25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

MALASUSA AWEKA REHANI UASKOFU


Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM     |

UAMUZI wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kumwadhibu kwa kumtenga Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa kwa tuhuma za usaliti, huenda ukamweka katika wakati mgumu zaidi ikiwa hata kuupoteza uaskofu, iwapo hatatimiza sharti la kuomba msamaha.

Jana gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumamosi, liliripoti habari za ndani, likieleza kiini cha tuhuma hizo za usaliti dhidi ya Askofu Malasusa, kinaelezwa ni uamuzi wake wa kuzuia waraka wa Pasaka ulioandaliwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo, usisomwe katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani anayoiongoza.

Inaelezwa taarifa za uamuzi huo, ulitangazwa pia kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT cha siku mbili, ambacho nacho kilikuwa kikifanyika mkoani Arusha sanjari na kile cha Baraza la Maaskofu na kuhudhuriwa na wajumbe wake, ambao ni maaskofu, makatibu wakuu wa dayosisi zote 25 na wakuu wa vitengo.

Jana kwa mara nyingine tena, MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Askofu Malasusa ili kufahamu iwapo ataliomba kanisa msamaha kama alivyoelekezwa na kikao hicho cha Baraza la Maaskofu baada ya kupewa muda wa kujitafakari, hadi ifikapo Septemba, lakini hakupatikana.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili limezikusanya toka katika vyanzo mbalimbali ndani ya kanisa hilo na kikao ambacho kilimchukulia hatua, inadaiwa ndani ya kikao hicho cha Baraza la Maaskofu alijaribu kufanya hivyo, lakini alikataliwa.

Baadhi ya wachungaji waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, mbali na kushangazwa na taarifa hizi kufika chumba cha habari cha gazeti hili kwa kile walichokieleza zilikuwa ni taarifa ambazo ni za ndani sana, lakini walisema Askofu Malasusa ana kibarua kigumu mbele yake iwapo hataomba radhi.

Wanaotoa hoja hiyo wanasema iwapo atapuuza suala la kuomba radhi, huenda akakumbana na kukataliwa na wachungaji wa dayosisi yake, ambao kimsingi baadhi yao ndio waliopeleka taarifa za kumshtaki kwenye kikao cha Baraza la Maaskofu, wakidai kuwazuia kuusoma waraka huo.

Chini ya utaratibu wa kanisa hilo, inaelezwa pamoja na kwamba linaongozwa na Baraza la Maaskofu, lakini uamuzi wa kumvua uaskofu Dk. Malasusa uko chini ya dayosisi anayoiongoza.

Akizungumzia uamuzi huo dhidi ya Dk. Malasusa ambaye amekuwa mkuu wa kanisa hilo kwa miaka mingi, mmoja wa wachungaji hao, alisema walitarajia uamuzi kama huo kuja kutokea kutokana na mambo mengine na kitendo cha kutosomwa waraka katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

“Nafasi hii aliyopewa ni vizuri akaomba msamaha ili arudi kwenye mstari, akiamua kuacha kuomba msamaha dayosisi ifanye uamuzi wake, atachafuka zaidi, dayosisi kama dayosisi hatuwezi kukubali kutokuwa na mwakilishi,” alisema mchungaji mwingine aliyezungumza na gazeti hili.

Mchungaji mwingine alisema uamuzi wa Baraza la Maaskofu kumtenga Askofu Malasusa hauwezi kulitikisa kanisa isipokuwa litazidi kuwa imara zaidi.

Gazeti la MTANZANIA Jumamosi la jana, liliripoti taarifa za ndani ya vikao hivyo viwili, kile cha Baraza la Maaskofu na kile cha Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo kuhusu uamuzi wa kudaiwa kutengwa kwa Askofu Malasusa kwa tuhuma za kusaliti waraka, likiona jambo hilo kama hujuma na uchonganishi kati ya kanisa hilo na watu walio nje.

Taarifa hizo zilidai wakati Waraka wa Pasaka unaandaliwa, Askofu Malasusa hakuwapo, lakini alipigiwa simu kutaarifiwa na inaelezwa alitoa baraka, lakini ulipotoka anadaiwa kuagiza usisomwe.

Inadaiwa katika kikao hicho, Askofu Malasusa, alipewa nafasi ya kujitetea na katika maelezo yake alisema aliona tayari waraka huo umesambaa vya kutosha kwenye mitandao ya kijamii.

Inaelezwa alipoulizwa kuhusu ujumbe anaotuhumiwa kuagiza utumwe kwa wachungaji ukiwakataza kuusoma waraka huo, Askofu Malasusa, alijibu si wake na kutaka aulizwe aliyeutuma.

Pamoja na Askofu Malasusa kutoa maelezo hayo, inadaiwa baadhi ya wachungaji wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ndio waliopeleka kwenye Baraza la Maaskofu vielelezo vya barua, wakiwa wamezisaini na kuthibitisha walipewa maelekezo ya kutousoma waraka huo.

Inadaiwa hoja hizo za Askofu Malasusa hazikuliridhisha Baraza la Maaskofu na hivyo kutangaza kumtenga na masuala yote yanayohusu baraza hilo.

Zaidi inaelezwa kwa sasa ameondolewa kwenye kamati zote alizokuwa akiziongoza na haruhusiwi kuliwakilisha kanisa hilo mahali popote.

Juzi gazeti la MTANZANIA liliwasiliana kwa simu na Askofu Malasusa ili kufahamu ameupokeaje uamuzi huo, lakini alimtaka mwandishi wetu kuwasiliana kwa namba ya ofisini kwake na si yake binafsi.

Mwandishi alipomweleza namba hiyo imekuwa ni vigumu kumpata, alisema muda huo wakati akipigiwa simu, saa sita mchana, alikuwa kwenye kikao na kisha akakata simu.

Jana pia gazeti hili lilimtafuta kwa mara nyingine, lakini hakupatikana.

MAASKOFU WENGINE WAWILI WAGUSWA

Uamuzi huo wa Baraza la Maaskofu wa KKKT, pia unaelezwa kuwagusa kwa namna nyingine maaskofu wengine wawili wa kanisa hilo.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata, zinaeleza uamuzi dhidi ya maaskofu hao ulichukuliwa sambamba na ule wa Askofu Malasusa.

Taarifa nyingine mpya zaidi zinaeleza Askofu wa Dayosisi ya Kusini na Mashariki, Lukas Mbedule na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomoni Massangwa, wamepewa sharti la kuomba radhi na kuwa ndani ya dayosisi zao.

“Kuna dayosisi hazikusoma waraka wa Pasaka, Halmashauri Kuu ya Kanisa haijaridhishwa na hawa maaskofu wawili, hawajatengwa bali nao wamepewa kazi ya kufanya, ambayo ni kuomba msamaha na wawe ndani ya dayosisi zao,” kilieleza chanzo cha gazeti hili toka ndani ya kanisa hilo.

MTANZANIA Jumapili jana liliwasiliana na Askofu Mbedule kupitia simu yake ya kiganjani na kumuuliza kuhusu uamuzi huo. Alisema jambo hilo wamekwishalimaliza kwenye vikao vyao.

Alipoulizwa iwapo kama wamelimaliza jambo hilo kwa kuomba msamaha, Askofu Mbedule alisisitiza: “Tumekwishalimaliza jambo hilo, taarifa atatoa mkuu wa kanisa ambaye ndiye msemaji wa kanisa.”

Askofu Mbedule alipotakiwa na gazeti hili kueleza zaidi kile kilichotokea hadi kudaiwa kuchukuliwa hatua na Baraza la Maaskofu, aliendelea kusisitiza pasipo kufafanua zaidi kwamba wamekwishamaliza vikao.

Kwa upande wake, Askofu Massangwa, alipoulizwa kuhusu jina lake kutajwa katika uamuzi huo, alisema hafahamu jambo hilo.

Alipoulizwa iwapo katika dayosisi anayoiongoza waraka wa Pasaka ulisomwa, alisema hata yeye aliusoma kwenye mitandao.

MTANZANIA Jumapili lilipomuuliza iwapo waraka huo ulisomwa katika Usharika wa Mjini Kati ambako mara nyingi husali hapo, Askofu Massangwa alijibu: “Hata mimi sijui kama ulisomwa,” kisha akakata simu. Gazeti hili linafahamu kuwa wakati wa Sikukuu ya Pasaka waraka huo haukusomwa katika kanisa hilo.

MTANZANIA Jumapili, jana pia liliwasiliana na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Asa Shoo, ili kuzungumzia jambo hilo, lakini alisisitiza anayepaswa kulizungumzia si yeye bali ni Katibu Mkuu wa KKKT, aliyemtaja kwa jina la Brighton Killewa.

Alipoambiwa kwamba Killewa alikwishazungumza na MTANZANIA Jumamosi na kumwelekeza mwandishi awasiliane na kiongozi wa kanisa hilo, Askofu Dk. Shoo, Katibu Mkuu huyo, alisisitiza jambo hilo lipo chini ya viongozi hao.

Gazeti hili lilipomwambia linazo taarifa kwamba uamuzi huo ulifikishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ambacho wajumbe wake ni pamoja na yeye, alijibu: “Ni kweli lililetwa kwa ufupi sana.”

Alipotakiwa kueleza kuhusu huo ufupi, Asa alikataa na kusisitiza yeye si msemaji na kutaka atafutwe Killewa au Askofu Dk. Shoo.

Juzi na hata jana juhudi za MTANZANIA Jumamosi na MTANZANIA Jumapili kumtafuta Askofu Dk. Shoo kupitia simu yake ya kiganjani na hata ofisini kwake mjini Moshi hazikuzaa matunda.

Waraka huo wa Pasaka ambao unadaiwa kuwa kiini cha mashtaka dhidi ya viongozi hao wa kiroho, ni ule uliotolewa na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo, mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, wiki moja kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.

Pamoja na mambo mengine, waraka huo uligusa na kuonya mwenendo wa masuala ya uchumi, siasa na kijamii, uliamsha mjadala mkali ndani ya jamii, viongozi wa Serikali na kisiasa na hata kumwibua Rais Dk. John Magufuli.

Mijadala na malumbano na pengine iliyoonekana kuchagiza kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali kuhusu waraka huo, iliwafanya baadhi kukumbuka waraka uliotolewa mwanzo na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Februari 9, mwaka huu, ukiwa ni ujumbe wa Kwaresma chini ya kaulimbiu “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu: Mt.28:19.”

Ni waraka huo na ule uliokuja baadaye wa maaskofu 27 wa KKKT, ndio uliotajwa na pengine kujenga hisia kwa baadhi kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, alilitumia kongamano la vijana lililofanyika Bagamoyo katika wiki hiyo hiyo ya kuelekea Pasaka kuupinga, akisema viongozi wa dini hawapaswi kuchanganya siasa na kazi yao ya kitume.

Siku moja baadaye, baada ya waraka huo wa KKKT kutolewa, Rais Magufuli, katika hafla ya uzinduzi wa magari 181 ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD), aliwaomba maaskofu na viongozi wengine wa dini kuhubiri ujenzi wa viwanda vya dawa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika andiko lake lililosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, alitumia mafumbo na mifano mingi kuchambua yale yaliyoandikwa kwenye waraka huo.

Waraka huo wa KKKT ulioandaliwa na maaskofu 27 akiwamo Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Fredrick Shoo, ulichambua masuala ya jamii, uchumi, maisha ya siasa, umuhimu wa katiba mpya na matukio yaliyo kinyume na kile walichokiita tunu na misingi ya taifa.

Katika eneo la uchumi, waraka huo ulionya kile ilichokiona kuwako kwa dhana ya Serikali kutaka kushindana na wadau wa maendeleo, lakini pia mfumo usio sahihi wa ukusanyaji kodi na ambao unafilisi wafanyabiashara.

Kuhusu siasa, waraka huo ulikumbusha misingi ya siasa safi na uongozi bora na kuonya Serikali kuminya demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa Bunge na vyombo vinavyotoa na kusimamia haki kama Mahakama na Tume ya Uchaguzi.

Zaidi ulizungumzia dhana ya kile kinachodhaniwa baadhi ya wanasiasa kununuliwa na gharama za kurudia uchaguzi, huku katika suala la ajira kwa vijana ukitaka jitihada za wazi zifanyike na kuonya elimu kuchokonolewa.

Waraka huo ulishauri suluhisho la yote hayo ni kupatikana kwa Katiba Mpya ambayo ina maoni ya wananchi na kupendekeza suala hilo lifanyike kabla ya uchaguzi wa mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles