24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYECHUNGUZA MALI CCM, AMRITHI KINANA


*NEC yateua makatibu wapya jumuiya za chama

*Mwakilishi CCM afukuzwa uanachama, wabunge EALA wapewa onyo

Na MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM

HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Ma

pinduzi (NEC), imemteua Dk. Bashiru Ali kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho tawala akirithi nafasi ya Abdulrahman Kinana.

Dk. Bashiru ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuchunguza mali za CCM anachukua nafasi hiyo na kuwa Katibu Mkuu wanane wa chama hicho tawala nchini.

Uteuzi huo wa Muhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), umekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli kuridhia barua ya kujiuzulu Kinana mbele ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam juzi.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jioni na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema NEC imeridhia uteuzi wa kiongozi huyo.

JUMUIYA ZAPATA MAKATIBU WAPYA

Polepole alisema katika taarifa yake kuwa NEC imeteuwa makatibu wapya wa Jumuiya za chama ambapo, Raymond Mangwala ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), ambapo hadi anapata uteuzi alikuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza.

Pamoja na hali hiyo pia ni moja ya vijana waliokulia na mwenye kujua silka na hulka za UVCCM kwa kushika nafasi mbalimbali.

Nafasi alizopata kushika ni pamoja na Mwenyekiti wa Chipukizi Taifa, Katibu wa UVCCM Wilaya za Kyela na mikoa ya Dodoma na Ruvuma pamoja na kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya.

Pia ilitaja wengine walioteuliwa Mwalimu Queen Mlozi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, huku Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Erasto Sima ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba.

JINSI ALIVYOTEULIWA

Akizungumza baada ya uteuzi huo, Rais Magufuli alisema amempa dhamana hiyo Dk. Bashiru katika kipindi hiki kigumu baada ya kunong’ona na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

“Tumekupa dhamana hii katika kipindi kigumu na tumenong’ona na Makamu wa Mwenyekiti na Rais wa Zanzibar kwamba kazi hii nzuri uliyoifanya Tanzania Bara ikafanyike na Tanzania Zanzibar.

“Tumekupa jukumu hili tukiwa na matumaini makubwa kwamba yote uliyoyaona kwa miezi mitano sasa ukayafanyie kazi katika chama chote na jumuia zake kwa nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM,” alisema Rais Magufuli.

Pia Rais Magufuli aliipongeza tume iliyoongozwa Dk. Bashiru kwa kuchunguza mali za chama hicho kwa uadilifu mkubwa.

“Kuunda tume ni jambo moja, lakini kupata watu waliojitolea kiasi hiki na ukizingatia ugumu wa kazi yenyewe hata kuhatarisha maisha yao ni jambo jingine,” alisema Rais Magufuli.

Hatua ya uteuzi wa Dk. Bashiru zilithibitishwa na MTANZANIA kutokana na mapendekezo ambayo Mwenyekiti wa CCM Rais Magufuli aliyokuwa nayo.

Katika mapendekezo hayo ambayo gazeti hili liliripoti kutoka ndani ya duru za CCM kwamba katika majina matatu ambayo Rais Magufuli alikuwa akiyafanyia uhakiki wa nani avae viatu vya Kinana (Katibu Mkuu mstaafu) jina la Bashiru lilikuwapo katika chaguo la kwanza.

MALI ZA CHAMA

Katika taarifa hiyo, Polepole alisema NEC imeazimia mapendekezo yote ya tume ya kuhakiki mali za chama hicho yafanyiwe kazi mara chini ya Baraza la Wadhamini na Uongozi wa Katibu Mkuu wa CCM.

“Kazi hii ya kufanyia kazi mapendekezo ya tume ya Mwenyekiti inaanza mara moja na taarifa ya utekelezaji itatolewa katika kikao kinachofuata.

MWAKILISHI AFUKUZWA

AJenda nyingine  iliyojadiliwa ilihusu masuala ya maadili ya viongozi wa CCM ambapo kikao cha NEC kimwachisha uanachama Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe, Abdallah Maulid Diwani kwa kwenda kinyume na maadili na miiko ya viongozi wa CCM.

Katika siku za hivi karibuni akichangia hoja ndani ya Baraza la Wawakilishi alisema kwamba CCM wamshukuru Jecha kwa kuwabeba na kushinda kwenye Uchaguzi na wasitegemee mwaka 2020 kuwa Jecha (Jecha Salim Jecha Mwenyekiti wa ZEC), atakuwapo.

Hoja hiyo ambayo ilizua mjadala katika maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar huku wana CCM wengi wakionekana kukashirishwa na hoja hiyo ambayo ilionekana kwenda kinyume na misingi na maadili ya chama.

WABUNGE EALA WAONYWA

Alisema kikao hicho pia kimempa karipio kwa Fancy Nkuhi na Mariam Ussi Yahya, ambapo ni wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa mwenendo usioridhisha na usiolinda maslahi ya nchi.

KAULI YA DK. BASHIRU

Akizungumza mbele ya wajumbe wa NEC Katibu Mkuu mpya wa CCM,  Dk. Bashiru Ali, aliwashukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwa heshima na imani kubwa waliyompa na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi kubwa, uadilifu na kujituma huku akiwa mtii kwa Katiba ya CCM na Katiba ya Nchi.

 

Akifunga kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Ndg. Magufuli, Mwenyekiti wa CCM ameelekeza viongozi wa CCM kuendelea kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM huku akisisitiza Viongozi wa Serikali ngazi za Mikoa na Wilaya kushiriki katika Vikao vya Uongozi vya CCM kwa mujibu wa ratiba bila kukosa.

“Asanteni sana, jambo lingine ni kuwahidi utumishi uliotuka utii wa katiba yetu ya nchi, chama na kwa historia ya mapambano ya ukombozi wa Taifa letu,” alisema Dk. Bashiru

HARAKATI ZA BASHIRU

Ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Siasa ana anatajwa ni miongoni mwa vijana waliofuzu makuzi ya kitaaluma na kijamii kutoka kwa watu wanaoheshimika na historia ya nchini, ambayo haikuhifadhiwa rasmi vitabuni.

Anatajwa ni moja ya wasomi wenye uwezo wa kujenga hoja mbele ya umma.

Hivi karibuni alishiriki mjadala wa DW juu ya miaka 15 ya mapambano dhidi ya ugaidi, ambapo alitoa msimamo na utetezi wa mtazamo wake juu ya jinsi vita hii inavyopiganwa.

Pia anatajwa kuwa ni mtu aliyejipambanua kuwa na msimamo usiyoyumba katika masuala ya Kitaifa na yale yote anayoyaamini baada ya kuyatafiti kwa kina.

Si mtu wa papara na kuropoka, ambapo hisia zake juu ya jambo lolote hazijathibitika kufungamana na imani au itikadi.

Kutokana na hali hiyo huweza kumwita mtu huru, mwenye fikra chanya kwa mustakhabari wa jambo lolote analoshiriki kulitenda au kulipendekeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles