Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freemon Mbowe, hajanyang’anywa gari bali dereva aliyekuwa akiliendesha amestaafu, hivyo inahitajika dereva mwingine.
Ndugai alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), aliouomba wiki iliyopita.
Waitara katika mwongozo wake kwa Spika, alitaka kujua sababu za Mbowe kupokwa gari na watumishi waliokuwa wakisadia kambi hiyo kuandaa hotuba kuondolewa.
Mbunge huyo alisema kambi hiyo imepata usumbufu kwa kushindwa kuandaa hotuba na kusababisha kutowasilisha hotuba mbadala za bajeti bungeni.
“Naomba mwongozo wako Spika utueleze masuala haya au kambi imefutwa bungeni?” alihoji Waitara.
Akijibu mwongozo huo jana, Spika Ndugai alisema gari la kiongozi huyo lipo, lakini dereva aliyekuwa akiliendesha alikwishastaafu na kwamba kinachohitajika ni dereva mwingine.
Alisema dereva huyo alistaafu siku nyingi, lakini alikuwa anafanya kazi kwa mkataba takriban miaka minane, hivyo wameona ni vyema sasa akapumzika.
“Kuna mambo ya ndani ambayo si vizuri kila kitu kijadiliwe hapa, huyu dereva alistaafu wakati mzee Sitta (marehemu Samuel Sitta) akiwa Spika, alipewa mkataba wa mwaka mmoja na aliendelea kupewa mkataba wa miaka mitano katika kipindi cha uongozi wa Spika Anne Makinda na pia kwa sasa akapewa tena,” alifafanua.
Spika alisema dereva huyo pia alipewa mkataba wa miaka miwili katika uongozi wake, hivyo sasa hajaongezewa ili apumzike.
“Hakuna sababu ya kuwepo malumbano, hivyo dereva huyo anapaswa kupumzika, lakini kama atafanya kazi kwa mkataba wa mtu binafsi, hiyo ni suala lingine, kwa sasa lazima apatikane dereva mwingine na madereva wapo,” alisema.
Kuhusu watumishi, Spika Ndugai alisema Bunge linaangalia upya utaratibu gani unaopaswa kutumika kuhusu watumishi hao.
“Kambi mbili za Bunge ambazo ni za chama tawala (CCM) na upinzani zimekuwa na watumishi wanaowahudumia ambapo CCM ina watumishi watano ambao wanaletwa kutoka CCM,” alisema.
Kwa upande wa kambi ya upinzani, Ndugai alisema ilikuwa na watumishi wanne ambao pia walipewa mkataba wa muda ambao umekwisha.
Hata hivyo, alisema anadhani kwa sasa watumishi wa aina hiyo wasiwepo, kwahiyo hata wale wa CCM nao wameshafungashiwa virago.
Alisema kuendelea kugoma kuleta hotuba kwa kigezo cha hakuna wanaoweza kuwaandikia kunashusha hadhi ya wabunge.
“Naamini tunaweza kuandika hotuba zetu na kama kuna hoja za misingi kwamba lazima hotuba hizi wabunge wa upinzani waandikiwe, jambo hilo linaweza kuzungumzwa kwenye vikao vyetu huko,” alisema.
Baada ya majibu hayo, Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF), alisimama na kuomba mwongozo kwa Spika kuhusu uamuzi huo akitaka kujua mabunge ya nchi zipi yamekuwa na utaratibu huo au uamuzi huo ndio wa kwanza kufanyika nchini.
Naye, Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alisimama pia kuomba mwongozo akisema anaheshimu uamuzi wa Spika, lakini kambi hiyo inashindwa kuandika hotuba kwa kuwa zinazoandikwa na Serikali zinaandikwa na wataalamu kwa kipindi kisichopungua miezi sita.
“Hotuba haziandikwi na mawaziri, sisi kambi wale watumishi wanne wapo kikanuni na wanafanya kazi kwa niaba ya kambi nzima, tuoneeni huruma kwenye hili jambo,” alisema.
Akijibu, Spika Ndugai, alisisitiza kama kuna hoja za msingi bado jambo hilo linazungumzika.
“Hili ni eneo ambalo bado tunalitazama na tutalitazama zaidi kwenye vikao vyetu vya kamati, lakini hoja za kuchapa kuna ma-sekretari wa Bunge, wapo muda wote na vifaa vipo,” alisema.