NA MARKUS MPANGALA, Mitandaoni |
NCHINI Kenya kuna mnyukano wa kisiasa unafukuta chini kwa chini na kusababisha mpasuko miongoni mwa wabunge wanaotoka ukanda wa Pwani mwa nchi hiyo.
Makundi mawili yameibuka yakiwa na nia ya kuwaunga mkono wanasiasa wanaotarajiwa kugombea kiti cha urais ifikapo mwaka 2022.
Jina linalotawala kwa sasa ni la Naibu Rais William Ruto, dhidi ya kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi.
Wabunge wanaohusishwa katika mnyukano huo ni Sharrif Alwy wa Lamu na Ali Mbogo wa Kisauni, ambao kwa kauli moja wamemwambia kiongozi wa ANC, kuwa malengo yao katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022 ni kumuunga mkono Ruto kama mgombea urais.
Mudavadi, ambaye wiki iliyopita alifanya ziara huko Matuga, katika Kaunti ya Kwale, ikiwa ni nyumbani kwa mbunge wa ANC, Kassim Tandaza, ameshuhudia mnyukano mkali kati ya chama hicho na wale wanaokiunga mkono Chama cha Jubilee, hususan Ruto.
Ruto anatajwa kujipanga kumrithi Rais Uhuru Kenyatta. Duru za kisiasa zinasema makubaliano ya mwaka 2013 ndiyo yanayowaongoza Uhuru Kenyatta na Ruto.
Makubaliano hayo yalikuwa kuachiana nafasi ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, baada ya Ruto kumwachia Rais Uhuru mwaka 2013 na 2017.
Wanasiasa kutoka eneo la Pwani ya Kenya wameonyesha wazi nia ya kumuunga mkono Ruto kinyume na matarajio, huku baadhi ya wabunge kutoka upinzani wakitamka hadharani kuwa watampigia kampeni mgombea wa Jubilee, yaani Ruto.
Alwy na Mbogo wamelumbana vikali na Mudavadi, hali inayoelezwa kuwachanganya wanachama na wafuasi wa ANC.
Akizungumza kwenye mkutano wa Umoja wa Wanawake wa ANC, Mudavadi alisisitiza kuwa, wanachama na wabunge hao ni lazima wawe tayari kukiunga mkono ANC kwenye uchaguzi ujao, hoja ambayo ilikataliwa hadharani na wabunge hao.
Taarifa zinaeleza baada ya malumbano hayo, Mudavadi alilazimika kubadili mada kwenye mkutano huo.
Mbogo anadaiwa kumuomba Mudavadi kumuunga mkono Ruto na kumkumbusha kuwa wamewahi kufanya kazi pamoja walipokuwa wanachama wa ODM.
Ombi hilo halikuwaridhisha Mudavadi na wafuasi wake na kuamua kumshambulia Mbogo.
Kwa upande wake Alwy, aliwaambia wanachama na wafuasi wa ANC kuwa, hana mpango wa kumuunga mkono mgombea mwingine wa urais, isipokuwa Ruto.
“Mathalani, nikiwa nina mke ambaye ni mjamzito kwa sasa. Bila shaka nitakuwa nangojea kuzaliwa mtoto, na mtoto huyo ni Ruto,” anasema Alwy.
Kauli hiyo inadaiwa kumkasirisha Mudavadi na wafuasi wake na kuzua vurugu na kumshambulia, ili aache kuendelea na hotuba yake.
Baadhi ya wananchi wamewashutumu wabunge wanaomuunga mkono Ruto, wakidai uamuzi huo unatokana na majimbo yao kutengenezewa barabara zenye kilomita chache, wakati wakazi wa Pwani wana matatizo mengi sugu yaliyopuuzwa na serikali za kila awamu tangu enzi za ukoloni.
Mwananchi mmoja aitwaye Omar Mwinyi alisikika akisema: “Wanadanganyika na ujenzi wa barabara chache hizi, ndiyo kigezo chenu cha kumsapoti Ruto agombee urais mwaka 2022”.
Kinyang’anyio cha urais mwaka 2022 kimesababisha Ruto kujijenga kisiasa pamoja na kuweka ngome yenye nguvu katika ukanda wa Pwani wa Kenya.
Ruto anakumbuka katika uchaguzi uliopita namna chama chake cha Jubilee kilivyokuwa kimekosa kura, idadi kubwa waliwapigia kura wagombea wa upinzani kutoka vyama vya Wiper, ANC na ODM, waliokuwa kwenye Muungano wa Nasa.
Hatua ya Ruto kujikita Pwani ya Kenya imesababisha malumbano miongoni mwa wafuasi wa vyama hivyo, hali ambayo Mudavadi na chama chake wakilazimika kuchukua ajenda ya kuchagua kumuunga au kutomuunga mkono Ruto.
ANC kimebaini nguvu ya Pwani ya Kenya ikihamia kwa Ruto inaweza kukikosesha wawakilishi au kupata kura chache. Inatarajiwa kwenye mikutano yao ijayo ya Kamati Kuu ya Chama hicho itajadili iwapo wamuunge mkono Ruto, pamoja na kupata baraka za wanachama au waendelee na mipango yao.
Ziara ya ANC kwenye kaunti za Pwani imekuja siku chache baada ya Ruto kutembelea Kijiji cha Kadongo kilichopo katika kaunti ya Kisauni wiki iliyopita wakati akizindua uhakiki wa ardhi jimboni humo.
Kwa muktadha huo, Mudavadi na Ruto wamechochea joto la urais katika kaunti za Pwani.
Gavana wa Kilifi, Amason Kingi, naye amekoleza moto katika mnyukano huo, baada ya kutamka kuwa, viongozi wa ukanda wa Pwani wanafanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Uhuru na Ruto.
Ingawa Kingi alijenga hoja yake kwenye msingi wa maendeleo, hata hivyo hakutamka kufanya kazi na serikali ni kumkingia kifua Ruto, ambaye amekuwa akizunguka maeneo mengi ili kuhakikisha anaungwa mkono, hali ambayo inawapasua wapinzani wake.
Mapatano ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, yaliyofikiwa Machi 9, mwaka huu, yamechochea kuibuka kwa mijadala na juu ya nani atakuwa mgombea urais wa Jubilee kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022, licha ya kufahamika kuwa Ruto anatarajiwa kupeperusha bendera ya chama hicho.
Aidha, haijafahamika iwapo Odinga atamuunga mkono Ruto ama Uhuru atatimiza ahadi yake kwa Ruto kuwa mgombea urais mwaka 2022.
Kumalizika tofauti za kisiasa baina ya Kenyatta na Odinga kumebadilisha upepo wa urais mwaka 2022, huku Ruto akiwa mstari wa mbele kuutaka urais.
Kibarua kigumu kitakuwa kwa Ruto iwapo Odinga ataamua kugombea urais mwaka 2022. Upande mwingine Uhuru atakuwa na mtihani mgumu kati ya kumuunga mkono Ruto au Odinga.
Itakumbukwa kuwa, Odinga anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa ukanda wa Pwani, huku akiwa na uswahiba na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, Mbunge wa Likoni, Mishi Mboko na Mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir, ambao hawakujihusisha na ziara ya Ruto.
Hadi sasa Ruto ametembelea kaunti sita mara nane tangu Machi 9, mwaka huu, kiongozi huyo anafanya ziara mara kwa mara kwa sababu kaunti sita za Mombasa, Kilifi, Kwale, Taita-Taveta, Lamu na Tana River zilizopo ukanda wa Pwani zina mtaji wa kura milioni 1.7.
Ruto amechanga vema karata za kumaliza uhasama kati ya Uhuru na Odinga, kwa kujipenyeza ndani zaidi kisiasa katika ukanda wa Pwani ambako chama cha Jubilee kilipata kura chache.
Katika ziara hizo, Ruto ametoa ahadi ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo, ikiwemo suala la ardhi, ambalo halijawahi kutatuliwa tangu wakati wa ukoloni.
Akiwa kijijini Kadongo, aliwaahidi wananchi kupata hati za umiliki wa ardhi ndani ya miezi miwili ijayo. Katika Kijiji cha Majaoni, aliwaambia wananchi kuwa watapatiwa hati za ardhi zao za ekari 409.
Mkakati anaotumia umeelezewa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu baadhi ya watu wa maeneo hayo wengi walimuunga mkono Odinga, lakini sasa wanaelekea kumpigia kura Ruto.
Badala ya kuambatana na wanachama na wafuasi wa Jubilee na maofisa wa serikali, Ruto anatumia njia tofauti, kwani amekuwa akiwashirikisha wabunge waliochaguliwa na wapigakura wa maeneo hayo ili kufikisha ujumbe wake kwa ufasaha.
Licha ya mbinu hiyo, Ruto yuko makini na kutumia suala la kumalizika uhasama wa kisiasa kati ya Odinga na Uhuru pamoja na mipango ya maendeleo, ambapo amefikisha ujumbe wake kupitia wabunge wa ODM.
Hata hivyo, Ruto mwenyewe hajatamka lolote juu ya mbinu za kuhamasisha maendeleo katika ziara yake, kama nyenzo ya kujitangaza kuwania urais mwaka 2022.
Licha ya mikakati hiyo, yapo mambo kadhaa yanayoashiria kumnyima Ruto urais 2022.
Mosi, ni ukimya wa viongozi hao wawili, Uhuru na Raila, kwani hadi sasa hawajasema chochote kuhusu mbio za urais wa mwaka 2022, mbali ya kutangaza kumalizia uhasama wa kisasa kwa masilahi ya taifa lao.
Hivyo, huenda mazingira ya kisiasa yakasalia kama yalivyo sasa. Hivyo tunaweza kuhitimisha kuwa Uhuru ataendelea na mpango wake wa kumuunga mkono Ruto.
Pili, Huenda Uhuru Kenyatta akavunja ahadi yake na Ruto kwa kumuunga mkono Odinga katika uchaguzi mkuu huo.
Licha ya kuwa jambo hilo limekuwa gumu kati ya wanasiasa hawa, ambao wamekuwa mahasimu kuanzia ngazi ya familia zao, Jomo Kenyatta na Jaramogi Odinga, haijapata kutokea Jaramogi Odinga akaungwa mkono na Jomo Kenyatta kwenye mbio za urais.
Tatu, Uhuru Kenyatta anaweza kuamua kunyamaza na kufuata nyayo za Rais Mstaafu Mwai Kibaki na kuamua kutounga mkono mtu yeyote. Baada ya kumaliza muda wake wa urais, Kibaki hakumuunga mkono mgombea yeyote kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2013. Iwapo Uhuru atachukua hatua hiyo inaweza kuwa pigo kwa Ruto.
Nne, Odinga anaweza kumuunga mkono Ruto mkono kama mgombea wa chama cha Jubilee katika uchaguzi wa mwaka 2022.
Januari mwaka huu, Odinga alisema alikuwa na uwezo wa kumuunga mkono Ruto, lakini siku moja baadaye, mshauri wake, Salim Lone, alisema alikuwa akimtania tu. Iwapo hilo litatokea, litakuwa faida kwa Ruto, lakini kama halitatokea ni hasara kubwa kwake.
Tano, Ruto anaweza kuungana na viongozi wengine wa Nasa, akiwamo Mudavadi, Moses Wetangula na Kalonzo Musyoka, kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mwaka 2022.
Ruto anaweza kubadilishana kambi na Raila Odinga kwenye uchaguzi ujao. Hakuna maadui katika siasa au marafiki, ni maazimio tu na masilahi ambayo husukuma wanasiasa kuunda kambi zao. Ndiyo kusema kama Uhuru atamuunga mkono Raila, maana yake Ruto atatakiwa kuwa na ushirika mwingine, hivyo kulazimika kupambana nao ili aweze kushinda nafasi hiyo.