NA MWANDISHI WETU
BODI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (TPLB) imehusishwa kwenye uvurundaji wa utoaji wa tuzo kwa waliofanya vizuri msimu uliopita wa ligi hiyo.
Kampuni ya Vodacom Tanzania ilifanya hafla ya utoaji wa tuzo hizo Alhamisi iliyopita jioni baada ya zoezi hilo mijadala mikubwa imeibuka kwenye vijiwe vya soka kutokana na baadhi ya waliopewa tuzo kutokidhi vigezo.
Habari za uhakika zilizolifikia MTANZANIA jana zimedai kuwa baadhi ya wajumbe wa bodi ya ligi, walitaka kulinda maslahi ya timu zao na kuamua kupeleka baadhi ya tuzo kwenye timu wanazotokea.
“Kuna baadhi ya timu zina uwakilishi kwenye bodi ya ligi, nao wamechangia kubebwa kwa baadhi ya watu kwenye baadhi ya vipengele vya tuzo na hii ni kutaka kulipa fadhila kwa timu zao,” alisema mtoa habari wetu kutoka ndani ya bodi hiyo aliyekataa kuandikwa jina gazetini.
Aliongeza kuwa: “Viongozi wa hapa kusimamia maslahi ya timu zao, hili jambo limekuwa likitukwamisha sana na ndio limechangia kwa kiasi kikubwa ligi kutokwenda vizuri msimu uliopita, ni ngumu ligi yetu kuwa bora kama haya mambo yakiendelea.”
Gazeti hili lilifanya jitihada ya kuwatafuta viongozi wa TPLB ili kujua ukweli wa jambo hilo, tulifanikiwa kumpata Mwenyekiti wa bodi hiyo, Hamad Yahaya, ambaye alipinga na kudai kuwa watalirekebisha suala hilo kwa msimu ujao.
“Hizi tuzo hatukuchagua sisi wenyewe, sisi tulikuwa ni waandaaji tu, tuliwashirikisha viongozi wa mpira, makocha, viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na mwisho sisi ndio tuliofanya mchujo hadi kuwapata hao washindi, hivyo sidhani kama madai hayo ni ya ukweli,” alisema.
Hata hivyo, katika kuziboresha zaidi tuzo hizo, Yahaya amesema wataunda jopo maalumu litakalohusisha makocha, waandishi wa habari na viongozi ili kujadili mfumo mzuri wa kuwapata washindi kwa msimu ujao.
“Tumepata funzo kwenye hilo, tunajua watu wengi wanalalamika lakini kwa kutumia jopo hilo naamini msimu ujao tutakuja na njia nzuri ya kupata washindi,” alisema.
Baadhi ya tuzo zilizolalamikiwa ni ile ya Kocha Bora aliyopewa aliyekuwa kocha wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata, (sasa Kagera Sugar), wadau wengi wamehoji vigezo gani vilivyotumika kumpa tuzo kocha huyo aliyeiongoza Prisons kwenye mechi nane za mwisho, huku Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, akinyimwa baada ya kuiongoza timu hiyo kuwa mabingwa wa ligi.
Lakini kwa mujibu wa historia za tuzo hizo, zinaonyesha kuwa hakuna kocha wa kigeni aliyeweza kuitwaa tokea zianzishwe huku ikidaiwa ni kutokana na wao kutotambulika kwenye Chama cha Makocha wa Soka Tanzania (TAFCA), ambao nao huhusishwa kuchagua kocha bora wa msimu.
Tuzo nyingine zilizolalamikiwa ni zile za timu bora yenye nidhamu iliyokwenda kwa Mtibwa Sugar, pamoja na ile ya kipa bora wa msimu aliyopewa aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Shaaban Kado, aliyewabwaga Said Mohamed (Mtibwa Sugar) na Mohamed Yusuph (Tanzania Prisons).
Kwenye usiku huo wa tuzo, winga wa Yanga, Simon Msuva aling’ara vilivyo baada ya kuzoa tuzo mbili ya ufungaji bora na ile ya mchezaji bora wa msimu aliyochukua kwa kuwabwaga.