Na Waandishi wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amepiga marufuku uuzwaji wa vyakula na matunda katika maeneo yasiyorasmi.
Agizo hilo limelenga kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea kusambaa katika jiji la Dar es Salaam, ambapo hadi sasa watu watatu wameripotiwa kupoteza maisha.
Sadick alitoa amri hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema wagonjwa wa kipindupindu wamefikia 56.
“Wagonjwa wameendelea kupokelewa na hadi jana walikuwa wamefikia 56 wakitokea maeneo ya Makumbusho, Kijitonyama, Kimara, Saranga, Manzese, Kigogo, Tandale na Mwananyamala, maeneo yote yakiwa Manispaa ya Kinondoni.
“Wagonjwa 36 kati yao wamelazwa katika kambi maalum tulizotenga,17 wametibiwa na kuruhusiwa na watatu wamefariki hadi sasa,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo ni lazima jamii na serikali kwa ujumla ikachukua hadhari vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya.
Alisema, ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, serikali mkoani humo imepiga marufuku uuzwaji wa vyakula mitaani pamoja na mikusanyiko katika misiba ya watu wanaopoteza maisha kwa ugonjwa huo.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwenye vituo vya afya vilivyokaribu nao iwapo watagundua mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Alitaja dalili zake kuwa ni pamoja na kutapika, kuharisha mfululizo choo cha majimaji meupe, ngozi kusinyaa, kiu kali, midomo kukauka, mapigo ya moyo kwenda mbio, kuumwa na misuli na mwili kukosa nguvu.
“Imefika wakati wananchi wanatakiwa kubadilika na kujua kwamba, suala la usafi ni la kila mtu.
“Tusisubiri serikali ije itufayie tuone kuwa uchafu ni adui yetu, tuwe wa kwanza kusafisha mazingira yetu ili tuwe salama,” alisema.
UCHAFU MITAANI
Wakati Sadiki akieleza hayo, uchafu kwenye maeneo mbalimbali ya jiji umekithiri, huku pia vyakula vikipikwa na kuuzwa kwenye maeneo yasiyo salama.
Kwenye eneo la Buguruni Maruzuku Kata ya Mnyamani Wilaya ya Ilala, hali ya mazingira si nzuri kutokana na mitaro kujaa uchafu na kusababisha maji taka kutuwama.
Fatuma Nasoro ambaye ni mfanyabiashara wa chakula na mjumbe wa nyumba 10 kwenye eneo hilo, alisema magari makubwa yamekuwa yakichangia kuharibu mitaro hali ambayo inachangia kutuwama kwa maji taka katika maeneo ya nyumba zao ambazo zimezungukwa na mitaro hiyo.
“Ni kweli mazingira machafu lakini tumekuwa tukitoa taarifa kwa Serikali ya Mtaa kuhusu uchafu na magari makubwa ambayo yamekuwa yakiharibu hii mitaro lakini serikali ya mtaa imekuwa ikituambia kuwa haihusiki,” alisema Fatuma.
Mfanyabiashara mwingine wa mishikaki na chipsi ambaye alijitambulisha kwa jina la Omary Salum, amekiri kuwa mazingira ni machafu na wamekuwa wakifanya jitihada za kuyasafisha pindi wanapomaliza biashara zao lakini siku inayofuata wanakuta zimejaa tena.
Alisema katika eneo hilo wanalofanyia biashara wao ni wapangaji na kwamba wachafuzi ni wakazi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakifungulia maji machafu kutoka chooni ikiwa ni pamoja na kutupa takataka ovyo majira ya usiku.
“Sisi ni wapangaji tu lakini watu wanaochafua mazingira hapa ni wakazi wa maeneo haya ambao wamekuwa na tabia ya kufungulia maji machafu pamoja na kutupa takataka,” alisema Salum.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Maruzuku Kata Mpya ya Mnyamani, Jabir Sanze, alisema taarifa za ugonjwa wa kipindupindu wamezipata hivyo amekwishachukua hadhari.
Alisema ameweka vijana wa kufanya usafi katika mitaro ya mtaa wake ikiwa ni pamoja na kuchukua dawa katika ofisi ya mtendaji wa kata kwa ajili ya kunyunyiza kwenye madimbwi, vyoo na mitaro yote ya mtaa wake.
Alisema pia amechukua dawa kwa ajili ya kutibu maji ili kuhakikisha wanadhibiti kuenea kwa ugonjwa huo ambao umesababisha baadhi ya watu kupoteza maisha.
“Nimechukua pesa yangu nimeweka vijana ili wakafanye usafi katika mitaro yote inayozunguka makazi ya watu wa mtaa wangu halafu baada ya hapo tunaanza zoezi la kunyunyizia dawa kwenye madimbwi ya maji taka, vyoo, mitaro pamoja na kutibu maji kwa Water Guard,” alisema Sanze.
Alisema pamoja na jitihada hizo lakini kumekuwa na tatizo kwa wakandarasi walioingia mkataba na Manispaa kwa ajili ya kusafisha mitaa lakini wamekuwa hawafanyi kazi inavyotakiwa na badala yake wamekuwa wakisubiri wakati wa matukio.
“Jana nilitoa taarifa kwa Afisa Afya wa kata ili awaite hao wakandarasi tupeane majukumu ya namna ya kuyasafisha mazingira yetu na badala yake mpaka hivi sasa hawajatokea lakini nitafanya juhudi zangu niwapate tuweze kuchukua hatua kutokana na kuwa janga likitokea litanihusu mimi na wananchi wangu,” alisema Sanze.
Habari hii imeandaliwa na Veronica Romwald, Jonas Mushi, Koku David.