25.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

KITWANGA AFICHUA SIRI SAKATA LA LUGUMI

Na EVANS MAGEGE            |          


WAZIRI wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amefichua siri iliyosababisha ashindwe kuchukua hatua juu ya sakata la mfanyabiashara, Said Lugumi, ambaye alipewa zabuni ya kuweka mashine za utambuzi wa alama za vidole yenye thamani ya Sh bilioni 37 katika vituo 108 vya Jeshi la Polisi.

Kitwanga ambaye ni Mbunge wa Misungwi, alifichua siri hiyo wakati akizungumza na MTANZANIA Jumapili katikati ya wiki hii, lililotaka kujua sababu za mawaziri wawili, yeye na Mwigulu Nchemba kushindwa kushughulikia suala hilo kipindi wakiongoza wizara hiyo.

Alisema alishindwa kulitolea uamuzi sakata hilo kwa sababu tayari lilikuwa chini ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Waziri huyo ambaye alidumu Wizara ya Mambo ya Ndani kwa miezi sita tu na kisha akaondolewa na Rais Magufuli, alisema huwa hapendi kuzungumzia mambo ya wizara hiyo lakini amelazimika kuongelea hilo la Lugumi ili Watanzania waelewe.

Alisema yeye binafsi alishindwa kuchukua hatua kuepuka kuingilia uchunguzi wa Takukuru.

“Mara kwa mara nimekuwa nikisema sipendi kuzungumzia jambo kwenye wizara ambayo nimewahi kuiongoza,  sasa ngoja nikwambie kwa kifupi tu na uwajuze Watanzania. Lugumi nafahamu alikuwa na zabuni ya kuweka mashine za utambuzi wa alama za vidole katika vituo vya polisi, sakata lake liliibuka lakini nikashindwa kulitolea uamuzi kwa sababu tayari Takukuru walikuwa wanalifanyia uchunguzi,” alisema Kitwanga.

Alisema anafahamu wapo ambao wamekuwa wakimhusisha na suala hilo la Lugumi ingawa hawako karibu.

“Binafsi naheshimu taratibu, isingekuwa vyema kutoa uamuzi kwa jambo ambalo lipo kwenye uchunguzi. Najua baadhi ya watu wanajaribu kunihusisha mimi na suala la Lugumi, lakini ukweli ni kwamba tuko mbali kama Mwanza na Mtwara,” alisema Kitwanga.

Kitwanga alidaiwa kuhusishwa na sakata la Lugumi kupitia kampuni ya Infosys  anayodaiwa kuwa mmoja wa wanahisa wakati akiwa mfanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kampuni ya Infosys ilidaiwa kuisaidia Kampuni ya Lugumi kupata mashine za utambuzi wa alama za vidole kutoka Kampuni ya Dell ya Marekani.

Hata hivyo, madai hayo yaliwahi kukanushwa na Naibu Meneja Mkuu wa Infosys, Sweki Donald, ambaye alisema kampuni yake haijawahi kufanya biashara na Kampuni ya Lugumi Enterprises.

Majibu ya Kitwanga kwamba suala la Lugumi lipo chini ya Takukuru ndiyo yaliyolielekeza gazeti hili kuwasiliana na  Msemaji wake, Musa Misalaba, ambaye alijibu kuwa uchunguzi wake umefika pazuri.

“Uchunguzi wa sakata hili bado unaendelea na tupo sehemu nzuri tu, ukikamilika tutawapeni taarifa,” alisema Misalaba.

Awali kabla ya kuwasiliana na Msemaji wa Takukuru, mwandishi wa gazeti hili alimtafuata Dk. Mwigulu Nchemba, ambaye alikuwa mrithi wa Kitwanga ili aeleze sababu ya kushindwa kulishughulikia sakata la Lugumi hadi alipoondolewa Juni mwaka huu, lakini hakupatikana.

Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, alimpa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, siku 10 hadi Julai 31, mwaka huu kumfikisha ofisini kwake Lugumi  au ajisalimishe mwenyewe saa mbili asubuhi.

Alisema uamuzi wa kutaka Lugumi akamatwe ama ajisalimishe aliuchukua baada ya kumpa maagizo IGP Sirro kupeleka taarifa ya kampuni hiyo ya kufunga vifaa ambayo ilionyesha kazi hiyo haijakamilika.

Alipoulizwa na mmoja wa waandishi iwapo Lugumi hatopatikana hatua ambazo angechukua ikizingatiwa suala hilo limeonekana kuwashinda mawaziri wawili waliotangulia, Lugola alisema mfanyabiashara huyo ni Mtanzania hivyo hadhani kama hatua hiyo itafika.

Kinachofanywa na Lugola kwasasa ni kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli, ambaye wakati alipomwapisha, Ikulu Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine alimtaka kuhakikisha anashughulikia suala la Lugumi.

Siku mbili baada ya kuapishwa, Lugola alimtaka IGP Sirro kumwandalia taarifa muhimu itakayotoa mwongozo wa suala  hilo.

Sakata la Lugumi liliibuka mwaka 2016 na Aprili 6, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Aeshi Hilaly, walibaini utata mkubwa wa utekelezaji wa mkataba huo na kuagiza upelekwe mbele ya kamati hiyo ili wajumbe waweze kujadili.

Baada ya kukolea kwa sakata hilo bungeni, Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliunda kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti huyo wa PAC, Hilary.

Kamati iliyoundwa na Bunge ilikabidhi ripoti Ofisi ya Spika ambayo ilisema ingeishauri Serikali cha kufanya.

Mwishoni mwa Juni, 2016, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliiagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo wa vifaa vya utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi, unafanya kazi ndani ya miezi mitatu kuanzia siku hiyo.

Tulia ambaye aliikabidhi Serikali matokeo ya uhakiki uliofanywa na kamati ndogo iliyoundwa, alisema ripoti ilikuwa na maoni, ushauri, mapendekezo ya namna na kutatua changamoto zilizoainishwa na taarifa ya PAC na alizuia wabunge kulijadili.

Hata hivyo, Aprili mwaka jana, sakata la Lugumi liliibuliwa tena na ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo ilieleza kampuni hiyo ilifunga mashine vituo 36 tu kati ya152.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles