NEW YORK, MAREKANI
SERIKALI ya Marekani imemuonya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, kwamba haruhusiwi kuwania muhula wa tatu madarakani.
Taarifa ya Ikulu ya nchi hiyo imemkariri Rais Donald Trump kuwa anaamini Joseph Kabila ataheshimu katiba ya nchi yake, lakini haitapenda kuona kinyume cha hatua hilo.
Kauli kama hiyo imetolewa pia na wajumbe wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zikiwamo Uingereza na Ufaransa.
Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Jonathan Cohen, amelieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, nchi yake inasikitika kuona Rais Kabila hakuitumia hotuba yake iliyopita mbele ya bunge kuondoa utata uliopo kuhusu malengo yake katika nafasi hiyo.
“Tumebaki na miezi mitano kabla ya uchaguzi kufanyika, muda wa kusuasua umekwisha,” alisema Cohen.
Taifa hilo kubwa na lenye utajiri wa madini liko chini ya shinikizo kuhakikisha linafanya uchaguzi huru Desemba 23, mwaka huu, huku kukiwa na wasiwasi kwamba Rais Kabila, ambaye amekuwapo madarakani tangu mwaka 2001, huenda akagombea tena au kung’ang’ania madaraka.
Muhula wa pili wa Kabila ulimalizika mwishoni mwa 2016, lakini alisalia madarakani kwa sababu ya kuchelewesha uchaguzi, hatua ambayo ilisababisha maandamano makubwa.
Kwa upande wake, Balozi wa Kongo kwenye Umoja wa Mataifa, Ignace Gata Mavita, hakutoa maelezo yoyote kuhusu nia ya Rais Kabila, akidokeza tu kwamba, zoezi la usajili wa wagombea urais lilishafunguliwa na litadumu hadi Agosti 8, mwaka huu.
Hata hivyo, amedai kwamba, jumuiya ya kimataifa inaingilia mchakato wa uchaguzi bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Gata amesema maandalizi ya uchaguzi yameiva, serikali inatarajia vyama vyote vya siasa nchini Kongo pamoja na washirika wake wa kimataifa ambao mara nyingi hufanya mipango ya kuingilia uchaguzi, waunge mkono zoezi hilo kwa ufanisi kupitia matendo chanya.
Aidha, balozi huyo ameongeza kuwa, serikali ya nchi yake inathamini uungwaji mkono wa washirika wa kikanda, kama vile SADC, ambako Kongo ni mwanachama.
Leila Zerrougui, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kongo, ameliambia Baraza la Usalama kwa njia ya video kwamba, uchaguzi unazidi kuleta matarajio kwa Wakongo na jumuiya za kimataifa na kwamba utaongeza usalama ndani ya nchi yao na ukanda mzima.
“Ingawa maendeleo makubwa yamepatikana katika kukamilisha hatua muhimu katika ratiba ya uchaguzi, mchakato huo unabaki kuwa chanzo cha wasiwasi na kutoaminiana baina ya chama tawala na upinzani na kati ya upinzani na tume ya uchaguzi,” alisema Zerrougui.
Ameongeza kuwa, malalamiko ya upinzani yanajumuisha uamuzi wa serikali wa kutumia mashine za kielektroniki za kupigia kura, usajili wa uchaguzi na Tume ya Uchaguzi.
Cohen, ambaye ni naibu Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, ameitaka Tume ya Uchaguzi nchini Kongo kutotumia mashine hizo za kielektroniki, ambazo hazikujaribiwa na kutumia karatasi za kupigia kura ambazo zitaaminika.
Wakati huo, makamu wa zamani wa Rais, Jean-Pierre Bemba, ameiomba kambi ya upinzani nchini humo kuteua mgombea mmoja atakayepambana na chama tawala katika uchaguzi ujao.
Akizungumza na Shirika la Habari la Reuters, Bemba amesema atakuwa mgombea sahihi iwapo ataungwa mkono na vyama vyote vya upinzani nchini humo, lakini atakuwa tayari pia kumuunga mkono yeyote atakayeteuliwa.
Mwanasiasa huyo aliachiliwa na mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita (ICC), amesema yuko tayari kushika madaraka makubwa kwakuwa anazo sifa za kuongoza.
“Uzoefu katika uongozi, ulinzi, jeshi na uchumi, ni vigezo nilivyo navyo. Vyote havidanganyi. Kwahiyo sisi wapinzani tunaweza kushinda na kutekeleza mipango yote ya maendeleo kwa kiwango kikubwa, na kwa maslahi ya umma,”