[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=aFxcR5ToxTc[/embedyt]
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, ameridhia uamuzi wa kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), jijini Dar es Salaam leo Mei 28, Rais Magufuli amesema Kinana aliomba kujiuzulu nafasi hiyo mara kadhaa lakini amekuwa akimzuia kutokana na juhudi zake katika chama hicho.
“Huyu ni kweli ameshaomba zaidi ya mara mbili na mara nyingine ameomba kisiri siri nikawa namzuia kila akiweka neno hilo, Nikamuuliza Makamu Mwenyekiti (Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein) akaniambia tumkubalie, nikamuuliza Mzee Mangula (Makamu Mwenyekiti, Bara, Philip Mangula), akasema tumkubalie kuchoka kupo.
“Nikaona nimuite tena jana (Kinana), labda atakuwa amebadilisha mawazo nikamwambia bwana, mimi nataka kubadilisha uendelee tu, akasema hapana, na mimi nimeridhika na nimejiridhisha, nimeridhia nimkubalie amalize muda wake wa ukatibu mkuu tutafute Katibu Mkuu mwingine,” amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Kinana amesema anamshukuru mwenyekiti kwa kukubali ombi lake kwani kila lenye mwanzo lazima liwe na mwisho.