UMOJA wa nchi za Ulaya pamoja na Canada ambayo ni mwenyeji wa mkutano wa kilele wa nchi saba tajiri duniani, umemwonya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuwa hawaogopi chochote licha ya hofu ya kuzuka vita ya kibishara
Tamko dhidi ya Rais Trump limetolewa na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau na kusisitiza kuwa hawatatetereka kuhusiana na nyongeza ya kodi juu ya bidhaa za chuma na bati.
Naye Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema atakutana na viongozi wa Uingereza, Ujerumani na Italia kufikia msimamo wa pamoja kabla ya kukutana na Trump katika mkutano huo wa G7 unaoanza leo.
Kupitia ukurasa wa Twitter, Macron amesema Rais wa Marekani huenda asijali kutengwa na washirika, lakini pia nao hawatajali kutia saini makubaliano ya kibiashara yanayohusisha nchi sita iwapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.
Macron amesema nchi hizo sita zinawakilisha misingi ya maadili, soko la kiuchumi ambalo lina uzito kihistoria na ambazo ndizo dola halisi zenye nguvu zaidi kimataifa.
Kwa upande wake, Trump amewajibu Trudeau na Macron kwa kuwaambia kuwa zipo bidhaa za Marekani ambazo wanazitoza kodi ya juu na kuweka vizingiti dhidi ya biashara za nchi yake.
Trump ambaye alikutana na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe juzi mjini Washington, huenda kwa hivi sasa mawazo yake yote yako katika mkutano ujao wa kilele kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, utakaofanyika wiki ijayo, lakini ameweka wazi kuwa hana nia ya kulegeza kamba kuhusiana na suala la nyongeza ya kodi.
Mvutano kati ya Marekani na washirika wake ni mkubwa kiasi cha baadhi ya wachambuzi kupendekeza kuwa mkutano wa kilele wa G7 ubadilishwe jina na kuitwa G6 na Moja, huku Macron akisema viongozi wa nchi sita zinazounda G7 hawapaswi kusita kufikia makubaliano bila ya Trump.
Mvutano huo unatishia kulitikisa kundi hilo ambalo kwa miaka 43 iliyopita limekuwa likijaribu kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu masuala ya kibiashara na mengineyo.