LEONARD MANG’OHA Na FERDNANDA MBAMILA -DAR ES SALAAM
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), imesema mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Juni mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 3.6 Mei mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ephrahim Kwesigabo, alisema kushuka kwa mfumuko huo kumetokana na kushuka kwa bei ya bidhaa zisizo cha chakula.
Kwesigabo, alizitaja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na bia iliyopungua kwa asilimia 1.1, gharama za ukarabati vifaa vya umeme na viyoyozi 1.8, gesi za kupikia 5.6 majiko ya mkaa 2.0 na gharama za mawasiliano kwa asilimia 2.6.
“Hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2018 imepingua ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia Mei 2018,” alisema Kwesigabo.
Alisema mfumuko wa bei wa taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Alisema wakati wa upimaji huo jumla ya bidhaa 278 za chakula na zisizo za chakula hufanyiwa tathmini
Kuhusu hali ya mfumuko wa bei nchini Kenya ulipanda hadi asilimia 4.28 kutoka 3.95, huku Uganda ukipanda hadi 2.2 kutoka 1.7 katika kipindi hicho.
“Hapa ni kama nilivyowaeleza siku za nyuma kuwa si kila tunapopanda na wao wanapanda au sisi tunaposhuka na wao wanashuka, ndivyo ilivyotokea hapa wakati sisi tumeshuka wao mfumuko umepanda,” alisema Kwesigabo.