Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
Baadhi ya wazazi katika shule ya Msingi St. Florence iliyoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam, wameanza kuhamisha watoto wao baada ya taarifa za mwalimu wa shule hiyo anayetambuliwa kwa jina la Ayoub Mlugu kudaiwa kuwadhalilisha watoto wanne wa darasa la saba katika shule hiyo.
Wazazi hao ambao (majina yanahifadhiwa) wamesema kitendo hicho kimewatisha na kusababisha hofu juu ya usalama wa watoto hao.
“Tulipopata taarifa za kubakwa kwa baadhi ya wanafunzi tumeogopa sana, mimi mwanangu yuko darasa la saba na kitendo hicho kimefanywa kwa wanafunzi wa darasa la saba, nimeogopa, nimeamua kuchukua uhamisho niwapeleke shule nyingine,” amesema mzazi huyo.
Naye mzazi mwingine ambaye mwanawe anasoma darasa la nne amesema kitendo kilichofanywa na mwalimu huyo ni kibaya na kwamba serikali inabidi ifuatilie na kuwachukulia hatua wahusika.
“Tumeshangaa kusikia mwalimu amekimbia wakati uongozi wa shule unajua suala hili wiki mbili zilizopita, siwezi kumuacha mwanangu, namhamisha,” amesema.
Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Mikocheni Venus Kimei amefika kwenye shule hiyo baada ya kupata taarifa za kubakwa kwa watoto hao ambapo amesema anasubiri kikao cha maofisa wa polisi na uongozi wa shule ili kujua kinachoendelea kuhusu suala hilo.
Amesema kama mzazi hawezi kuvumilia suala hilo kwa sababu ni kinyume na maadili lakini pia linadhalilisha watoto na kuwaumiza kisaikolojia.
“Nasubiri nipate taarifa za ndani kuhusu suala hilo ili nijue kinachoendelea ikiwamo kushirikiana na jeshi la polisi kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa mhusika aliyefanya kosa hilo,” amesema.