Veronica Romwald, Dar es Salaam
Watumishi wa afya kuanzia ngazi ya jamii na hospitali za kliniki za mama na mtoto kuhakikisha wanawachunguza watoto uakisi wa mwanga kwenye mboni zao kila wanapopelekwa kliniki ili kupunguza uwepo wa saratani ya macho kwa watoto (Retinoblastoma).
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi amesema hayo leo Mei 16, jijini Dar es Salaam wakati akitoa tamko la saratani ya macho kwa watoto kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Amesema watoto 137 wenye saratani ya jicho wameonwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa mwaka 2017 ambapo kati ya hao 80 hadi 100 hupewa rufaa na kufika kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wengine hutibiwa KCMC Moshi.
“Iwapo mtoa huduma za afya unahisi kuwa mtoto ana tatizo kwenye jicho usimrudishe nyumbani hadi uhakikishe mtoto huyo ameonwa na mtaalamu wa macho ili kugundua kama ana tatizo kwenye macho yake” amesema Profesa Kambi.
Profesa Kambi amesema katika kuboresha huduma hizo Wizara imeandaa mwongozo ambao utasaidia kuinua uelewa wa wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua watoto wenye tatizo hilo na kuwapa rufaa mapema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa mpango wa Macho wizara ya Afya Dk. Benadertha Shilio amewashukuru wadau wote wa macho ambao wamekuwa bega kwa bega na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha kuboresha huduma za macho kwa watoto.