30.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

REKODI YA WANAWAKE WANAOWANIA UONGOZI YABADILI USO WA DUNIA

LONDON, UINGEREZA                    |             


IDADI ya wanawake wanaowania nafasi za uongozi wakati wa uchaguzi inabadili uso wa dunia na kuchochea uwepo wa usawa wa jinsia katika mabunge ya mataifa mbalimbali.

Mathalani nchi ya Mexico imechagua idadi sawa ya wanawake na wanaume bungeni katika mabunge yote mawili, hatua inayodhihirisha kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa.

Juni mwaka huu Serikali mpya ya Hispania, ilichaguliwa ikiwa ya kwanza tangu nchi hiyo ilipokuwa ya kidemokrasia kuwa na wanawake wengi kuliko wanaume kwenye baraza la mawaziri.

Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern, alijifungua mtoto wa kike Juni 21 na kuwa mwanamke wa pili pekee kuwa na mtoto akiwa madarakani, baada ya waziri mkuu, Benazir Bhutto, mwaka 1990.

Hillary Clinton avutia wanawake Marekani

Mwaka mmoja baada ya Hillary Clinton kushindwa nafasi ya urais nchini Marekani, kumekuwa na wanawake ambao wanawania nafasi mbalimbali nchini humo kuliko ilivyokuwa zamani.

Mgombea wa chama cha Democrat, Alexandria Ocasio-Cortez, alimshinda mwanasiasa mkongwe, Joe Crowley, mwenye miaka 56, jijini New York mwezi uliopita. Binti huyo mwenye miaka 28, aliwashangaza wengi kwa kuwa hakuwa na historia ya kuwa kwenye siasa, lakini alipambana na mtu aliyetumika kwenye siasa kwa awamu 10.

Profesa Farida Jalalzai, mkuu wa idara ya sayansi ya siasa katika Chuo cha Oklahoma, anaamini kuwa uthubutu wa wanawake kuwania nafasi mbalimbali ni kwa sababu pia hawapendezwi na Donald Trump.

Anasema wanawake wanafanya vizuri mwaka huu kwenye bunge la Congress. Lakini kuna safari ndefu bado kwa kuwa kuna asilimia 20 pekee kwenye bunge la wawakilishi.

Wanawake Bara la Ulaya wajikongoja

Kwa upande wa Bara la Ulaya, wanawake wamefikia asilimia 30 kwenye mabunge ya mataifa ya Ulaya.

Mwaka 2017 idadi ya wanawake iliongezeka kwenye chaguzi duniani, lakini hakukuwa na mafanikio makubwa. Ulaya ilipata wanawake wachache kuwa wawakilishi bungeni, lakini wengi walikosa nafasi hizo.

Kila nchi duniani imerekodiwa kuwa na ongezeko la idadi ya wabunge wanawake tangu mwaka 1997 baada ya umoja wa mabunge (IPU) kukusanya matokeo.

Miongo miwili iliyopita Sweden, Norway, Finland, Denmark na Uholanzi zilikuwa na zaidi ya asilimia 30 ya wabunge wanawake, huku Sweden ikiongoza kwa asilimia 40.4.

Zeina Hilal, ambaye ni kiongozi wa masuala ya mpango wa jinsia ndani ya IPU, anasema juhudi za kufanikisha usawa kati ya wanawake na wanaume katika uwakilishi bado ndogo.

“Tunasikitika kwa kuwa miaka michache iliyopita kulikuwa na ongezeko la kiasi cha asilimia 0.6 kwa mwaka 2016 na 2017, kwa miaka miwili mfululizo tumefikia uwiano wa asilimia 0.1, hii inaogofya,” anasema Hilal.

IPU inakisia kuwa itachukuwa miaka 250 kufikia usawa wa jinsia kwenye mabunge. Nchi nyingi duniani hazina viongozi wanawake. Kwa sasa kuna viongozi wajuu wanawake 11 duniani, ukijumuisha marais idadi inafika 21.

Kasi ya wanawake yaongezeka

Angela Merkel ni kiongozi pekee aliyedumu muda mrefu kwenye Serikali ya Ujerumani tangu alipoingia madarakani mwaka 2005. Sheikh Hasina Wajed wa Bangladesh, yuko kwenye muhula wa tatu kuongoza nchi hiyo.

Wanawake wengine walioingia kwenye rekodi ya uongozi ni Jacinda Ardern (New Zealand), Katrin Jakobsdottir (Iceland) na Ana Brnabic (Serbia) wote walichaguliwa mwaka 2017.

Erna Solberg, alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Norway mwaka 2013. Nchini Namibia, Saara Kuugongelwa, aliingia madarakani mwaka 2015, Theresa May, akawa waziri mkuu wa pili mwanamke mwaka 2016 na Aung San Suu Kyi, akachaguliwa kuongoza nchini Myanmar.

Viorica Dancila ni mwanamke wa kwanza katika historia kuwa waziri mkuu, alichaguliwa Januari mwaka 2018.

Rwanda kinara wa uongozi wa jinsia

Kwa mujibu wa IPU nchi za Rwanda, Cuba na Bolovia, zinaongoza kwa kuwa na wawakilishi wanawake zikiwa na zaidi ya asilimia 50. Mexico ina kiasi cha asilimia 48.6.

Rwanda na nchi za Bolivia, Grenada, Mexico, Nicaragua, Costa Rica na visiwa vya Caribbean kama vile Cuba, ni miongoni mwa nchi 10 zenye zaidi ya asilimia 40 ya wabunge wanawake.

Mabadiliko ya katiba mwaka 2003 ya Rwanda yameruhusu asilimia 30 ya viti kuwa vya wanawake bungeni. Tangu wakati huo wanawake wamekuwa wakijitokeza katika chaguzi mbalimbali nchini humo.

Rwanda ilifanya mabadiliko hayo baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994 ambapo watu 800,000 wengi wanaume walipoteza maisha, wanawake walilazimika kufanya majukumu mapya mengi ili kuijenga upya nchi yao.

Rwanda ni moja kati ya nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi barani Afrika ingawa Rais Paul Kagame, amekuwa akikosolewa kuwa amekuwa akiwabana wapinzani.

Baadhi ya nchi zina wanawake wachache wawakilishi bungeni, kwa mfano   Yemen, Oman, Haiti, Kuwait, Lebanon na Thailand, zote zikiwa na asilimia 5 ya uwakilishi au chini ya hapo.

Nchi gani hazina viongozi wanawake?

Baadhi ya nchi hazina wawakilishi wanawake kabisa katika uongozi. Visiwa vya Vanuatu, Micronesia, Papua New Guinea pamoja na nchi kama El Salvador na Sierra Leone ambazo idadi ya uwakilishi wa wanawake haifahamiki.

Nchini Yemen kuna mwanamke mmoja tu aliyechaguliwa bungeni kati ya wabunge 301. Mpango wa kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa angalau asilimia 30 haujafanikiwa.

Ufisadi ulimwangusha Shinawatra

Yingluck Shinawatra, aliweka historia ya kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Thailand mwaka 2011.

Wakati huo alikuwa mmoja kati ya wawakilishi wanawake kwa asilimia 16 bungeni, lakini mwaka 2015 alishtakiwa kwa shutuma za ufisadi na kutoroka nchini humo. Tangu wakati huo idadi ya wanawake imeshuka mpaka kufikia asilimia 5.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles