32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga ‘funika bovu’

yangaNA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

FUNIKA Bovu! Ndivyo unavyoweza kuielezea timu ya Yanga ikiwa ni baada ya kuweka rekodi ya kutwaa taji la Ngao ya Jamii mara tano tofauti na timu nyingine yoyote Tanzania.

Yanga imeandika rekodi hiyo mara baada ya kuiliza Azam FC juzi kwa mikwaju ya penalti 8-7 kufuatia suluhu ndani ya dakika 90 na kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo mbele ya matajiri hao.

Wanajangwani hao wametwaa taji hilo tena mwaka 2001 na 2010 kwa kuifunga Simba mara mbili. Hivyo ni mabingwa wa kihistoria kabisa wa Ngao ya Jamii. Simba yenyewe imetwaa mara mbili (2011 na 2012), huku Mtibwa Sugar ikitwaa mara moja mwaka 2009.

Mabingwa wa Kombe la Kagame Azam FC, wenyewe hawajawahi kutwaa ngao hiyo licha ya kucheza mechi hiyo kwa mara ya nne mfululizo.

Akizungumzia ushindi wa juzi Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, amesema alijipanga kuhakikisha hawarudii makosa waliyoyafanya na kufungwa na Azam kwenye robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye mikwaju ya penalti.

“Niliweka akilini hilo na nililifanyia kazi na sasa tumepata, nilipoona dakika 90 zinaisha bila kufungana ilinibidi kuhakikisha mabadiliko tunayoyafanya yanaweza kutupa matokeo mazuri kwenye hatua ya penalti na tumefanikiwa,” alisema.

Mholanzi huyo alisema alikuwa na kila sababu ya kushinda mchezo huo kwani walifanya mazoezi ya kutosha na ya muda mrefu hivyo ilikuwa ni lazima kwao kushinda mchezo huo.

Akizungumzia mchezo huo kwa ujumla alisema: “Tulianza vizuri kipindi cha kwanza kwa kasi kubwa ingawa hatukufanikiwa kupata bao, lakini baada ya kurudi kipindi cha pili tuliweza kuutawala mchezo vizuri hasa dakika 20 za kuelekea mwishoni.”

Kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea, Medeama na Ashanti Gold za Ghana, alimalizia kwa kusema kuwa atatumia wiki chache zilizobakia kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu kuufanyia kazi upungufu aliouona kwa wachezaji wake kwenye mchezo huo.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, wataanza kulitetea taji lao Septemba 13 mwaka huu kwa kucheza na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles