Na TUNU NASSOR,DAR ES SALAAM
SERIKALI imezitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinaweka miundombinu rafiki katika maeneo ya taasisi zake hususan shuleni ili kuwalinda wanafunzi na ajali za barabarani.
Akizungumza katika uzinduzi wa programu ya usalama barabarani kwa shule za msingi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema kuna haja ya kuboresha Miundombinu hasa maeneo wanayopita wanafunzi ili waweze kutembea kwa usalama.
Alisema wanafunzi wanapaswa kufikia malengo yao na asiwepo mtu wa kukwamisha kwa njia yoyote, ikiwamo ajali za barabarani.
“Niziombe halmashauri zetu wanapojenga miundombinu ta taasisi kama shule wahakikishe wanaweka njia salama kwa wanafunzi,” alisema Jenista.
Alizitaka halmashauri kujifunza kutoka kwa taasisi ya Amend ambao wanaboresha miundombinu kwa wanafunzi.
“Barabara ambazo zinapita katika taasisi hasa shule ambazo watoto wanasoma, zizingatie kutengeneza mapito salama kwa watoto wetu waweze kutembea salama,” alisema Jenista.
Alitoa shukrani kwa wafadhili wa programu hiyo taasisi za Amend, Puma Energy na Fia na kuwataka wapeleke huduma hiyo katika mikoa mingine nchini.
“Halmashauri zetu zijifunze kutoka kwa Taasisi ya Amend, Puma na FIA ambazo zimetuonesha mfano mzuri wa kurekebisha miundombinu,” alisema Jenista.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa shirika la Amend, Tom Bishop aliitaka serikali kurekebisha sheria ya usalama barabarani ili vyombo vyote vya moto vipite katika maeneo ya shule kwa mwendo wa Kilomita 30 kwa saa badala ya 50.
Alisema kwa kufanya hivyo kutapunguza ajali zinazoepukika hasa kwa wanafunzi.
“Ifikie wakati mwendo wa magari katika maeneo karibu na shule iwe ni KM 30 kwa saa na si 50 ili kupunguza ajali ambazo zinaepukika.
Naye Meneja Mkuu wa Puma, Philippe Corsaletti alisema licha ya kuwa ni wafanyabiashara wa mafuta lakini pia wanawajibu wa kuhakikisha usalama barabarani hasa kwa wanafunzi.