26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KANGI AFIKISHA MAAGIZO 21 *NI NDANI YA SIKU 26 TU ALIZOKAA WIZARANI

 

Na GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, sasa amefikisha maagizo yasiyopungua 21 aliyoyatoa ndani ya siku 26 tangu aapishwe kushika nafasi hiyo.

Agizo jipya kabisa na ambalo katika orodha ya maagizo yake linashika nafasi ya 21 ni lile alilokaririwa na gazeti moja lililotoka jana (si MTANZANIA) akilitaka Jeshi la Polisi kupeleka taarifa za awali kuhusu mtuhumiwa Pascali Kanyembe, anayedaiwa kufariki akiwa mikononi mwa askari wa doria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, Kanyembe, aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Muungano, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita na wenzake watatu inadaiwa walikamatwa na askari wa doria kwa tuhuma za kujishughulisha na uvuvi haramu.

Ukiacha agizo hilo, kubwa kabisa ni lile alilolitoa wiki iliyopita ambapo alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, kumtafuta na kumfikisha ofisini kwake ifikapo Julai 31 mfanyabiashara, Saidi Lugumi, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Lugumi, ambaye anadaiwa kusuasua pamoja na mambo mengine kutekeleza mkataba alioingia na Jeshi la Polisi  wa ufungaji wa vifaa vya kielekitroniki vya utambuzi wa alama za vidole.

Lugola, ambaye awali alikuwa ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, amechukua nafasi  hiyo baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mwigulu Nchemba Julai mosi, mwaka huu.

Mbunge huyo wa Jimbo la Mwibara, Mkoa wa Mara, ambaye aliapishwa Julai 3, mwaka huu, ameonekana kuanza kwa kasi kubwa na hivyo kuonekana kuwa Waziri anayeongoza kwa kutoa maagizo na kauli kwa kipindi kifupi tangu ateuliwe.

Wiki hii Gazeti la Rai, ambalo ni gazeti Dada la MTANZANIA, liliandika habari ya uchambuzi ikichambua jinsi Waziri huyo anavyoongoza kwa maagizo.

Miongoni mwa maagizo mengine aliyotoa Lugola ni pamoja na lile alilolitoa Julai 3 mwaka huu, mkoani Mbeya, la kuvunjwa kwa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na kamati zake zote nchi nzima kutokana na kushindwa kupambana na ajali.

Siku kadhaa baadaye alisikika akimwagiza IGP Sirro kufungia leseni za madereva waliokwishaonywa zaidi ya mara tatu na kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa na askari wazembe wa mikoa 10 ya kipolisi inayoongoza kwa ajali za barabarani.

Julai 6 mwaka huu, Waziri Lugola aliagiza kushushwa vyeo Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Mrakibu wa Polisi, Leopord Fungu  na Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Kagera, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, George Mrutu.

Pia aliagiza wakuu wa vyombo vya usalama chini ya wizara yake kubeba ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kutekeleza yale yaliyoahidiwa na chama hicho.

Julai 12 alipotembelea Idara ya Uhamiaji, aliagiza na kuwataka askari wa idara hiyo waliopo mipakani kujitafakali kwa kuwa na utendaji usioridhisha.

Julai 14, katika ziara katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Upanga, Waziri Lugola alimpa siku 14 IGP Sirro kumueleza mikakati ya kuwawezesha Watanzania kufanya kazi saa 24, na endapo Jeshi hilo limeshindwa kupambana na majambazi hadi kufikia hatua ya kufunga maeneo yao mapema.

Pia akiwa ziarani Ukonga, Dar es Salaam, Lugola alimnyooshea kidole tena IGP Sirro, akimtaka amweleze kwanini magari hayatembei usiku na kuuliza endapo jeshi lilo limesalimu amri kwa majambazi.

Aidha, liliibuka suala la Mbwa Hobby, ambapo Waziri alibaini kuwa hayupo mahala pake pa kazi, hivyo kumtaka IGP Sirro afuatilie na kumpa ripoti kwa muda usiozidi saa 10.

Siku mbili baadaye alipozungumza na waandishi wa habari, Waziri huyo akizungumzia sakata la mbwa huyo pasipo kusema kama amepatikana ama la, alisema kuwa amebaini Kikosi cha Mbwa na Farasi kina changamoto nyingi na hivyo kumwagiza tena IGP Sirro azishughulikie.

Siku hiyo hiyo ya Julai 21 alipozungumza na waandishi wa habari, aliagiza kuwekwa mahabusu dereva atakayebainika kusababisha ajali kwa uzembe na endapo ni ubovu wa gari basi mmiliki atahusika kulala mahabusu.

Pia Lugola alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dk. Andrew Massawe, kufika ofisini kwake akiwa na watu waliopewa tenda ya kuleta mtambo wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa wenye thamani ya shilingi bilioni 32, na kumweleza kwanini mtambo haujafika au warudishe fedha.

Julai 16, Waziri Lugola alipokuwa katika mahojiano na kipindi cha Tuambie cha Kituo cha Televisheni cha Taifa (TBC1), aliagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha wanawatumia wafungwa kuzalisha chakula chao wenyewe cha kula wakiwa gerezani.

Julai 13 aliagiza kuwekwa mahabusu askari polisi aliyekuwa  katika kituo cha utalii na diplomasia, baada ya kushindwa kueleza vitabu muhimu vinavyotakiwa kuwa kwenye chumba cha mashtaka.

Pia Lugola aliagiza kukamilika haraka mchakato wa askari 10 kusoma lugha za kimataifa na masuala ya kidiplomasia, ili wakafanye kazi kwenye kituo hicho.

Amemwagiza IGP Sirro kupeleka mkakati wa uchumi na viwanda zaidi kupeleka majina na sifa za wakaguzi wa magari.

Waziri huyo pia ametaka raia yeyote akipokea mgeni akatoe taarifa serikalini, pia mtu atakayehusisha uhalifu na vyombo vya serikali atapata cha mtema kuni.

Pia ametaka kuonana na watu wa Baraza la Kiswahili nchini (BAKITA) juu ya msemo wa ‘ajali haina kinga’.

Ameagiza kuwekwa ndani polisi waliomshikilia mwanamke aliyekwenda kuripoti kutoweka kwa mumewe anayedaiwa 5,000 na mwanamke huyo kuachiliwa.

Lugola pia ameagiza na hata kutangaza kushughulika na watu  wanaobambikiwa kesi na kufuatilia endapo kuna watu wasio na kesi ndani ya mahabusu ya vituo vya polisi.

Siku ya kuapishwa, Rais Dk. John Magufuli alimpa maelekezo waziri huyo mpya wa Mambo ya Ndani  kwenda kushughulika na mambo yasiyopungua 10.

Mambo hayo ni pamoja na kushughulikia maelekezo ya Kamati ya Bunge iliyotaka hatua zichukuliwe dhidi ya mkataba wa ufungaji vifaa katika vituo 108 vya polisi, uliogharimu Sh bilioni 37, ulioihusu Kampuni ya Lugumi.

Kushughulikia uagizaji wa magari 777 ya polisi ambayo yamekwama bandarini na baadhi yake kuonekana yametumika.

Kufatilia suala la uingizwaji wa vifaa vya Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) na endapo fedha zimerudishwa baada ya serikali kuwaondoa waliokuwapo madarakani wakati huo.

Pia kushughulikia kashfa ya ununuzi wa sare za Polisi, uhaba wa magari katika Jeshi la Zimamoto, upandishwaji wa vyeo kwa askari wa vyeo vya chini waliokaa muda mrefu, Kudhibiti mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) ambayo hayana maslahi kwa Taifa.

Utoaji wa vibali vya kufanyia kazi kwa wageni, suala la wakimbizi, ambapo alidai kuna wakurugenzi wanaojihusisha na biashara ya wakimbizi.

Jingine ni ongezeko kubwa la ajali za barabarani, ambapo alitaka kuwawajibisha mara moja Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na Mkuu wa Usalama Barabarani kutokana na ajali tatu zilizotokea mkoani humo na kusababisha watu 40 kupoteza maisha ndani ya wiki mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles