Gabriel Mushi, Dodoma
Serikali inatarajia kuajiri walimu 10,140 katika shule za msingi ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 2, bungeni jijini Dodoma na Naibu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa (CCM).
Ngalawa alitaka kujua ni lini serikali itaanza kuajiri walimu katika jimbo lake ambalo linalokabiliwa na uhaba wa walimu hususani katika shule za msingi.
Akijibu swali hilo Kakunda amesema kwa sasa serikali inaendelea na ukaguzi wa vyeti vya walimu 10,140 ili waajiriwe kuanzia Juni 30 mwaka huu.
Aidha, amewataka wabunge kuvuta subira wakati serikali inakamilisha taratibu za ukaguzi wa vyeti hivyo.