Tunu Nassor, Dar es Salaam    |
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa amesema kuanzia sasa mkandarasi atakayeshindwa kumaliza mradi wa maji kwa wakati atamfuta katika Bodi ya Wakandarasi nchini ili asiweze kufanya kazi.
Aidha, ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), kuhakikisha wanachunguza uwezo wa mkandarasi kabla ya kumpa kazi ili kupata aliye bora.
Profesa Mbarawa amesema hayo jana alipotembelea mradi wa maji wa Chalinze, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka Dawasa kufuatilia kwa makini sifa na kazi alizowahi kufanya mkandarasi kabla ya kumpa kazi.
“Lakini pia niwapongeze Dawasa kwa kushinda kesi alizokuwa akishtaki mkandarasi kwa kuwa amepewa muda wa kutosha lakini hili liwe funzo kwetu tunapotafuta mkandarasi ni lazima tufuatilie sifa na kazi alizowahi kufanya,” amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ametoa masharti manne magumu kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji katika jiji la Dar es Salaam na Pwani na akiahidi kuwanyang’anya pasi za kusafiria iwapo watashindwa kumaliza ujenzi kwa wakati.
“Kama tungefanya uchunguzi makini nadhani tusingekuwa tunapitia changamoto hii ya kuchelewa kwa mradi, hatuwezi kuvumilia kuona miradi ya maji inacheleweshwa wakati wananchi wana uhitaji mkubwa wa maji kwa sababu ya uzembe wa wakandarasi, pia namtaka Meneja Mradi kuwapo ‘site’ muda wote akifanya kazi nitakuwa nakuja kukagua mara kwa mara,” amesema Profesa Mbarawa
Pamoja na mambo mengine, amesema mradi wa upanuzi wa mfumo wa uzalishaji na ugawaji maji Chalinze kwa awamu ya tatu umegharimu Dola za Marekani Bilioni 41.223 ambapo unajengwa kwa mkopo kutoka India na wakandarasi ni kutoka nchini humo.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Dk. Suphian Masasi amesema ataangalia na kukagua kazi za wakandarasi zote kila kukicha ili ajiridhishe utendaji wao.
“Nitakula sahani moja na wakandarasi na wahandisi wazembe ambao wanarudisha nyuma juhudi za serikali kuwapatia maji wananchi,” amesema Dk. Masasi.