27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

WANASAYANSI WATENGENEZA MADIRISHA YASIYOPITISHA KELELE HATA YAKIWA WAZI

HASSAN DAUDI NA MITANDAO


HAKUNA ubishi kuwa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yamekuwa na msaada mkubwa katika kila hatua ya mabadiliko ya mwanadamu hapa ulimwenguni.

Katika hilo, hebu fikiria namna ugunduzi wa vifaa vya kiteknolojia, mfano simu, ulivyosaidia kwa kiwango kikubwa kurahisisha utendaji kazi wa kila siku, ziwe za nyumbani au ofisini.

Mathalan, si tena barua ambayo huenda ingechukua majuma kadhaa kumfikia mlengwa. Kupitia teknolojia ya simu, ujumbe utafika kwa dakika moja au chini ya muda huo, bila kizuizi cha umbali unaoweza kuwapo kati ya anayetuma ujumbe na anayeupokea.

Kwa lugha ya vijana wa kizazi cha sasa, unaweza kusema maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yameyafanya maisha kuwa rahisi kama ambavyo wengine wanaweza kusema.

Kutokana na umuhimu wake katika karne hii ya 21, mataifa yaliyoendelea yameshituka na kuelekeza uwekezaji wao katika soko la teknolojia.

Baada ya gunduzi nyingi zilizowahi kufanyika, kuna hii ya hivi karibuni ya wanasayansi walioyatambulisha madirisha ya kisasa yenye uwezo wa kuzuia kelele hata yanapokuwa wazi.

Ndiyo kazi hiyo imefanywa kwa ushirikiano wa watafiti kutoka vyuo vikuu vya mataifa matatu; Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nanyang (NTU) cha Singapopre, Chuo Kikuu cha Southamton nchini Uingereza na Chuo Kikuu cha Tottori, Japan.

Lengo la teknolojia hiyo ni kukabaliana na kero za sauti za magari katika maeneo ya barabarani au majirani wenye kelele zinazoweza kukufanya ukose usingizi. Yaani, hizo tena zisiwe sababu za kutoishi mjini ukiwa na dirisha la aina hiyo.

Wakiyaelezea madirisha hayo, wagunduzi hao wanasema ni asiliminia 50 pekee ya kelele zinazozalishwa nje ndizo zitakazofanikiwa kupenya pindi yanapokuwa hayajafungwa.

Kwa mujibu wa  wanasayansi hao, kifaa maalumu kimepandikizwa katika dirisha na kazi yake kubwa itakuwa ni kufyonza sauti ili zisiweze kumfikia aliye chumbani.

Profesa Gan Woon Seng, Mkurugenzi wa NTU, ambaye ndiye aliyeusimamia utafiti huo kuanzia mwanzo hadi ulipokamilika, anasema: “Hapo sasa utaweza kuliacha wazi dirisha kwa ajili ya hewa safi, bila kuhofia usumbufu unaoweza kutokana na kelele za nje.”

Mkurugenzi huyo anaongeza kuwa kifaa hicho cha kuzuia sauti za nje, ambacho tayari kimeshafanyiwa majaribio na kufaulu, kinatumia umeme wa ‘watts’ nane, sawa na spika ndogo za ‘bluetooth’.

Kuthibitisha utendaji kazi wake, watafiti hao walitumia chumba kimoja cha Chuo cha NTU, ambapo nje waliweza kuandaa mazingira ya kelele za wajenzi na injini za ndege na gari moshi (treni).

Akiizungumzia mipango yao ya baadaye juu ya teknolojia hiyo, Profesa Seng anasema kwa sasa bado hawajaridhika kwani wanatafuta njia ya kuiboresha zaidi ili katika siku za usoni iweze kutumika katika eneo kubwa na si dirishani pekee.

Mbali ya hilo, aliongeza kuwa wanaangazia pia watakavyoweza kuhakikisha inakuwa teknolojia ya bei rahisi ili iweze kuwafikia watu wa kipato cha chini na si kubaki kuwa ya wenye uwezo.

Hii ni mara ya pili NTU kuhusika katika gunduzi kubwa na za kihistoria ndani ya mwaka huu pekee kwani tayari taasisi hiyo iliyojikita katika Sayansi ya Baiolojia kinatamba na teknolojia yake ya ‘peni ya kamera’  katika sekta ya afya.

Peni hiyo maalumu imepachikwa kamera ndogo ambayo madaktari wa macho huitumia kugundua mapema mgonjwa anayekaribia kupoteza uwezo wa kuona (upofu).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles