JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
MAHAKAMA Kuu yaAfrika Kusini imetoa amri ya muda ya kumzuia Rais wa Sudan, Omar al Bashir anayehudhuria kikao kilichoanza jana cha viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) kutoondoka nchini humo.
Mahakama hiyo imemuagiza al-Bashir abakie hadi leo wakati itakaposikiliza kesi inayoitaka iiamrishe Serikali ya Afrika Kusini kumkamata kiongozi huyo i akajibu mashitaka yanayomkabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ya mjini Hague, Uholanzi.
Mapema jana, Rais Bashir alikaribishwa na maofisa wa Afrika Kusini wakati akiwasili mjini Johannesburg.
Licha ya a mahakama kutangaza uamuzi huo, kiongozi huyo wa Sudan alipiga picha ya pamoja na viongozi wengine wa Afrika akiwa amevalia suti ya bluu, tai na akitabasamu wakati picha ikichukuliwa.
Rais al Bashir anasakwa na mahakama hiyo kwa uhalifu wa vita na mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.
AU inakutana chini ya uenyekiti wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe katika mkutano unaoonekana kughubikwa na mzozo wa Burundi na migogoro ya uhamiaji, ugaidi na mihula mitatu ya urais.
AU imekuwa ikikiuka maombi kadhaa ya kuitaka imkamate al- Bashir tangu amri hiyo mkamata ilipotolewa mwaka 2009.
Hali hiyo imezusha mvutano baina ya ICC na AU huku baadhi barani Afrika wakiituhumu mahakama hiyo kuwa chombo cha kuwalenga Waafrika tu.
Hata kabla ya matukio ya jana, AU imekuwa ikiitaka ICC iache kuwaandama marais walio madarakani na kwamba haitalazimisha wanachama wake kumkamata kiongozi yeyote kwa niaba ya mahakama hiyo.
Chama tawala cha African National Congress (ANC), kilisema Serikali ya Afrika Kusini ilitoa msamaha ‘kwa washiriki wote wa mkutano wa wa AU kama sehemu ya taratibu za kimataifa kwa nchi wenyeji wakati wa mikusanyiko ya AU au hata Umoja wa Mataifa (UN).
“Ni katika msingi huu, pamoja na mambo mengine ANC inatoa mwito kwa Serikali ya Afrika Kusini kupinga agizo hilo lililoletwa kuilazimisha kumkamata Rais al-Bashir,” taarifa ya ANC ilisema na kuongeza kuwa mataifa ya Afrika na Ulaya Mashariki yanaendelea kukandamizwa kwa kulengwa isivyo halali na uamuzi wa ICC.
Lakini kwenye taarifa yake , ICC ilisema kuwa waranti mbili za kumkamata Bashir bado zipo. Mwendesha Mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda amesema Afrika Kusini ina wajibu wa kumkamata al-Bashir na kumkabidhi kwa mahakama hiyo.
Ofisi yake imekuwa ikiwasiliana na mamlaka za Afrika Kusini tangu iliporipotiwa kuwa rais huyo wa Sudan atazuru nchi hiyo kuhudhuria mkutano wa AU.
Iwapo al-Bashir hatakamatwa, suala hilo litawasilishwa kwa mkutano wa mataifa wanachama wa mahakama hiyo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo liliiwasilisha kesi hiyo ICC mwaka 2005, alisema.
Al-Bashir, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1989, anatuhumiwa kutenda uhalifu ambao pamoja na mambo mengine umeshuhudia vifo vya watu 300,000 na wengine milioni mbili kukimbia makazi yao.
Hati za kumkamata Bashir, ambaye amekana tuhuma zinazomkabili, zimemfanya anatembelea nchi chache duniani, hasa mataifa rafiki ya Afrika na Mashariki ya Kati.