31.3 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI MDOGO NA MUSTAKABALI WA MORALI YA WAPIGA KURA

Na ANDREW MSECHU                       |                     


IMEKUWA kawaida kusikia diwani au mbunge amejiuzulu nafasi yake. Hatua hiyo ni safari mpya kuelekea kwenye uchaguzi mdogo. Wabunge na madiwani wanajiuzulu katika nafasi zao kwa sababu mbalimbali.

Alipojiuzulu ubunge na nyadhifa zake zote ndani ya CCM, aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alisema amechukua uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na mwendo wa siasa nchini Tanzania, ukiukwaji wa haki za binaadamu, ongezeko la vitendo vya kidhalimu dhidi ya raia na kutokuwapo kwa mipaka baina ya mihimili ya dola, yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

Ilitafsiriwa kwamba alichukua uamuzi huo baada ya kushuhudia yaliyompata mbunge mwenzake, Tundu lissu (Singida Mashariki-Chadema) aliyekuwa ameshambuliwa kwa risasi na sasa anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji kwa mwaka mzima sasa.

Baada ya Nyalandu, lilifuata wimbi la kujiuzulu kwa madiwani na wabunge wengine kutoka Chadema na kuhamia CCM, sababu zao kwa ujumla wao, walieleza kuwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na utendaji wake.

Muda mfupi baadaye, Mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) na mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) walitangaza kujiuzulu nafasi zao, ikiwa ni mwendelezo wa wimbi la zaidi ya madiwani 23 wa Chadema kujiuzulu na kurejea CCM.

Wiki hii, wabunge wawili wametangaza kujiuzulu nafasi zao hawa ni aliyekuwa Mbunge wa Ukonga (Chadema) Mwita Waitara na aliyekuwa Mbunge wa Monduli (Chadema) Julius Kalanga na kuongeza idadi ya majimbo yanayotakiwa kurudia uchaguzi.

Hili linafanyia wakati kampeni za marudio ya uchaguzi zikiendelea katika kata 76 kote nchini kwa sababu tu madiwani wa kata hizo walijiuzulu nyadhifa zao kisha kuteuliwa na chama kipya walichohamia, CCM kuwania nafasi hizo hizo ambazo walijiuzulu awali.

Mengi yamefuata, mengi yameendelea kushuhudiwa, lakini zaidi ni hatua ya wananchi kulazimika kurejea katika uchaguzi wa marudio ambazo zimekuwa na gharama ya fedha, muda na morali.

Veronica Charles, mkazi wa Kinondoni alisema yeye ni mwanachama wa CCM lakini kwake yeye, marudio ya uchaguzi yaliyofanyika jimboni kwake Februari mwaka huu hayakuwa na maana tena kwake na hakuona sababu ya kupoteza muda wake kushiriki katika uchaguzi mwingine.

Alisema hata kama aliyekuwa akiwania nafasi hiyo alitokea katika chama cha upinzani na kuwania kupitia chama ambacho yeye ni mfuasi, hakuona mantiki ya kupotea muda wake kupiga kura kwa mara nyingine, wakati ingewezekana tu muhusika akajiuzulu muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kuwania kupitia chama hicho katika uchaguzi huo.

“Nilishiriki kikamilifu katika uchaguzi uliopita wa 2015. Ni kweli aliyekuwa mgombea wa chama changu CCM alishindwa. Maisha yaliendelea, lakini huyu mbunge hadi alipojiuzulu na kurudia uchaguzi sikuwahi kuona mkate mezani kwangu, sasa kwanini nipoteze muda wangu kwenye kampeni hadi uchaguzi mwingine wakati sjui hata wanangu watakula nini?” alisema.

Rai ya Veronica ni sehemu ya kile wanachozungumza wananchi wengi wanaopelekwa katika uchaguzi mdogo katika maeneo mengi na inaonesha taswira halisi ya mapokeo ya wananchi ambao ndio wapiga kura, kuhusu kushuka kwa morali ya kushiriki katika uchaguzi wa mara kwa mara hivyo kupunguza idadi ya wapiga kura wanaojitokeza katika uchaguzi mdogo.

Tume ya Uchaguzi

Katika uchaguzi zilizorudiwa kwenye majimbo yote matatu, yaani katika Jimbo la Singida Kaskazini, Jimbo la Siha na Jimbo la Kinondoni na katika Kata 23 ambazo madiwani wake walijiuzulu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekiri kwamba idadi ya wapiga kura imeshuka katika uchaguzi huo.

Katika taarifa yake ya baada ya uchaguzi mdogo wa madiwani Oktoba mwaka jana na uchaguzi mdogo wa wabunge Februari mwaka huu, NEC inasema kweli wameshuhudia mwitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kupiga kura tofauti na idadi ya watu waliojiandikisha.

Ufafanuzi wa NEC unaeleza kuwa hiyo inatokana na idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha uliofanyika Februari 17 pamoja na uchaguzi mwingine wa ubunge na udiwani.

Katika Jimbo la Kinondoni kati ya wapiga kura 264,066 waliojiandikisha ni wapiga kura 45,454 tu waliofika kupiga kura, hivyo wapiga kura 218,612 kutojitokeza kabisa katika upigaji kura huo.

Katika Jimbo la Siha, ilieleza kuwa kati ya wapiga kura 55,313 waliojiandikisha waliopiga kura ni 32,277 hivyo wapiga kura 23,036 kutojitokeza kupiga kura.

Takwimu zinaonesha kuwa katika uchaguzi mdogo zilizowahi kufanyika miaka ya nyuma pia wapiga kura wamekuwa wakishindwa kushiriki kikamilifu kutokana na sababu mbalimbali lakini zaidi kutokana na nia ya wale wanaojiondoa kwenye nafasi zao baada ya kuaminiwa katika uchaguzi wa awali na kurudi kuwania nafasi hizo hizo kupitia vyama vingine kupitia chaguzi ndogo.

Kwa miaka iliyopita, takwimu zinaonesha kuwa uchaguzi mdogo zilizowahi kufanyika katika majimbo ya Kalenga na Chalinze Machi 16, 2014, kati ya waliojiandikisha kupiga kura 71,964 ni 29,541 tu walijitokeza kupiga kura huku Chalinze kati ya 92,000 walioandikishwa waliopiga kura walikuwa 24,422.

Pia, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ni wapiga kura milioni nane pekee waliopiga kura kati ya milioni 21 waliojiandikisha huku mwaka 2015, kati ya wapiga kura milioni 23.2 walioandikishwa na waliojitokeza kupiga kura walikuwa milioni 15.6.

Hata hivyo, Naibu Katibu Uendeshaji Uchaguzi wa NEC, Irene Kadushi amewahi kukaririwa akisema mwitikio wa wapiga kura wakati wa uchaguzi mdogo hutofautiana na wakati wa uchaguzi mkuu na kitendo cha watu kuhama chama kimoja na kisha kuruhusiwa kugombea nafasi ile ile imechangia idadi ndogo ya wapiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Februari 17.

“Miaka ya nyuma tulikuwa na changamoto ya fedha katika kutoa elimu ya mpiga kura, lakini tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wa kutosha na sasa elimu ya mpiga kura ni endelevu. Hakuna taasisi yoyote inayoiingilia NEC katika utendaji wake ikiwamo Serikali ambayo jukumu lake huishia kwenye kuipatia tume fedha kwa ajili ya shughuli zake,” alisema.

Bosi huyo wa uchaguzi wa NEC alisema muundo wa tume hiyo unachangia wananchi kuwa na mtazamo kuwa wateule wa Serikali wanaosimamia uchaguzi kwenye ngazi za chini wanakipendelea chama tawala.

“Hii imepelekea (sababisha) sisi kuomba tupatiwe ofisi kwenye kanda mbalimbali hapa nchini jambo litakalotusaidia pia katika utunzaji wa vifaa vyetu vya kazi. Pia, tunataka tuwe na uwezo wa kuajiri wafanyakazi hasa wasimamizi wa uchaguzi hali itakayoiongezea tume kuaminika kwake,” alisema.

Anaonesha kwamba iwapo hilo litafanyika, litasaidia watu kuongeza uaminifu wao kwa tume ambayo imekuwa ikifanya kazi kubwa, kwani hata nchi ambazo tume zake zinaonekana ziko huru na haki bado zinalalamikiwa kwa mambo kadhaa.

Gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) linaikariri NEC ikieleza kwamba uchaguzi mdogo wa madiwani na wabunge ambazo zimekuwa zikifanyika kutokana na wawakilishi hao wa wananchi kufariki dunia au kuhama vyama vyao zitakoma miezi 12 kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Kauli hii inatolewa huku kukiwa na taarifa ya wimbi kubwa zaidi kuwakumba madiwani na wabunge kutoka katika kambi ya upinzani kuhamia CCM na hivyo kuwapo kwa uwezekano wa kuitishwa kwa uchaguzi mdogo ndani ya muda mfupi kila unapomalizika uchaguzi mdogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,507FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles