29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

BOGGOS MUSICA WAMEONYESHA MFANO, WENGINE FUATENI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, leo anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa bendi mpya ya muziki wa dansi, Bogoss Musica, katika fukwe za Escape One, jijini Dar es Salaam.

Bendi hiyo mpya inayomilikiwa na kiongozi wa zamani wa Fm Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’, Nyosh El Sadaat, imethubutu kufanya mambo ambayo katika siku za hivi karibuni yalizoeleka kufanywa na wasanii wa Bongo Fleva.

Katika siku za hivi karibuni, wanamuziki wa dansi wamekuwa wakilalamika kutopewa nafasi katika vyombo vya habari, ili kutangaza muziki wao, lakini kupitia Boggos Musica imethibitika kuwa, hali haipo hivyo.

Karibia mwezi mzima sasa kiongozi wa bendi na wanamuziki wake wapatao 20 wamekuwa wakiinadi Boggos Musica kwa njia mbalimbali, ikiwamo kufanya ziara katika vyombo vya habari, jambo ambalo lilikuwa halifanywi sana na wanamuziki wa dansi.

Ndiyo maana mwitikio wa mashabiki katika uzinduzi wa bendi hiyo inayotabiriwa kuleta mabadiliko makubwa katika muziki wa dansi nchini umekuwa ni mkubwa, kutokana na mashabiki wa dansi kusikia kile ambacho hawajawahi kukisikia.

Itakumbukwa katika kipindi cha nyuma kabla ya Bongo Fleva haijakita mizizi yake kwenye anga la burudani nchini, dansi ilipata kutawala na kujizolea mashabiki wengi walioupa nguvu muziki na wanamuziki wake.

Kutokana na sababu kadhaa ambazo wanamuziki wenyewe wa dansi wanazifahamu, hali ilibadilika ghafla na vijana wa Bongo Fleva wakafanikiwa kuchukua nafasi ya dansi kutawala sekta ya muziki.

Hali hiyo imewapa tabu sana wadau na wanamuziki wa dansi, ambao kiu yao kubwa ni kuhakikisha wanarudi kwenye ramani ya miziki pendwa nchini na katika kipindi hicho alitakiwa apatikane mtu au bendi itakayoongoza harakati hizo.

Kwa mtazamo wangu, sina shaka kabisa na harakati za Boggos Musica, kikubwa wanamuziki wengine wanaweza kuiga mfano wa bendi hiyo kuendeleza harakati zao za kurudisha muziki wa dansi kwenye chati kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kupitia harakati za Boggos, nimebaini kuwa, muziki wa dansi una mashabiki wengi, japokuwa kwa muda mrefu wamekuwa hawapati burudani wanayostahili kutokana na wadau na wanamuziki wenyewe kushindwa kukidhi haja za mashabiki kutokana na sababu kadha wa kadha

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,327FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles