Na GRACE SHITUNDUÂ – DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi, aliyedumu katika taasisi hiyo kwa takribani miaka minne.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwenye vyombo vya habari, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ludovick Nduhiye, alisema Waziri Mwijage alitengua uteuzi huo jana.
Alisema kutokana na hatua hiyo, Kanyusi atasubiri kupangiwa kazi nyingine.
Ingawa taarifa hiyo haikuelezwa sababu za Kanyusi kuondolewa, lakini Brela imekuwa ikisemwasemwa na baadhi ya watu kuhusu utendaji wake.
Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakisemwasemwa dhidi ya Brela ni taasisi hiyo kuendeshwa kizamani, kwa maana ya kushindwa kupata baadhi ya huduma kupitia mfumo wa kompyuta.
Lakini pia kutokana na sababu hiyo, baadhi ya huduma kuchukua muda mrefu, mfano kusajili kampuni na kutumia mfumo wa kizamani wa kufika ofisini, badala ya ule wa kisasa wa kusajili kupitia kwenye mfumo wa kompyuta.
Zaidi Brela kushindwa kuwa na mfumo wa wazi wa kwenye kompyuta wa kuweka majina, anuwani za kampuni zote zilizosajiliwa ama kufutwa na hivyo kufanya mazingira ya kibiashara kuwa magumu.