wana Mlimani wa zama hizo waliokuwa ukumbini mle.

Tume ya Jaji Nyalali ilipomaliza kukusanya maoni na Sheria ya Vyama Vingi ikapitishwa rasmi Julai 1992, CCM – dola ilibakia na taswira ile ile, hali ambayo imeendelea kubakia ile ile.

Ni miaka 26 sasa tangu Profesa Shivji alipoyasema maneno hayo, ambayo kila siku inayosonga mbele, uhalisi wake katika medani ya siasa za Tanzania na hususani katika uongozi wa taifa letu unazidi kuakisi kile alichokisema.

Ndani ya mfumo wa vyama vingi, CCM ya leo inazidi kujizatiti kidola pengine kuliko wakati mwingine wowote tangu mfumo wa vyama vingi uanze.

Ni juzi tu hapa Rais Dk. John Magufuli, mkuu wa nchi ambaye sina shaka hata kuandika kwamba huko tuendako baada ya kuhitimisha urais wake ataacha alama nyingi zitakazoumiza na kukuna vichwa wanazuoni, alitamka bila kuuma maneno kwamba CCM ndiyo mhimili wa uongozi wa taifa.

Huku akiwataja kwa majina na nyadhifa zao wasaidizi wake wakuu, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kuwa wote ni wana CCM jambo ambalo ni kweli, JPM kwa kauli thabiti alikwenda mbele na kusema hadharani kwamba hata Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi eti naye alikuwa mwana CCM.

Haikuwa mara ya kwanza, ya pili au ya tatu kwa Rais Magufuli ambaye yeye mwenyewe hupenda kujiita ‘Msema kweli’, kutanabahisha hilo la CCM kwa kauli na mara kadhaa kwa vitendo vilivyo bayana.

Ni Rais Magufuli yeye mwenyewe ambaye katika moja ya kauli zake kwa wakurugenzi wa wilaya, miji na majiji, alipata kutoa kauli ya kueleza kushangaa kwake iwapo atatokea mmoja wapo akatangaza matokeo ya uchaguzi utakaompa ushindi mwanasiasa ambaye si mwana CCM ilhali akijua ameshika wadhifa huo kwa uteuzi uliofanywa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.

Kauli zenye mwelekeo huo za JPM ambaye sina shaka kumwelezea kuwa ni mmoja wa marais madhubuti kutokea hapa nchini na pengine Afrika, si tu kwamba zinarejea tafakuri ya miaka 26 ya Profesa Shivji juu ya udola-dola wa CCM, bali zinaibua pia shaka iwapo washauri wa Rais huwa wanapata muda wa kutosha kutafakari kwa kina athari na pengine maana halisi ya kile ambacho kiongozi huyo anakisema na kukifanya akiwa mkuu wa nchi.

Ingawa JPM ninayemjua kwa miaka mingi ni kiongozi mkali kwa hulka, asiye na masihara katika kazi tangu nilipomfahamu akiwa naibu waziri zaidi ya miaka 20 iliyopita, kwa nafasi ya juu kitaifa aliyoishika sasa, anapaswa kuwa na washauri wa masuala ya siasa wa aina au wa kiwango cha profesa, ambao watachagiza kumwongezea umakini na pengine umahiri wakati anapotekeleza wajibu wake.

JPM huyu si yule tena waziri ambaye baadhi yetu tulikuwa huru kuingia katika ofisi yake akiwa ofisini na kueleza kwa maana ya kupambana naye kwa hoja na kifikra juu ya namna mambo yalivyokuwa yakienda ndani ya wizara alizopata kuziongoza.

JPM huyu wa leo ni Rais ambaye naamini baada ya kukaa Ikulu akiwa Amiri Jeshi Mkuu, mkuu wa nchi na kwa sehemu ndogo Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, sasa anatambua kwamba swali lake au maoni tu vinatosha kuonekana, ikatafsiriwa na ikafanyiwa kazi kama amri halali.

Ni rahisi leo kwa mchambuzi wa aina yangu kufikia hitimisho kirahisi – rahisi na pengine kwa makosa, kwamba kile kinachotokea leo hii mitaani, ambako tunaona askari polisi wakiwa na jeuri isiyomithilika ya kumkamata yeyote, wakati wowote na popote na kufanya lolote pasipo kujali chochote, ni matokeo ya tafsiri potofu za kauli za ki-maelekezo zilizopata kutolewa na wakuu mbalimbali akiwamo Rais.

Ingawa si busara na kimsingi ni jambo la aibu kubwa kuwa na jeshi lenye askari dhaifu na wasiojiamini, lakini ni fedheha kwa taifa lililojengwa na kulelewa katika misingi ya kuheshimu sheria na kutambua haki za raia, kuwa na polisi wababe wasiosikia la mtu, ambao kwa sababu tu ya kuwa na dhamana ya kulinda usalama, wako tayari pasipo kujali kupiga na kuumiza watu wasio na hatia.

Ukatili unaofanywa na baadhi ya polisi katika siku na miaka ya karibuni na ambao kwa bahati mbaya umeshindwa kukemewa hadharani si tu na wakuu wa jeshi hilo, bali pia hata na Amiri Jeshi Mkuu JPM ambaye amekuwa mwepesi sana kufuatilia taarifa mbalimbali za namna hiyo na kuzitolea kauli za kimamlaka, kwa kiwango kikubwa unaongeza shaka juu kule ambako taifa linaelekea.

Katika mazingira ambayo CCM inajitanabahisha na dola, si rahisi leo hii kumsikia kiongozi wa juu wa chama hicho tawala akitoa kauli yenye mamlaka ya kuwataka polisi kuheshimu haki za msingi za raia, kuwalinda na kutenda haki.

Unapomsikiliza Katibu Mkuu wa CCM, mwanasiasa msomi, Dk. Bashiru Ally na kumuona akitoa kauli za kuhofia kukemea matendo yasiyostahili na ya kikatili ya polisi, hupati shida kubaini ukweli kwamba hekima za kiongozi huyo zimezongwa na kivuli cha kumtaka mkuu wa nchi ndiye awe wa kwanza kuonyesha njia.

Katika mazingira ambayo sehemu mbalimbali nchini hivi sasa watuhumiwa vinara wa uhalifu ni viongozi na makada wengi zaidi wa vyama vya siasa vya upinzani, ni rahisi kwa baadhi yetu kujiuliza, matukio ya namna hii ni ya bahati mbaya au ya kupangwa.

Ni jambo lisiloingia akilini kwa Jeshi la Polisi kutaka kuliaminisha taifa leo hii, kwamba ndani ya vyama vya siasa vya upinzani na si CCM, ndiko kuliko hasa na wavunja sheria za nchi na wachochezi wanaopaswa kudhibitiwa kwa mkono wa dola kwa namna inavyoendelea sasa.

Limekuwa ni jambo la kawaida sasa, kuona na kusikia baadhi ya wabunge au madiwani wanaotokana na vyama vya upinzani, kuburutwa na polisi kwa namna ya kudhalilika na isiyo na staha, ambayo kwa baadhi yetu ukakasi wake haupaswi kuishia katika kulalamika na kulaani tu bali kuchukuliwa kwa hatua madhubuti.

Taifa limeshuhudia kumalizika kwa kampeni na uchaguzi mdogo wa madiwani na wabunge katika maeneo mbalimbali nchini.

Kile kilichotokea Tarime kwa mfano wakati wa mikutano ya kampeni ya udiwani, ambako Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema) alikamatwa na kusemekana kupigwa na polisi, ni mfano mmojawapo wa matukio ya namna hii ambayo kwangu yanalifedhehesha taifa.

Pengine ni matukio ya aina hii ambayo yamechagiza andiko la Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo), ambaye alikuwa eneo la tukio wakati Esther akikamatwa na polisi, akitaka kutafutwa kwa kile alichokiita haja ya kutafutwa kwa ‘maridhiano ya kisiasa’.

Katika sehemu moja ya andiko lake hilo lenye sehemu kuu tatu, Zitto ambaye anapendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi kwa matukio mengine kadhaa ambayo nachelea kuyataja kwa leo kwani si sehemu ya muktadha wa makala yangu, analigusa Jeshi la Polisi.

Kwa maneno yake mwenyewe, mwanasiasa huyo kijana ambaye mara kadhaa ameikosoa Serikali ya JPM kwa kukosa maarifa anaandika; “…Yafanyike mabadiliko makubwa ya Jeshi la Polisi ili kulifanya kuwa linatoa huduma ya kulinda raia badala ya kutesa raia (Polisi Service badala ya Police Force).”

Ninao uhakika wa asilimia 100 kwamba matamshi na maandishi kadhaa ya Zitto kwa Serikali, yakiwamo yale ya msingi, yamekuwa na ukakasi mwingi ambao unaonekana bayana katika majibu ya kejeli, dhihaka na dharau kutoka ama kwa viongozi wa Serikali, msemaji wa CCM au makundi mahususi ya propaganda yaliyoibuka zama hizi, yakihusisha kampeni za mitandaoni na katika magazeti.

Pengine niliseme hili mapema kwamba ziko nyakati tena mara nyingi tu, Zitto mwenyewe amekuwa mwepesi na pengine kinara wa maandishi na kauli za dharau, dhihaka, kejeli na za kuudhi dhidi ya viongozi, Serikali na hata CCM.

Mwenendo huo wa hovyo wa Zitto, wakati mwingine unaweza ukafanana na mara kadhaa kubeba ujumbe ule ule wa makundi kadhaa ya propaganda yaliyoibuka zama hizi, yakipigia chapuo yale wanayoyaona kuwa ni mafanikio ya mfano na kujivunia ya Serikali ya JPM. Haya yanahitaji mjadala mahususi.

Hata hivyo, makosa au upungufu huo wa kibinadamu wa Zitto kama ulivyo kwa viongozi wengine wa kisiasa walioko ndani na nje ya Serikali, hayafuti ukweli wa kile ambacho mara kadhaa mwanasiasa huyo kijana jasiri amekuwa akikibeba nyuma ya msamiati wake mama wa sasa, ‘maarifa’.

Kwa muktadha wa andiko langu la leo, maarifa ambayo taifa tumeyakosa leo, ni kushindwa kwetu kuchukua hatua madhubuti na makini za kuliondoa taifa katika mkondo wa CCM kuendelea kuwa chama dola badala ya kuwa chama kilicho madarakani.

Kwamba Rais wa nchi, Katibu Mkuu wa CCM na Mwenyekiti kukifungamanisha chama na Serikali katika falsafa zao za kiuongozi na katika uamuzi na mwelekeo wa jumla wa kitaifa, hilo peke yake ni tatizo.

Katika mazingira ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi anapata jeuri na anaachwa tu aendelee pasipo kukemewa hadharani, kutembea na kuitangaza Ilani ya CCM kwa wakuu wa vyombo vya usalama vilivyo chini ya mamlaka yake kwa namna ile ile ilivyofanywa wakati wa mfumo wa chama kimoja, ni rahisi sana kujua ukubwa wa tatizo hili kifikra.

Katika mazingira ya namna hii, wala sipati shida ninapoona msamiati ‘haki’ ukiwa adimu midomoni mwa viongozi takriban wote wa juu, ambao ama wanashiriki au kuchagiza kuteuliwa kwa makada kindakindaki wa CCM katika nafasi za utumishi wa umma kama za ukurugenzi wa majiji, manispaa, miji na wilaya.

Hivi unatarajia nini kitafanyika au kutokea wakati wa uchaguzi wa udiwani, ubunge na hata urais utakapofanyika huku wakurugenzi hao ndio huwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)?

Ni jambo la bahati mbaya kwamba katika mkutano wake wa juzi na waandishi wa habari, Dk. Bashiru, mmoja wa wachambuzi mahiri wa masuala ya siasa na uongozi zama akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ‘mwanafunzi’ wa fikra za Profesa Shivji hakuulizwa swali hilo.

Nitakuwa sijakosea iwapo nitahitimisha andiko langu nikiwa na kihoro kilichowekwa kiporo kwa miaka 26 sasa cha fikra za Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Shivji na chagizo la maarifa ya maudhi la mwanasiasa mwenye ushawishi, mtukutu na mahiri, Zitto kwa Serikali ya JPM na CCM yake.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Binafsi Sijaacha Herufi hata moja kuna Uchambuzi huu Kifupi niseme tu kua huu ndio uzalendo Kwa Taifa,Wenye mawazo kama haya wanahitaji Dua waishi kwa Afya njema na umli mlefu.Tatizo lilipo likisemwa Kwania njema Taifa litapiga hatua,Jema likisemawa kwa uhalisaia wake inaongesa ali ya utendaje,WTanzania Tutambue tu kua Tunaongozwa na binadam wenzetu tusitarajie matokea yakanakwamba tunaongozwa na Malaika,UPUNGUFU NDIO SIFA YA MWANADAM,TUSHIKANE MIKONO HILI TAIFA NILETU SOTE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles