MEZA FRIDE (SJMC) NaTUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) imesema haijaanza rasmi kumtibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamis Kigwangalla hadi atakapopona tatizo la kifua.
Dk. Kigwangalla amelazwa wodi ya Mwaisera katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kupata ajali ya gari katika Kijiji cha Magugu wilayani Babati Mkoa wa Manyara akitokea Arusha kwenda Dodoma Agosti 4, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Respicious Boniface alisema MOI itaanza matibabu kwa waziri huyo atakapopona tatizo la kifua.
Alisema kwa sasa hali ya afya ya waziri huyo imeendelea kuimarika na atakapopona kifua ndipo watakapoanza kumtibu mfupa wa mkono uliovunjika mara mbili.
“Nilienda kumuona Dk. Kigwangalla asubuhi (jana), anaendelea vizuri kwa kuwa aliumia zaidi kifua tutasubiri mpaka atakapopona ndipo tuanze matibabu ya mfupa wa mkono,” alisema Dk. Boniface.
Alisema kwa sasa Kigwangalla anaendelea na matibabu ya kifua MNH.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema Dk. Kigwangalla yupo chini ya uangalizi maalumu wa madaktari.
“Afya ya Dk. Kigwangalla inazidi kuimarika akiwa chini ya uangalizi wa karibu wa jopo la madaktari,” alisema Aligaesha.
Baada ya kutokea ajali hiyo, Dk. Kigwangalla alipelekwa Kituo cha Afya Magugu kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Serian Arusha na baadaye MNH.
Akizungumza baada ya kumpokea, Rais Dk. John Magufuli alisema Dk. Kigwangalla, alivunjika mbavu tano, mkono ulivunjika mara mbili huku pafu likitobolewa na mbavu zilizovunjika.