25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MILENGWELENGWE: SHULE INAYOTISHIA MAISHA YA WANAFUNZI

Na Ashura Kazinja, Morogoro


LICHA ya Serikali kufanya kila jitihada kuhakikisha inakabiliana na changamoto zinazozikumbuka shule nyingi nchini, hususani zile za vijijini, hali bado si nzuri kwa baadhi ya shule hizo kutokana na sababu kadha wa kadha.

Miongoni mwa changamoto hizo ni upungufu wa walimu, uhaba wa madawati, uhaba wa madarasa, ukosefu wa matundu ya vyoo vya kutosha, utoro na mimba.

Lakini hali ni tofauti kwa shule ya Sekondari Milengwelengwe, iliyopo Kata ya Mngazi, Tarafa ya Bwakila Chini, Halmashauri ya Morogoro, ambayo imejengwa bondeni, karibu kabisa ya mto, hali inayosababisha shule hiyo kukumbwa na mafuriko wakati wa mvua na hivyo wanafunzi kukosa masomo kipindi chote cha mvua.

Shule hiyo yenye wanafunzi 414 wa kidato cha kwanza hadi cha nne ilijengwa mwaka 1997 ikiwa ni miongoni mwa shule kongwe iliyojengwa  na wananchi na ya pili kwa shule za sekondari ili kuondoa tatizo la wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi kushindwa kuendelea na Sekondari.

Hali hiyo imewafanya wananchi wa Kijiji cha Milengwelengwe kupaza sauti zao na kulalamikia hali hiyo kwa kuwa inahatarisha maisha na usalama wa wanafunzi, pia huwafanya watoto wakose masomo kila inapofika kipindi cha mvua.

Wananchi hao wanatumia fursa iliyotolewa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) mkoani Morogoro, kuiomba serikali kuiangalia changamoto hiyo na nyinginezo zinazoikabili shule hiyo, ili kuwawekea wanafunzi mazingira mazuri na salama ya kusomea.

George Kibuguzwa anasema kujengwa kwa shule hiyo bondeni na katika ardhi oevu, kumesababisha ifungwe kwa takribani miezi minne mwaka jana, hivyo sasa hivi wanahofia mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza kuleta mafuriko kama ya awali.

“Mwaka jana shule ilifungwa kuanzia Machi hadi Julai, wanafunzi walikosa masomo hivyo, ikawalazimu wale wa kidato cha nne na cha pili wazazi wao wawaombee nafasi katika shule ya Msingi Milengwelengwe, hata sasa shule itafungwa” anasema Kibuguzwa.

Anasema kuwa shule hiyo ipo karibu na mto ambao unazidisha mafuriko na kwamba kuna kipindi  wanafunzi hutumia mitumbwi kuingia shuleni hapo, huku vyoo vikifurika na kusababisha kinyesi kuelea juu ya maji hali ambayo ni hatari kwa afya.

Naye Grace Jeremia anasema: “Kuna mitaro imechimbwa eti kuzuia athari za mafuriko katika shule hiyo, lakini kwa bahati mbaya haina uwezo huo, maji yanajaa na kusababisha vyoo kutoa kinyesi nje na kuelea katika maji, shule yenyewe imejengwa katika eneo la diwani.”

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Gwacha Albin anakiri kwamba matatizo wanayokutana nayo ni makubwa na yanaathiri utendaji kazi.

Anasema juhudi za kuinusuru shule hiyo zinahitajika, kwani madhara ambayo wanaweza kukumbana nayo hapo baadaye yanaweza kuwa makubwa zaidi ya ilivyotokea hapo awali hadi kusababisha shule kufungwa kwa miezi minne mfululizo na kuwafanya wanafunzi kukosa masomo.

“Ni kweli shule ipo bondeni, kipindi cha masika huwa tunapata shida mno kutokana na mazingira yenyewe yalivyo, kuwe na mafuriko au yasiwepo vyoo lazima vijae kipindi cha masika. Tunahofia sana usalama wa hawa watoto kiafya. Hali hii tunakabiliana nayo tangu mwaka 2014 na ilipofika mwaka jana, mambo yalikuwa mabaya zaidi,” anasema Albin.

Anaongeza kuwa changamoto nyingine zinazowakabili kuwa ni nyumba za walimu ambazo zinalika na kutoboka kutokana na ardhi kuwa ya chumvi.

Anasema kuwa kutokana na ardhi ilivyo, zilipaswa kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara lakini jambo hilo huwa halifanyiki na kwamba mara ya mwisho kufanyiwa ukarabati ni mwaka 1997.

“Walimu hawana namna, inawalazimu kila mmoja kutafuta mbinu ya kuziba matundu hayo ikiwamo kuziba kwa kutumia viloba au matofali. Yaani kwa kifupi ni kwamba kila mwalimu anapambana na hali yake,” anasisitiza Albin.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Elimu Kata ya Mngazi, Yudasi Zaganzwa anasema awali hali ilikuwa shwari na wanafunzi walisoma kwa mwaka mzima bila kukumbwa na mafuriko, lakini kutokana na uharibifu wa mazingira, wingi wa mifugo na ongezeko la watu hali imebadilika.

“Serikali imeamua kuchimba mitaro ili kuzuia mafuriko, lakini eneo limeshakuwa oevu, hivyo hata kusipokuwa na mafuriko, mvua kidogo tu chem chem inajaa na kusababisha vyoo navyo kujaa usawa wa futi moja kutoka kwenye mashimo ya vyoo,” anasema Zaganzwa.

Zaganzwa anasema awali ulikuwapo mpango wa kuisogeza shule hiyo lakini kutokana na majengo kuwa makubwa na ya gharama kubwa, ilishindikana na hivyo kuamua kuchimbwa mitaro ya kupambana na mafuriko hayo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro, Sudi Mpili anasema wakati shule hiyo inajengwa ardhi ilikuwa kavu na hakukuwa na mafuriko bali uharibifu wa mazingira ndio uliobomoa kingo za mto na kubadilisha njia ya maji kupita, hivyo kuyafanya yaelekee shuleni.

“Shule si kwamba imejengwa bondeni, ni uharibifu wa mazingira ulioharibu kingo za mto na kuufanya mto kubadilisha njia na kuelekea shuleni, huku mto mkubwa ukiwa umejaa michanga na kuufanya kukosa kina na hivyo maji yakijaa nayo yanatapakaa kuelekea shuleni,” anafafanua Mpili.

Mpili anasema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imeweka tuta kubwa kuzuia maji yasielekee shuleni  hapo na kwamba mipango ipo ya kuiendeleza shule hiyo. Hivyo, mwaka huu haitafungwa kwakuwa  wamejipanga kwa tahadhari.

Hata hivyo, serikali haina budi kulishughulikia suala hili kwa haraka na kusimamia ukarabati wa nyumba za walimu ili waweze kufanya kazi kwa moyo bila kuwaza mahali pa kulala.

Hakuna jambo baya kama watoto kusoma katika shule ambayo inahatarisha uhai wao. Jambo hili linahitaji ufumbuzi wa haraka ili kuwanusuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles