Na JANETH MUSHI-ARUMERU
HALMASHAURI ya Wilaya ya Arusha Vijijini, Mkoa wa Arusha, imeagizwa kuweka mikakati ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ilkorot kabla ya mwisho wa mwaka huu ili kuwapunguzia wananchi kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo, alipokuwa akikagua ujenzi unaoendelea wa kituo hicho kilichopo Kata ya Olkokola, wilayani hapa.
Waziri Jafo alisema halmashauri hiyo ina wajibu wa kuweka mpango wa kuhakikisha wanatafuta fedha kwa ajili ya kumalizia kituo hicho kabla ya mwisho wa mwaka huu kwa kuwa kinajengwa kwa fedha za wananchi.
Katika maelezo yake, Jafo alisema halmashauri hiyo inapaswa kuunga mkono juhudi za wananchi za kuboresha sekta ya afya ili kuwaondolea kero ya kufuata huduma hiyo maeneo ya mbali.
“Halmashauri hakikisheni mnatafuta fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hao kumalizia ujenzi wa kituo hiki. Binafsi nimefarijika kuona wananchi mnahamasishana hadi mnajenga kituo cha afya, huu ni mfano wa kuigwa na maeneo mengine nchini.
“Hadi sasa kuna vituo vya afya 535 ambavyo vinafanya kazi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na jitihada za wananchi za kujenga vituo vya afya katika maeneo yao zitasaidia kusogeza huduma karibu na watu.
“Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, Serikali itahakikisha upatikanaji wa dawa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya ni wa uhakika pamoja na ukarabati wa vituo vingine,” alisema